NIKIWA binti mdogo wakati nasoma shule ya msingi
miaka ya 1980, nilizoea kusikia na kuimba wimbo mmoja ambao niliupenda sana
mpangilio wake wa ala za muziki, na sauti zilizokuwa zikisikika. Huu si wimbo
mwingine, bali ni wimbo ambao ulihusu alama kubwa sana ya Taifa letu: Mwenge wa
Uhuru.
Wimbo ulikwenda namna hii: “Sisi tumekwisha uwasha
Mwenge, tumekwisha uwasha Mwenge. Na kuuweka juu ya mlima, Mlima Kilimanjaro.
Kuwasha Mwenge, Kuwasha Mwenge na kuuweka Kilimanjaro; Kuwasha Mwenge, Kuwasha Mwenge
na kuuweka Kilimanjaro.”
Naam. Niliupenda mahadhi yake na nakumbuka hata
tukiwa sekondari, tulitakiwa kuchangia shilingi tano za mafuta ya taa kwa ajili
ya Mwenge huo. Tulijivunia Mwenge huu na tuliaminishwa pia kwamba una maana
kubwa sana kwa Taifa letu.
Siku za hivi karibuni, hata hivyo, Watanzania wengi
wanaonekana wameuchoka Mwenge. Imefikia hatua kwamba picha zinasambazwa kwenye
mitandao ya kijamii zikionyesha Mwenge wa Uhuru na chini yake kukiwa na maneno:
Mtumishi hewa namba moja. Picha hiyo imesambazwa sana na kuendelea kusambazwa
kwake kunaweza kutafsiriwa kwamba watu wengi wanakubaliana na kauli hiyo ya
kuwa kweli alama hii ya Taifa ni mtumishi hewa namba moja.
Wapo pia, nikiwamo mimi, ambao tulidhani kwamba
baada ya Rais John Magufuli kuingia madarakani, basi angeufutilia mbali Mwenge,
kwa maana ya kufuta kabisa hizi mbio za Mwenge ambazo zimekuwa zikifanyika kila
mwaka. Huenda wengi wetu tulifikiri hivi kutokana na sababu mbalimbali ambazo zinasababisha
tudhani kwamba Mwenge huu wa Uhuru hauna faida.
Bahati nzuri, niliposikia kwamba Mwenge haujafutwa,
bado upo na utaendelea kukimbizwa mwaka huu, nikaamua kujiuliza maswali kadhaa.
Kwanini hasa mbio hizi za Mwenge wa Uhuru hazijafutwa?
Kwa kuanzia, naomba nitofautishe vitu viwili hapa:
Kuna Mwenge wa Uhuru, halafu kuna Mbio za Mwenge wa Uhuru. Ni mambo mawili
tofauti. Ili kuelewa tofauti ya mambo haya mawili, nadhani inatupasa kurudi
kwenye historia.
Kwa ninavyoelewa, Mwenge wa Uhuru ulianza Disemba 9,
1961, siku ya Uhuru wa Tanganyika. Wakati bendera ya Malkia wa Uingereza
ikishushwa Uwanja wa Taifa, bendera ya Tanganyika ilipandishwa, sambamba na
Mwenge wa uhuru kuwashwa juu ya kilele cha Mlima Kilimanjaro. Hiyo
inadhihirisha kwamba Mwenge wa Uhuru una maana kubwa sana kwa uhuru wa nchi
hii.
Kwa mujibu wa tovuti ya Serikali ya Tanzania, Mwenge
wa Uhuru huzunguka nchi nzima ukiwa na ujumbe wa matumaini, upendo, heshima na
amani. Mwenge huo huanzia katika mkoa wowote utakaochaguliwa kila mwaka na mbio
hizo hufika tamati Oktoba 14, siku ambayo Taifa huadhimisha kumbukumbu ya kifo
cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Vilevile, tovuti ya
Serikali inaongeza kwamba Mwenge huwa na ujumbe tofauti kila mwaka, kulingana
na vipaumbele vya maendeleo vya mwaka husika.
Historia pia inatueleza kwamba siku Mwenge wa Uhuru
ulipokuwa ukiwashwa juu ya Mlima Kilimanjaro kwa mara ya kwanza, Mwalimu
Nyerere alisema maneno yafuatayo: “Tunataka kuwasha Mwenge na kuuweka juu ya
Mlima Kilimanjaro, umulike hata nje ya mipaka yetu; ulete tumaini pale ambapo
hakuna matumaini; upendo mahali palipo na chuki na heshima palipojaa dharau.”
