Gari la
Hayati Sokoine baada ya ajali.
Tanzania leo inaadhimisha kumbukumbu ya miaka 32 ya
kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu wa zamani wa awamu ya Kwanza Edward Moringe
Sokoine (Pichani)aliyekufa kwa ajali ya gari katika eneo la Dakawa Mkoani
Morogoro tarehe 12 Aprili 1984 wakati akirejea Dar es Salaam kwa barabara
akitokea Dodoma ambako alikuwa akihudhuria Bunge.
Marehemu Edward Moringe Sokoine alikuwa Waziri Mkuu
wa Tanzania kwa awamu mbili, tangu tarehe 13 Februari 1977 hadi 7 Novemba 1980,
na tangu tarehe 24 Februari 1983 hadi kifo chake, alipofariki kutokana na ajali
ya gari.
Wengi wanashuku ajali hiyo kuwa ilipangwa, ingawa
mpaka leo bado ni kiza kitupu.
Uongozi wake ulionekana kuwa wa mfano kwa jinsi
alivyokuwa na uadilifu na kufuatilia utendaji kazi huku akikemea ulaji rushwa
na ubadhirifu wa mali za umma.
Kifo chake kilileta majonzi makubwa kwa Watanzania
wa kawaida ambao walikuwa wanamtarajia kuwatetea wanyonge na kuinua hali ya
maisha yao.
Mwili wa Edward Moringe Sokoine ulizikwa nyumbani
kwao Monduli, mkoani Arusha.
Sokoine aliongoza katika kipindi ambacho nchi
ilikuwa katika hali ngumu sana ya kiuchumi.
Zifuatazo
ni nukuu muhimu za shujaa huyo kutoka katika Kitabu cha Edward Moringe Sokoine:
Kiongozi wa Watu Aliyejitolea kilichoandikwa na Luteni Kanali Albert N. Kigadye
mnamo mwaka 1984:
"Ole
wake kiongozi mzembe na asiye na nidhamu nitakayemkuta: Kiongozi wa siasa hana
usalama wa aina yoyote. Usalama wake ni kudra ya Mungu na Wananchi peke yake.
Viongozi wazembe na wabadhirifu wahesabu siku zao. Labda tusiwajue. Hawa hatuna
sababu ya kuwapa imani, kuwa tutawalinda kama vitendo vyao viovu" - Edward
Moringe Sokoine, 26 Machi 1983
"Juu
ya suala hili la mapato kutolingana na matumizi ni kwamba tungependa kupunguza
uongezaji wa wataalam wasiohitajika katika Serikali na katika mashirika ya umma
mpaka hapo hali yetu ya uchumi itakapokuwa katika hali nzuri" - Edward Moringe
Sokoine, 23 Oktoba 1982.
"Serikali inasimamia bei, lakini Serikali yetu itakwenda mpaka
itasimamia bei ya mhogo, dagaa na bei ya kila kitu? Haiwezekani, vitu vingine
ni lazima vizalishwe kwa wingi ili bei yenyewe iweze kujirekebisha" -
Edward Moringe Sokoine, 24 Septemba 1983
"Wajibu wa kila Mtanzania, kila familia na kila anayekula ni
kujilisha mwenyewe. Si wajibu wa Taifa kumlisha mtu. Unaweza ukasaidiwa
unapopatikana na janga. Lakini kama hakuna janga ni wajibu wa kila mtu aweze
kujitosheleza kwa chakula na atoe ziada kwa Taifa" - Edward Moringe
Sokoine, 4 Oktoba 1983.
"Vijana leo wengi wana mali zaidi kuliko wazee waliofanya kazi
miaka thelathini hadi arobaini. Lakini wanaitaka Serikali ndiyo iwaulize mali
hiyo wameipata wapi. Hivi kwa nini mzazi asimuulize mwanae, 'mali hii umeipata
wapi?'" - Edward Moringe Sokoine, 23 Oktoba 1983
"Katika nchi inayojali haki na usawa, majeshi hayana budi yawe ni
chombo cha kulinda haki na maslahi ya walio wengi. Na kamwe hayaruhusiwi kuwa
ni chombo cha wachache wenye kujali nafsi zao na kusahau maslahi ya walio
wengi" - Edward Moringe Sokoine, 1Februari 1977.


0 comments:
Post a Comment