Viongozi wa nchi za kiislamu wameanza mkutano wao wa
siku mbili katika mji wa Istanbul nchini Uturuki. Pamoja na masuala mengine
viongozi hao watajadili migogoro ya Syria, Yemen na pia njia za kukabiliana na
ugaidi.
Wakuu wa serikali na viongozi wa nchi zaidi ya 30
kutoka shirika la ushirikiano la nchi za kiislamu, OIC , wanaanza mkutano wa
kilele wenye lengo la kuziondoa tofauti baina ya nchi za kiislamu.
Mazungumzo ya viongozi hao pia watajadili masuala ya
Palestina,Libya na Nargono Karabakh.
Mwenyeji wa mkutano huo, Uturuki imesema inakusudia
kuitumia fursa ya mkutano huo ili kujaribu kupunguza tofauti zilizopo miongoni
mwa Waislamu wanaokadiriwa kufikia Bilioni 1.7 duniani.
Yemen na Syria kugubika mazungumzo
Hata hivyo wachunguzi wanaamini migogoro ya Syria na
Yemen inaweza kuyagubika mazungumzo yanayofanyika chini ya uenyekiti wa Rais
Tayyip Erdogan. Miongoni mwa viongozi muhimu wanaohudhuria mkutano huo wa
kilele mjini Istanbul ni Mfalme wa Saudi Arabia, Salman na Rais wa Iran Hassan
Rouhani.
Saudi Arabia na Iran zinatafautiana juu ya migogoro
ya Syria na Yemen. Rais wa Iran Rouhani aliewasili jana mjini Istanbul pia
anatarajiwa kufanya mazungumzo na wenyeji wake wa Uturuki.
Hata hivyo wakati mkutano huo ni muhimu viongozi
wenye uzito wa juu kama Mfalme wa Jordan Abdullah na Rais wa Misri Abdel Fattah
al-Sisi hawatakuwapo. Uhusiano baina ya Uturuki na Misri bado haujarejea katika
hali nzuri tangu kuondolewa madarakani kwa aliekuwa Rais wa Misri Mohammed
Mursi mnamo mwaka 2013. Mursi alikuwa mshirika mkubwa wa Uturuki.
Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki, Mevlut Cavusoglu
amesema mkutano wa mjini Istanbul unafanyika wakati ambapo jumuiya ya nchi za
kiislamu inakabiliwa na migogoro mingi.
Waziri Cavusoglu amesema umwagikaji damu miongoni
mwa ndugu katika nchi za kiislamu ni jambo linalosababisha machungu.Hata hivyo
Waziri huyo ameelezea matumaini kwamba mkutano wa viongozi wa nchi 57 za
kiislamu-OIC, unaoendelea mjini Istanbul utatoa mchango katika juhudi za
kuondosha uhasama.
Kabla ya mkutano kuanza, Mfalme wa Saudi Arabia
Salman alifanya ziara iliofungua ukurasa mpya katika uhusiano baina ya Saudi
Arabia na Uturuki.Rais Erdogan alimlaki Mfalme huyo kwenye uwanja wa ndege wa
Esenboga.
Katika ishara ya kuimarika kwa uhusiano baina ya
nchi hizo mbili, Rais Erdogan alimtunukia Mfalme Salman medali ya heshima ya
juu ya nchini Uturuki. Uturuki na Saudi Arabia zinakubaliana kwamba mgogoro wa
Syria utaweza kutatuliwa ikiwa Rais Bashar al-Assad ataondoka madarakani.
Uturuki na Saudi Arabia pia zinawaunga mkono waasi wanaopambana na utawala wa
Assad.
0 comments:
Post a Comment