Mwenge huo uliwekwa kwenye kilele cha Mlima
Kilimanjaro na Luteni Kanali, Alexander Nyirenda. Mwalimu Nyerere alisisitiza
kwamba Mwenge una umuhimu mkubwa katika kuijenga Tanzania yenye umoja, upendo
na mshikamano miongoni mwa watu wote.
Hiyo ilikuwa Disemba 9, 1961 na tangu mimi
nilipokuwa na ufahamu wa kuweza kuwaza mwenyewe, nimekuwa nikisikia kila mwaka
kukiwa na mbio za Mwenge. Nadhani lengo lake ni kujikumbusha kuhusu wajibu wetu
kama wananchi kuwa na umoja, mshikamano, upendo na amani.
Leo hii, mwaka 2016, wananchi wengi sana wanaonekana
hawana imani na mbio za Mwenge. Wana sababu zao za msingi kabisa, ambazo
pengine zingefaa kuangaliwa. Sababu moja kubwa ni kwamba mbio za Mwenge
zinamaliza tu hela kutokana na Mwenge huo kuwashwa kwa mafuta ya taa. Hela
inayotumika kuzunguka nchi nzima ni kubwa sana, pamoja na posho na usafiri kwa
wale wakimbiza Mwenge wote.
Sambamba na hilo, ni ukweli usiofichika kwamba
Mwenge ukilala kwenye eneo fulani, basi eneo hilo usiku huo kutakuwa na kucheza
ngoma usiku kucha, pamoja na vitendo vya wazi kabisa vya zinaa. Ukiwauliza
wahudhuriaji, watakueleza kwamba ifikapo asubuhi, kondomu zilizotumika huokotwa
kwa wingi na zinaweza kujaza ndoo kadhaa. Ikumbukwe kwamba hizo ni
zilizotumika. Kuna uwezekano mkubwa kwamba wapo watu ambao hata hawakutumia
kabisa kondomu. Ni alama mbaya sana, kwani mbio za Mwenge wakati mwingine
hutumika kama upenyo wa kufanya zinaa isiyo salama.
Lakini vilevile, swali lingine ambalo watu wengi
wamekuwa wakijiuliza, ni: Hivi kweli wananchi wanafahamu maana na umuhimu wa
Mwenge? Sisi tuliokwenda shule miaka ya 80 na 90, kabla ya kurejeshwa kwa mfumo
wa vyama vingi vya siasa, tulikuwa tukielezwa sana kuhusu Mwenge na kulazimika
kuchangia. Lakini, watoto wetu wanaosoma sasa hivi wanaelewa chochote?
Wanafahamu kuhusu historia ya Mwenge na Nyirenda kuuwasha juu ya Mlima
Kilimanjaro? Wanajua kuhusu kauli ya amani, upendo, mshikamano na matumaini
iliyotolewa na Baba wa Taifa? Wanamfahamu hata huyo Baba wa Taifa na umuhimu wa
kuuzima Mwenge Oktoba 14?
Haya ni maswali ambayo nadhani ofisi husika
inatakiwa kuyapatia si tu majibu, bali kuyafanyia mkakati ili Taifa lielewe maana
ya Mwenge na umuhimu wake.
Hivi, watu wanajua kwamba Mwenge ni alama ya Taifa,
na kwamba upo kwenye ngao ile ijulikanayo kama ‘Bibi na Bwana?’ Watu wanaelewa
kwamba Mwenge ukifutwa, maana yake ni kwamba unakuwa umefuta historia ya nchi
na huenda hata ile ngao ya Taifa itabidi ibadilishwe kwa kuwa imebeba alama za
Taifa?
Kila siku nasema, kwanini hatuwi wabunifu? Kwani ni
lazima kuukimbiza Mwenge kila mkoa, wilaya na kata kila mwaka? Hakuna njia
nyingine mbadala ya kuelimisha watu juu ya Mwenge na maana yake kwa Taifa?
Hakuna ubunifu wowote wa kusaidia hata watoto wetu kujua kuna kitu kinaitwa
Mwenge wa Uhuru na umuhimu wake kwa Taifa? Ni lazima kukimbia tu kila mwaka?
Yaani yale yaliyofanywa miaka ya 70 yaendelee kufanywa hadi leo?
Kama mbio hizi za Mwenge wa Uhuru zipo tu kufuata
utaratibu wa kila mwaka bila ya wananchi kukumbushwa umuhimu wake na watoto
kufundishwa maana yake, basi hakuna atakayekuwa na kosa atakayeuita Mwenge huo
mtumishi hewa namba moja.
0 comments:
Post a Comment