MWIGULU Nchemba Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi ameomboleza msiba
wa Christina Mughwai, mbunge wa zamani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) mkoa wa Singida, na kumsifu marehemu kuwa alikuwa mzalendo aliyetanguliza
maslahi ya taifa mbele katika ubunge wake, Anaandika Josephat Isango.
Nchemba
ameyasema hayo leo mchana, baada ya kuwasili nyumbani kwa marehemu, Mbezi
Beach, barabara ya Bagamoyo mtaa wa Makonde alipofika kusalimia ndugu pamoja na
waombolezaji.
Alitumia fursa hiyo kukaa na wanafamilia na ndugu
waliohudhuria hapo kabla ya kutoa maneno machache kwa jinsi anavyomfahamu
marehemu Christina.
“Msiba hauna itikadi za vyama, msiba unatuhusu wote,
na hawa ni ndugu zangu toka Singida, na huyu marehemu ni mtu wangu wa karibu nimefanya
naye kazi kwenye kamati ya bajeti, yeye akiwa naibu msemaji wa Wizara ya eEdha,
kweli ni mtu makini aliyetanguliza maslahi ya taifa badala ya maslahi binafsi.”
Alisema Mwigulu
Aliongeza kwamba, marehemu alikuwa ni mtu anayeweza
kushauri ukweli na ushauri mzuri hivyo kifo chake ni pengo kwa taifa, kwa chama
chake na watu wa Singida ambao amewatumikia kwa miaka mitano kwa nafasi yake ya
Ubunge wa viti maalumu.
Tofauti na ilivyotarajiwa kwa sababu za utani wa
Wanyiramba (kabila la Mwigulu) na Wanyaturu (Kabila la Lissu), Mwigulu alikuwa
mstaarabu hakuingiza utani kwenye msiba kama ilivyozoeleka kwa makabila
yanayotaniana humu nchini.
Alitumia muda mrefu kuongea na dada mkubwa wa Lissu
( Mama Kabula) kabla ya kukaa na wazee, kuwapa pole, kutoa rambirambi na
kuwaaga.
Wakizungumza baada ya kuondoka kwa Waziri huyo,
baadhi ya Wazee kutoka Singida walimsifu kwani wamekuwa wakihasimiana bungeni
lakini kwenye suala la msiba, ameonyesha hakuna itikadi za vyama na
ameshirikiana na ndugu zake toka Singida, jambo waliloita ni ukomavu wa siasa.
Christina, amefariki dunia Aprili 8 mwaka huu,
anatarajiwa kuagwa katika viwanja vya Karemjee, Jumanne, Aprili 12 na kuzikwa
nyumbani kwao wilaya ya Ikungi Aprili 13, siku ya Jumatano.
0 comments:
Post a Comment