Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya
Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira ilisema wafungwa wote
wamepunguziwa 1/6 ya vifungo vyao zaidi ya punguzo la kawaida linalotolewa
chini ya Kifungu 49(1) cha Sheria ya Magereza Sura 58 isipokuwa walioorodheshwa
katika Ibara ya Pili.
Meja Jenerali Rwegasira alisema msamaha huo
utawahusu wafungwa wenye magonjwa kama Ukimwi, Kifua Kikuu na saratani na wako
katika hatua ya mwisho, wazee wenye miaka 70 au zaidi ambao magonjwa na umri
viwe vimethibitishwa na Jopo la Waganga chini ya Uenyekiti wa Mganga Mkuu wa
Mkoa au Wilaya.
Alisema pia wafungwa wa kike walioingia na mimba
gerezani na walioingia na watoto wanaonyonya pamoja na wafungwa wenye ulemavu
wa mwili na akili ambao ulemavu huo umeidhinishwa na Jopo la Waganga chini ya
Uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa au Wilaya.
“Ni mategemeo ya Serikali watakaoachiwa huru
watarejea tena katika jamii kushirikiana na wenzao katika ujenzi wa taifa na
watajiepusha kutenda makosa ili wasirejee tena gerezani,” alisema Katibu Mkuu
huyo.
Alisema msamaha huo hautawahusu wafungwa
waliohukumiwa adhabu ya kunyongwa na wale wenye adhabu kama hiyo lakini
imebadilishwa kuwa kifungo cha maisha. Pia wanaotumikia kifungo wa makosa ya
kujihusisha na usafirishaji na matumizi ya dawa za kulevya kama cocaine,
heroine, bangi na mengineyo na wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kujihusisha
na uombaji, upokeaji au utoaji rushwa.
“Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya
unyang’anyi ukiwemo wa kutumia silaha au kujaribu kutenda makosa hayo, au
wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kupatikana na silaha, risasi au milipuko
isiyo halali,” ilisema sehemu ya taarifa ya Katibu Mkuu Meja Jenerali
Rwegasira.
Alitaja wafungwa wengine ambao hawatahusika na
msamaha huo ni wanaotumikia kifungo kwa makosa ya shambulio la aibu, kunajisi,
kubaka na kulawiti au kujaribu kutenda makosa hayo na wale wanaotumikia kifungo
kwa makosa ya wizi wa magari na pikipiki au kujaribu kutenda makosa hayo.
0 comments:
Post a Comment