Lina uwezo wa kuhimili tani zipatazo 1,300 na
limejengwa kwa ubia kati ya Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) iliyotoa
asilimia 60 ya gharama na Serikali kwa upande wake, asilimia 40. Jumla ya gharama
zote ni Sh bilioni 214. Hili ni jasho la Watanzania kwa asilimia 100.
Ni fahari kwa Watanzania kwa kuwa ni daraja la
kwanza na la kisasa kujengwa baharini Afrika Mashariki na Kati. Lakini wakati
tunajivunia mafanikio hayo, tuna kila sababu ya kuunga mkono angalizo
lililotolewa na Rais John Magufuli wakati anazindua rasmi daraja hilo kwa
kulibatiza jina la Daraja la Nyerere badala ya jina lake, kwamba Watanzania kwa
ujumla wao wanatakiwa kulitunza na kulithamini daraja hilo.
Watakaoharibu miundombinu yake hawaikomoi Serikali
bali wanajikomoa wenyewe. Katika jambo hili, Rais hakumung’unya manneno katika
hotuba yake na kutamka wazi kabisa kwamba kwa uharibifu wowote wa daraja hilo
atakuwa mkali na kuviagiza vyombo vya ulinzi kusimamia jambo hilo bila kufanya
ajizi.
Alifafanua kwamba mtu yeyote atakayegonga hata taa
tu atozwe faini kubwa ili kujenga heshima ya kulinda mali za umma. Tunapenda
kumwunga mkono Rais kwa agizo na angalizo hilo muhimu kwa rasilimali hii ya
Watanzania iliyojengwa kwa gharama kubwa na yenye kila aina ya kuleta matumaini
mapya kwa jamii ya wana Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla wake kiuchumi.
Sote tushikamane kuilinda rasilimali hii bila
kuwaachia wenzetu wachache kuiharibu. Licha ya ukweli kwamba daraja hilo
linatarajia kuajiri watanzania 300, faida nyingine ni pamoja na kukuza uchumi,
kupunguza tatizo sugu la msongamano wa magari na vyombo vingine vya usafiri na
kuondoa tatizo la muda mrefu la usafiri kwa wakazi wa Kigamboni.
Kuzinduliwa kwa daraja hilo, mji wa Kigamboni ambao
tayari ni wilaya, kasi ya kuujenga kuwa mji wa kisasa kulingana na mipango miji
ya jiji la Dar es Salaam itaongezeka. Faida za Daraja la Nyerere ziko nyingi na
fursa nazo ziko nyingi pia hivyo kama Watanzania tuna kila sababu ya kufanya
kila liwezekanalo kulitunza daraja hilo.
Tusikubali uzembe wa aina yoyote. Atakayeharibu
chochote achukuliwe hatua kwa kupewa adhabu inayostahili ili kuwa funzo kwa
wengine. Hili linawezekana cha msingi ni kushikamana dhidi ya waharibifu wote.
0 comments:
Post a Comment