Rais Dkt John Pombe Magufuli ameeleza kusikitishwa
kwake na baadhi ya taasisi za haki za binadamu zinazolalamikia hatua za
uwajibikaji zinazochukuliwa na serikali kwa baadhi ya watendaji wa serikali
wanaowajibishwa kwa tuhuma za ubadhirifu wa mali za umma, ufisadi na matumizi
mabaya ya ofisi na kutilia shaka uwajibikaji wao.
Rais Dkt John Pombe Magufuli ameyasema hayo jijini
Dar es Salaam wakati akizungumza na wenyeviti na makatibu wa CCM wa wilaya na
mikoa kutoka pande zote za jamhuri ya muungano wa Tanzania aliowaita kwa lengo
la kuwashukuru kwa kufanikisha uchaguzi mkuu wa 2015 ambapo ameonesha
kusikitishwa na malalamiko yanoyotolewa na baadhi ya taasisi za haki za
binadamu kuhusu suala la utumbuaji majipu huku akihoji ukimya wa taasisi hizo
wakati wananchi wa hali ya chini wakiibiwa.
Amesema hatua zinazochukuliwa na serikali yake ya
kuwawajibisha baadhi ya watendaji na watumishi wa serikali wabadhirifu
imesaidia kuokoa kiasi kikubwa cha fedha huku akitolea mfano suala la
wafanyakazi hewa kuwa mpaka sasa wamefikia zaidi ya elfu saba na mia saba.
Aidha Dkt Magufuli amewataka viongozi na wanachama
wa chama cha mapinduzi kusameheana kwa yale yote yaliyotokea wakati wa kampeni
huku akiwaomba kutofanya kile alichokiita kufukua makaburi na badala yake
washikamane ili kuwaletea maendeleo wananchi.
Kwa upande wake makamu wa rais wa jamhuri ya
muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi wa CCM
kuwachukulia hatua wale wote wanaokiuka maadili na taratibu huku akiwataka
kuiunga serikali mkono ili kutimiza adhma ya kuwaletea wananchi maendeleo.
0 comments:
Post a Comment