STRAIKA wa Simba, Ibrahim Ajib ametua nchini akitokea kwenye majaribio ya kucheza soka Afrika Kusini na Klabu ya Golden Arrows, lakini amekutana na mkasa ambao umemchanganya.
Mabosi Simba, wamedai Ajib ana mkataba nao hadi mwakani, lakini mwenyewe akauma kidole na kuapa kuwa mkataba wake umeisha na kama ataendelea kung’anganiwa yupo tayari kupigania haki yake.
Ajib alishindwa kusaini mkataba Afrika Kusini licha ya kufuzu majaribio kwa madai bado ana mkataba Simba, huku mwenyewe akikana na kudai umeshaisha na yupo huru.
Mabosi wake wameendelea kusisitiza kuwa Ajib ni mali yao na timu inayomhitaji lazima ifuate taratibu za kumsajili ikiwamo kuvunja mkataba uliopo unaomalizika mwakani.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ajib alisema hatakubali kuona anapoteza haki yake kwa kubaniwa na mabosi wake wa Msimbazi.
“Sitokubali haki yangu nidhulumiwe, mimi siidhulumu Simba, nimeifanyia kazi kwa mujibu wa mkataba ambao umemalizika msimu huu ila nahisi kuna kitu kinataka kufanyika.
“Mungu ndiye mpangaji, kama naidhulumu Simba ukweli utajulikana, ila kama nina haki juu ya mkataba wangu basi Mungu pia ataamua ila ukweli sina mkataba na Simba,” alisema Ajib.
Akizungumzia mtu anayejitambulisha kama meneja wake, Juma Ndabile ambaye aliambatana naye Afrika Kusini, Ajib alisema: “Kila mtu anajua meneja wangu, ndiye anayefahamu kila kitu juu yangu, huyo Ndabile si meneja wangu, niliongozana naye tu, pengine haelewi vizuri mkataba wangu ulivyo, ndio maana akanukuliwa ndivyo sivyo.”
Uchunguzi wetu kupitia watu waliofanya mchakato wa mchezaji huyo kutua timu ya vijana ya Simba ambao pia walikiri straika huyo alisaini mkataba wa miaka miwili unaomalizika msimu huu na si mwakani.
“Nilimshughulikia hadi anaenda Polisi Moro waliomsainisha mkataba wa miaka miwili, baadaye Simba ilimnunua kutoka Polisi kwa Sh. 4 Milioni. Sh 2 milioni zilienda Polisi na zilizosalia walimpa Ajib na pia hawakumpa zote. Mwaka jana walitaka kumwongeza mkataba akagoma na mwaka huu pia aliitwa ili wakubaliane mkataba mpya ila washindwa kukubaliana,” alisema mmoja ya waliohusika kumuingiza Ajib Msimbazi na kuongeza;
“Ajib alitaka Sh 60 milioni wao walitaka kumpa Sh 40 milioni. Kitu ambacho hakifanyiki kwenye mikataba ya wachezaji ni kukosa ushirikiano kati ya viongozi wa klabu, TFF na mchezaji mwenyewe, mara nyingi viongozi hawatoi nakala kwa wachezaji wao,” alisema.
Mwanaspoti ilimtaka Ajib kufafanua kuhusu kupewa mkataba mpya ingawa inadaiwa aliugomea, alikiri ni ingawa jana viongozi wa Simba hawakutoa ushirikiano kufafanua madai ya Ajib.
0 comments:
Post a Comment