MKATABA tata wa Kampuni ya Lugumi Enterprises
uliosababisha kashfa ya ufisadi wa mabilioni ya fedha katika Jeshi la Polisi,
leo unatarajiwa kuwasilishwa mbele ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali
(PAC).
Mkataba huo huwenda ukawasilishwa na Mkuu wa Jeshi
la Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu, ili kutoa fursa kwa wajumbe wa kamati
hiyo kuupitia kipengele kwa kipengele kabla ya viongozi wa jeshi hilo kuanza
kuhojiwa juu ya ufisadi huo.
Kupitia mkataba huo wa 2011, Kampuni ya Lugumi
Enterprises ilipewa tenda ya kufunga mashine za kuchukua alama za vidole katika
vituo vya polisi 108 nchini kwa gharama ya Sh bilioni 37.
Tayari kampuni hiyo imekwishalipwa Sh bilioni 34
sawa na asilimia 99 ya fedha zote, huku ikiwa imefunga mashine katika vituo 14
tu katika jiji la Dar es Salaam ambavyo pia havijulikani vipo maeneo gani.
Uwasilishwaji wa mkataba huo ni utekelezaji wa agizo
la PAC, ambapo Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Aeshi Hilaly alitoa siku sita
kwa Jeshi la Polisi kuwasilisha mkataba huo.
Akizungumza Aeshi alisema baada ya kamati yake
kupokea mkataba huo wajumbe wataupitia na kuujadili kwa kina ili kuona kama
kuna upungufu.
“Kesho (leo) ndiyo tarehe 11, tutapokea mkataba kama tulivyowaomba watuletee,
wakituletea tutausoma na kuujadili kwa kina kisha tutawaapa maelekezo,” alisema
Aeshi.
Alisema iwapo kamati yake haitaridhishwa na maelezo
ya viongozi wa Jeshi la Polisi kuhusu mkataba na fedha zilizotumika, upo
uwezekano mkubwa wa kuundwa kwa kamati maalumu.
“Kama vifaa vimefungwa katika vituo vyote, ni
matumaini yetu vitakuwa vinafanya kazi, huwezi kufunga vifaa ambavyo ni
vibovu…kama maelezo tutakayoyapokea hayataridhisha kuna uwezekano wa kuundwa
kwa kamati ya uchunguzi,” alisema Aeshi.
Hivi karibuni Kamati ya PAC ilibaini kuwapo kwa
viashiria vya ufisadi katika Jeshi la Polisi kwa kuwaeleza waandishi wa habari
kuwa Kampuni ya Lugumi ililipwa Sh bilioni 34 kati ya Sh bilioni 37 za mkataba
wote.
0 comments:
Post a Comment