Rais John Magufuli akiwa ndani ya gari lenye namba za usajili T182
DFQ huku akiwapungia mkono watu waliokuwa nje ya Benki ya CRDB tawi
la Holland jijini Dar es Salaam jana, wakati akitoka katika benki hiyo.
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John
Pombe Magufuli amezua taharuki mjini leo baada ya kufika katika Tawi la CRDB
(Holland Branch), akiwa kwenye gari binafsi lenye namba T 182 DFQ huku likiwa
halina nembo ya Adamu na Hawa wala bendera.
Tukio hilo lililodumu kwa takribani dakika 25, limetokea majira ya saa
nne asubuhi ya leo jijini Dar es Salaam katika tawi la benki hiyo ambalo liko
katika makutano ya Barabara ya Ohio na Samora bila kutarajiwa.
Mara baada ya
Rais Magufuli kufika katika eneo liliko tawi hilo makutano ya barabara hizo
yalifungwa huku ndipo rais aliposhuka kwenye gari na kuingia ndani ya benki hiyo.
Wakati akikaribia kuingia ndani ilibidi baadhi ya
wateja waliokuwa wakijiandaa kuingia ndani ya benki hiyo ilibidi wazuiwe
kuingia huku huduma ikiendelea tu kwa wale ambao waliokwisha ingia.
Aidha, baada ya kuingia ndani baadhi ya wateja wa
tawi hilo na wananchi wengine walibaki wakishangaa huku wengine wakijiuliza
imekuwaje Rais kuingia benki kwa staili ile kwani baadhi ya wananchi kudai kuwa
hawajaona tukio kama lile kwa marais wote waliopita.
James Charles, ambaye ni dereva wa Texi, alisema
baadhi ya wananchi waliokuwa kwenye eneo hilo baada ya kuona ulinzi
unaimalishwa walishtuka huku wasijue ni nini kinaendelea, hadi pale walipomuona
Rais Magufuli akishuka kwenye gari hali iliyowafanya wafikirie anakwenda kutembelea
ofisi yake ya zamani.
“Lakini kufumba na kufumbua tukamuona anaelekea
kwenye benki ya CRDB tukajiuliza vipi rais leo kaamua kuwa kama mteja hata
hivyo hatujui kama hiyo ilikuwa inawezekana. Lazima kutakuwa na kitu
haiwezekani aende akachukue fedha kwa utaratibu ule ngoja tusubiri tutasikia amefuata
nini,” alisema Charles.
Joyce Godwin ambaye ni mwanafunzi wa chuo kimojawapo
cha elimu ya juu, alisema kuja kwake kumewashtua wafanyakazi wa tawi la benki
hiyo kwani walidhani alikwenda pale kwa ajili ya kutumbua majipu.
“Mimi wakati Rais Magufuli anaingia nilikuwepo ndani
kwenye foleni nikisubiri huduma kwa ujumla kila mmoja wetu alishtuka lakini hatukujua
kilichomleta,”alisema.
Baada ya Rais Magufuli kumaliza kazi yake
iliyompeleka alitoka na kuingia kwenye gari huku akiwapungia mkono wananchi.

0 comments:
Post a Comment