Rais amemsimamisha kazi Dk. Simba kutokana na kile
alichodai kushindwa kusimamia ipasavyo mkataba wa utekelezaji wa mfumo wa
usimamizi wa mawasiliano ya simu (TTMS), kitendo kilichosababisha nchi kukosa
mapato ya Sh bilioni 400 kwa mwaka – zaidi ya Sh trilioni 1 kwa kipindi cha
miaka mitatu tangu walipoingia mkataba na Kampuni ya SGS Machi 22, 2013.
Uamuzi wa Rais Magufuli umekuja siku moja baada ya
CAG, Profesa Mussa Assad kuwasilisha taarifa ya ukaguzi kwa mwaka 2014/15 kwa
wabunge mjini Dodoma juzi.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Ikulu,
Dar es Salaam jana na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Gerson Msigwa,
ilisema Rais Magufuli amechukua hatua hiyo baada ya kufanya kikao kazi, kati
yake na viongozi, wataalamu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano, Uchukuzi, Wizara
ya Fedha na Mipango na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
“Machi 22, 2013, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania
(TCRA) iliingia mkataba na Kampuni ya SGS juu ya uwekaji, uendeshaji na
uhamishaji wa mapato ya simu ambapo kampuni hiyo ilipaswa kutekeleza vipengele
vitano.
“Lakini mpaka sasa, Kampuni ya SGS haijaanza
kutekeleza kipengele kidogo kinachohusiana na udhibiti wa mapato ya simu ya
ndani (offnet), hali ambayo imesababisha Serikali kukosa mapato yanayokadiriwa
kuwa Sh bilioni 400 kwa mwaka,” ilisema taarifa hiyo.
Pamoja na hatua hiyo, Rais Magufuli ametangaza
kuvunja Bodi ya TCRA inayoongozwa na Profesa Haji Semboja.
Pia amemwagiza Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na
Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa kuteua Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo
mara moja.
Licha ya kutoa agizo hilo, Rais Magufuli amewataka Waziri Mbarawa, Katibu Mkuu wa
wizara hiyo, Profesa Faustine Kamuzora na naibu wake, Mary Sassabo kuchukua
hatua mara moja ili mfumo wa ukusanyaji mapato ya simu za ndani uanze kufanya
kazi na nchi ipate mapato yanayostahili.
“Waziri nakuagiza chukua hatua mara moja, nataka
tukusanye mapato yote ya Serikali yanayostahili na sitasita kuchukua hatua
dhidi ya yeyote atakayekwamisha jambo hili,” alisema Rais Magufuli katika
taarifa hiyo.
MIEZI 9.
Dk. Simba amedumu katika wadhifa huo kwa miezi tisa
tangu alipoteuliwa Julai 6, mwaka jana na aliyekuwa Waziri wa Mawasiliano,
Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa kwa mamlaka aliyopewa chini ya
sheria Na. 12 ya mwaka 2003 ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania
Kifungu cha 13 (1).
Kabla ya uteuzi huo, Dk. Simba alikuwa Mkurugenzi wa
Idara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi
na Teknolojia.
TAARIFA YA CAG.
Juzi akiwasilisha taarifa ya Ukaguzi wa Hesabu za
Serikali bungeni, CAG Profesa Assad, alisema TCRA inaendesha mfumo wa udhibiti
wa mawasiliano ya simu (TTMS) ambao unafuatilia mwenendo wa mawasiliano ya simu
kutoka kwa watoa huduma za mawasiliano waliopewa leseni, bila njia sahihi.
Alisema mfumo wa mawasiliano kwa sasa unaweza
kudhibiti mapato yatokanayo na mawasiliano ya kimataifa, lakini haujaweza
kudhibiti mapato yatokanayo na mawasiliano ya ndani.
“Kukosekana kwa mawasiliano ya kutosha kati ya
taasisi muhimu zinazoweza kunufaika na mtambo huu, kama vile Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kumesababisha Serikali kuendelea
kupoteza mapato yatokanayo na mawasiliano ya simu za ndani,” alisema Profesa
Assad.
0 comments:
Post a Comment