Imesema kipengele kinachodaiwa kuvunjwa ndani ya
Katiba kwa suala hilo ni Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ya mwaka 1977, ambayo hata hivyo inazungumzia uhuru wa kupata taarifa.
Kifungu hicho kinasema: “Kila mtu (i)anao uhuru wa
kuwa na maoni na kueleza fikra zake, (ii) anayo haki ya kutafuta, kupokea na
kutoa habari bila ya kujali mipaka ya nchi, (iii) anao uhuru wa kufanya
mawasiliano na haki ya kutoingiliwa katika mawasiliano yake na (iii) anayo haki
ya kupewa taarifa wakati wowote kuhusu matukio mbalimbali muhimu kwa maisha na
shughuli za wananchi na pia kuhusu masuala muhimu kwa jamii”.
Kwa mantiki hiyo hakuna sehemu ya Katiba hiyo,
inayotaka habari hizo lazima ziwe ‘live’. Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George
Masaju aliyasema hayo wakati akijibu hoja zilizojitokeza katika Hotuba ya
Bajeti ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha wa 2016/17.
Mwanasheria Mkuu huyo wa Serikali alisema hoja hiyo
ingekuwa na nguvu endapo waandishi wa habari wangezuiwa kuingia ndani ya ukumbi
wa Bunge kuchukua taarifa za mwenendo wa vikao vya Bunge.
“Ni jambo la aibu kwa wabunge kuacha kuchangia
Bajeti ya Waziri Mkuu kwa vile tu eti hawaonekani kwenye televisheni.
Tuwatumikie wananchi wetu ambao wametutuma. Haki ya kupewa taarifa si haki ya
kutangazwa ndio maana huwezi kwenda mahakama yoyote kudai kwamba sijui mimi
sijatangazwa,” alisema Masaju.
Kuhusu hoja kwamba Serikali imepoka madaraka ya
Bunge, alisema hoja hiyo haina ukweli wowote kwa vile Bunge linaendelea
kutimiza majukumu yake ya kikatiba ya kuisimamia serikali ili itimize majukumu
yake ipasavyo.
“Hoja kwamba serikali imepoka madaraka ya Bunge si
kweli na wabunge hawapaswi kusema hivyo kwa sababu Bunge limepewa uhuru na haki
ya kujadili haki ambayo haiwezi kupingwa na mahakama yoyote au kuhojiwa kwa
mujibu wa Ibara ya 100,” alisema Mwanasheria Mkuu.
Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa
na Michezo, Nape Nnauye alisema mpango wa serikali kutaka Bunge kuwa na studio
yake utasaidia kuwapunguzia gharama vyombo vya habari kuja Dodoma.
Nape alisema pamoja na mambo mengine mfumo huo
utavisaidia vyombo vya habari kupunguza gharama ya kufika Dodoma kufuata
taarifa na badala yake watakuwa wanapata taarifa moja kwa moja kupitia studio
hiyo kwa bei nafuu na kuongeza kuwa kinachotakiwa sasa ni kwa pande husika
kukaa na kuangalia upungufu uliopo ili kumaliza matatizo yaliyopo.
“Kwa tathmini tuliyoifanya wakati wa mkutano wa
Bunge ulipokuwa ukioneshwa ‘live’, watu wengi mchana walikuwa hawafuatilii kwa
wingi kama wanavyofanya hivi sasa, wakati kipindi cha Leo katika Bunge kinapooneshwa
usiku,” alisema Nape.
Akichangia bajeti hiyo, Mbunge wa Viti Maalumu,
Angela Malembeka (CCM) alisema kuna haja ya wabunge kupimwa akili kabla ya
kuingia bungeni kutokana na baadhi yao kuonesha vitendo vinavyotia shaka.
Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde (CCM) alisema
anashangazwa na wabunge wa upinzani kudai kwamba serikali inavunja Katiba huku
wao wakichukua posho wakati wamesusa. “Wanasema eti serikali imevunja Katiba
lakini posho wanachukua.
Bunge lililopita akina Wenje (Ezekiah – aliyekuwa
Mbunge wa Nyamagana) na wenzake walipiga kelele hapa eti Kabwe (Willson –
aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam) asimamishwe, leo Rais kamtumbua
wanasema anakurupuka yaani hawa hawaaminiki, wanazungumza kila kitu,” alisema
Lusinde.
0 comments:
Post a Comment