Image
Image

Wawili wafa maji baada ya gari yao kuserereka na kutumbukia ndani ya maji Kigamboni.


WATU wawili wamepoteza maisha baada ya gari waliyokuwa wamepanda iliyokuwa ndani ya Kivuko cha Mv Kigamboni cha jijini Dar es Salaam, kusererekea baharini. Watu hao waliokufa jana alfajiri ni dereva wa gari hiyo aina ya Toyota Hiace, yenye namba za usajili T 271 CRG, aliyefahamika kwa jina moja la Dani na abiria, Nice Mwakalago.
Kwa mujibu wa shuhuda wa tuko hilo ambaye ni kaka wa marehemu Nice, Brown Mwakalago alisema walikuwa wakitoka Mbeya katika maziko ya kaka yao, walipanda usafiri wa gari la kupeleka magazeti mikoani na likawashusha jijini Dar es Salaam saa 10 alfajiri Feri upande wa Magogoni.
“Baada ya kushuka hapo feri tunasubiri kuvuka kwenda nyumbani Vijibweni tulikuta hiyo gari imeegesha hapo nje ya kivuko ikitaka kuvuka pia, tukaongea na dereva ili atakaovuka atupeleke mpaka nyumbani tumlipe, akakubali tukapakia na mzigo yetu,” alisema kaka wa marehemu.
Alisema baada ya kupakia mzigo, marehemu Nice alikuwa hajisikii vizuri kutokana na uchovu wa safari na aliomba kukaa ndani ya gari ndugu wengine wakaenda katika kibanda cha kukaa abiria wakisubiri kuingia kwenye kivuko na baada ya kuruhusiwa gari lile liliingia kwenye kivuko na wao waliingia pia na kukaa kwenye mabenchi ya kivuko hicho cha Mv Kigamboni.
“Tukiwa tumekaa hapo kama dakika kumi kupita tukisubiri, kabla hata hatujaanza safari ya kuvuka tukaona gari inaserereka kuingia kwenda baharini hatukuweza kufanya jambo lolote, gari likatumbukia na ndugu yetu pamoja na dereva wa gari hilo wakiwa ndani,” alieleza.
Kaka huyo alilalamikia kutokuwepo kwa mnyororo, ambao huwa unafungwa mbele kuzuia magari kuwa ndiyo jambo lililopelekea gari hilo kutumbukia baharini na kusababisha vifo hivyo. Sigfrid Lyimo ambaye ni jamaa yake na dereva wa gari hilo, alisema Dani alikuwa akiishi naye nyumbani kwake Kigamboni ambalo walikuwa wakifanya biashara ya daladala.
“Ni mimi nilimwambia ahamie kwangu, akaja akawa tunafanya biashara ya daladala huku lakini kila baada ya siku 10 tunavuka kwenda kwake Tandika, Alhamisi alienda kwake na gari na hivi alikuwa anarudi kazini Kigamboni na gari lake,” alisema Lyimo.
Aidha, alisema jana alfajiri saa tisa alimpigia akamwambia anakaribia kuingia kwenye kivuko hivyo akaacha mpango wazi hata hivyo hakutokea mpaka asubuhi alipoamua kupiga simu yake ambayo ilipokelewa na askari na kumtaarifu kuwa jamaa yake amekufa.
Zoezi la uokoaji lilifanywa na Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji, Jeshi la Polisi na pia Jeshi la Maji (Navy). Saa 3.05 asubuhi waokoaji hao walifanikiwa kutoa mwili wa dereva Dani na baadaye saa 7.25 mchana walifanikiwa kutoa mwili wa Nice ambaye alipatikana akiwa ndani ya gari lililozama.
Jitihada za kutoa gari lilikozama ziliendelea hata hivyo, Mkuu wa Kikosi cha Fire, Mrakibu Mwandamizi, Briton Monyo alilalamikia vikosi vyao kuwa na vifaa duni vya uokoaji, jambo ambalo lilisababisha zoezi la uokoaji kuchukua muda mrefu na pia kuwa gumu.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment