Kutokana na uamuzi huo wa Rais Magufuli kufuta
sherehe za mwaka huu za maadhimisho ya Muungano, wanasiasa, wasomi na viongozi
wa dini wametoa maoni yao.
Akizungumza na kwa njia ya simu, aliyekuwa Waziri wa
Fedha katika Serikali ya awamu ya tatu, Profesa Simon Mbilinyi, alisema kuwa
anaungana na uamuzi wa Rais Magufuli na hauna athari yoyote inayoweza
kujitokeza kwa kusitisha sherehe za Muungano.
“Uamuzi wa rais ni mzuri na Muungano ulikuwepo tangu
siku nyingi, hivyo shamrashamra hazina athari zozote na badala yake
kinachotakiwa ni kuuheshimu na kuutunza basi,” alisema Profesa Mbilinyi.
PROFESA SAFARI.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Bara, Profesa Abdallah Safari, alisema ni
uamuzi mzuri uliofanywa na rais kwa kuwa watu walizoea kufanya sherehe hizo
kama sehemu ya kujipatia fedha kwa masilahi binafsi.
Alisema sherehe zilikuwa ni nyingi, hivyo kusitishwa
kwa sherehe za Muungano kutapunguza gharama zisizokuwa na ulazima.
“Mimi namuunga mkono Rais Magufuli kufuta sherehe
hizo kwani zilikuwa nyingi na watu walizoea kuzitumia kupiga dili kwa masilahi
binafsi,” alisema Profesa Safari.
BASHIRU ALLY.
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDSM), Bashiru Ally, alisema uamuzi huo wa Rais Magufuli unatoa ujumbe wa aina
mbili; kiuchumi na kisiasa.
Alisema Rais Magufuli yupo sahihi kutoa uamuzi huo
kwa sasa kwa kuwa hakuna maana kufanya maadhimisho hayo huku bado Taifa likiwa
tegemezi.
“Ni sawa kwa sababu anajenga uwezo wa ndani kwa
kuzielekeza fedha hizo kwenye shughuli za maendeleo, na naamini kwamba katika
bajeti tutaelezwa baadae kwamba hatua ya kufuta haya maadhimisho na safari za
nje imesaidiaje.
“Lakini Muungano una faida gani na uhuru uko wapi
ikiwa kwa mfano hatuna vitanda na dawa za kutosha kwenye hospitali zetu. Hivyo
hapa kuna ujumbe wa kiuchumi na kisiasa, kwamba lazima tuangalie mambo yetu
jinsi tunavyoamua,” alisema.
Alisema hata hivyo kazi iliyopo sasa kwa Serikali
mbali na kubana matumizi, ni kujitahidi kuongeza uzalishaji wenye tija kwa
jamii.
“Wakati Serikali inajitahidi kubana matumizi, lazima
iongeze uzalishaji wenye tija ili ipatikane ziada na igawiwe kwa usawa kusudi
maendeleo yapatikane, maana kama haya hayatazingatiwa itafika mahali wananchi
watayachoka haya,” alisema Ally.
ASKOFU MWAMBALANGA.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili, Amani na Haki
za Binadamu kwa Madhehebu ya Dini Tanzania, Askofu William Mwamalanga, alisema
kwamba uamuzi huo umeacha maswali mengi.
“Awali alifuta sherehe za Uhuru, kwa maana hiyo huu
ni uamuzi wa pili, lakini sherehe ina umuhimu wake… ni kumbukumbu ya Taifa
lolote duniani kwa sababu huleta watu pamoja kama Taifa,” alisema.
Alisema hata hivyo licha ya sherehe hiyo kuwa na
umuhimu kwa watu wote ameshangaa kitendo cha Rais Magufuli kuzipeleka fedha
zitakazookolewa kujenga barabara ya Uwanja wa Ndege wa Mwanza.
Askofu Mwamalanga alisema kuwa ni vema fedha za kila
sherehe ziwe zinagawanywa kwa usawa katika miradi ya maendeleo
“Zimeokolewa Sh bilioni mbili lakini amezipeleka
kujenga barabara ya mkoa mmoja, hii inaleta ubaguzi kwa sababu kuna mahali wana
tatizo la njaa, barabara na kwingine hakuna madawati, hii si haki,” alisema Askofu
Mwamalanga.
0 comments:
Post a Comment