WAJUMBE wa Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya ALAT wamesema
wakala wa Ufundi na Umeme (Tamesa) ni jipu linalohitaji kutumbuliwa.
Walitoa hoja hizo mbele ya Naibu Waziri Ofisi ya
Rais, Tamisemi, Suleiman Jafo wakati wakichangia hoja kwenye mkutano mkuu wa
ALAT.
Wajumbe hao waliomba serikali kuangalia muundo wa
utendaji wa Tamesa kwani umejaa mizengwe mingi huku wakiwa hawana wataalamu
katika suala zima la utengenezaji wa magari.
Mmoja wa wajumbe alisema kuna maelekezo magari yote
ya halmashauri kutengenezwa na Tamesa lakini yakienda huko hakuna mafundi bali
wanawapa watu wengine watengeneze na gharama zinakuwa kubwa mara mbili.
Naibu Waziri alisema anaichukua hoja hiyo kuifanyia
kazi na atakwenda kuangalia ni nini kinatokea. Alisema pamoja na nia njema,
lakini kutokana na wajumbe wengi kugusia suala hilo inaonesha wazi kuwa
utekelezaji hauko sawa na hivyo ni lazima kuangalia kuna tatizo gani.
Jafo alisema serikali itatoa mafunzo kwa madiwani
kwa kushirikiana na Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo na Uongozi Institute
kuhakikisha madiwani wanapata mafunzo ya kuweza kusimamia vyema miradi ya
wananchi na maendeleo yao.
Pia alisema Serikali ya Awamu ya Tano imejielekeza
kuhakikisha sekta za umma zinapata ushirikiano wa kutosha kutoka sekta binafsi
ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora.
Aidha alisema nchi haiwezi kujengwa bila kuwa na
ushirikiano na sekta binafsi na kuwataka wakurugenzi kutenga maeneo ya
uwekezaji wakati huu ambapo ujenzi wa viwanda unasisitizwa.
“Kila halmashauri itenge eneo kwa ajili ya uwekezaji
kwa kutumia sekta binafsi. Stendi ya mabasi ya Morogoro ni mfano wa kuigwa
kwani walitumia wadau kuwekeza na kuna aina ya uwekezaji ikiwamo maeneo ya
benki, maduka na baada ya muda itakuwa halmashauri yenye pato la uhakika la
ndani,” alisema.
Aliwataka mameya na wenyeviti wa halmashauri kwenda
kusimamia ukusanyaji wa mapato kwa njia ya kielektroniki kuwe na ufanisi.
Aliwataka wakurugenzi wasikubali kuangushwa na watumishi wa chini. Alisema
baadhi ya maeneo, wakuu wa idara wana sauti kuliko wakurugenzi.
0 comments:
Post a Comment