Siku
ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani ni siku ambayo huadhimishwa
tarehe 3 Mei kila mwaka. Kwa mwaka huu siku hii itaadhimishwa kwa mara
ya 19 tangu ilipoadhimishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1998, ikiwa na
kauli mbiu ya “Uhuru wa vyombo vya habari ni msingi wa haki za
binadamu.” Siku hii iliwekwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kama siku
ya uhuru wa vyombo vya habari; na lengo lake ni kuongeza uelewa juu ya
umuhimu wa vyombo vya habari na kuzikumbusha serikali kuhusu wajibu wao
wa kuheshimu na kulinda haki ya uhuru wa kujieleza, ambao unajumuisha
uhuru wa kupata taarifa, kama unavyobainishwa katika Ibara ya 19 ya
Tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu la mwaka 1948. Siku hii pia
inalenga kuwakumbuka wanahabari waliopoteza maisha katika utekelezaji wa
kazi zao na kushinikiza mataifa kutengeneza sheria rafiki ambazo
zitaviwezesha vyombo vya habari kutafuta na kutoa taarifa kwa uhuru.
Uhuru
wa kujieleza pia unapatikana katika mikataba mbalimbali ya kimataifa
ambayo Tanzania imeridhia na kuahidi kuitekeleza, ikiwemo Mkataba wa
Kimataifa wa Haki za Kijamii na Kisiasa wa mwaka 1966 na Mkataba wa
Afrika wa Haki za Binadamu na Haki za Watu wa mwaka 1981. Haki ya uhuru
wa kujieleza pia inapatikana katika Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Ibara hii inasema “kila mtu yuko
huru kuwa na maoni yoyote na kutoa nje mawazo yake, na kutafuta,
kupokea na kutoa habari na dhana zozote kupitia chombo chochote bila ya
kujali mipaka ya nchi, na pia ana uhuru wa mawasiliano yake
kutoingiliwa kati” kulingana na sheria zilizopo.
Kwa mwaka huu,
maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani yanabebwa na
kauli mbiu “Kupata taarifa ni haki yako ya msingi: Idai.” Kituo cha
Sheria na Haki za Binadamu kinaungana na vyombo vya habari na wadau
wengine wa habari katika kuadhimisha siku hii muhimu.
Pamoja na uhuru
wa vyombo vya habari kuwepo kikatiba katika Ibara ya 18 na kulindwa na
mikataba ya kimataifa, vyombo hivi vimekuwa havifanyi kazi zake kwa
uhuru hapa Tanzania. Tumeshuhudia
matukio mbalimbali ambayo yanakikuka uhuru wa vyombo vya habari katika
miaka ya hivi karibuni, ikiwemo kutishiwa ama kufungiwa kwa vyombo vya
habari, wanahabari kushambuliwa wakiwa wanatekeleza majukumu yao,
kuendelea kuwepo na kutumiwa kwa sheria mbalimbali kandamizi zinazominya
uhuru wa vyombo vya habari, na kutungwa kwa sheria mpya kandamizi kama
sheria ya makosa ya Kimatandao.
Taarifa ya Haki za Binadamu ya
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu ya mwaka 2015 inaonyesha kwamba
uhuru wa vyombo vya habari nchini Tanzania umeendelea kuminywa na
kusababisha wananchi kukosa haki yao ya msingi ya kupata taarifa
mbalimbali.
Kubwa
ni kutungwa kwa sheria mbili ambazo zinakandamiza na kunyima haki ya
uhuru wa kujieleza, kutafuta na kupata habari. Sheria hizi ni Sheria ya
Mtandao na Sheria ya Takwimu.
Sheria ya Mtandao inaminya kwa kiasi
kikubwa haki ya kupata na kusambaza habari na haki ya faragha. Sheria
hii ina vifungu mbalimbali ambavyo vinatoa makosa ya jinai kwa
kubadilishana taarifa mbalimbali na kuwapa askari polisi nguvu kubwa ya
kukagua na kukamata vifaa vya kielekroniki pale ambapo wanahisi
vimetumika kufanya kosa la mtandao au vina ushahidi. Vifungu ambavyo
vinaminya haki ya kupata habari na haki ya faragha ni pamona na vifungu
vya 7,8,14, 16, 31,32,37,41 na 45. Kwa mfano kifungu vha 16 kinakataza
na kutoa adhabu kwa kutoa taarifa ambazo sio sahihi, lakini hakikuweka
bayana taarifa zipi zinaweza kuwa sahihi na zipi sio sahihi.
Sheria
ya Takwimu inaminya uhuru wa vyombo vya habari na asasi za utafiti
kutoa taarifa kwa umma kwa kuzuia kutolewa kwa taarifa kwa kigezo cha
“taarifa ambazo zinapotosha”; kosa ambalo mtu akikutwa na hatia anaweza
kulipa faini ya million 10 au/pamoja na kwenda jela kwa miaka 3. Hili
linaleta uoga na hofu kwa upande wa watafiti, vyombo vya habari na asasi
za kiraia kufanya tafiti na kuziwasilisha kwa uhuru. Sheria hii pia
inahimiza tafiti zote zinazofanywa kutotolewa kwa umma kabla
hazijapitiwa na kupitishwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), jambo
ambalo linalorudisha nyuma uhuru wa kupokea taarifa tofauti za utafiti
na mawazo mdala.
Ukiacha Sheria za Makosa ya Mtandao na Sheria ya
Takwimu, bado zipo sheria nyingine kama Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976
na Sheria ya Usalama wa Taifa ya mwaka 1970 zinaendelea kutumika bila
kufanyiwa mabadiliko, zikiminya uhuru wa vyombo vya habari na habari.
Sheria ya Magazeti ilitokana na sheria kama hiyo ambayo iliwekwa na
wakoloni kwa dhumuni la kukwamisha harakati za ukombozi, ikiwanyima
uhuru waandishi wa habari kwa kuwa na vifungu vinavyowabana katika
kutafuta na kutoa taarifa fulani, hasa zinazoigusa serikali. Kwa upande
wa Sheria ya Usalama wa Taifa, vyombo vya habari vinazuiwa kuandika
kuhusu mambo ambayo ni kwa maslahi ya kulinda usalama wa taifa, lakini
sheria haijaweka bayana ni mambo gani hayo.
Pia Sheria ya Utumishi na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma zinawabana watumishi kutoa taarifa kwa umma.
Pia
hivi karibuni kuzuia vyombo vya habari kurusha matangazo ya moja kwa
moja ya majadiliano Bunge ni kuvinyima uhuru na kuwanyima wananchi haki
yao ya kikatiba ya kupata taarifa. Hatua hii inapaswa kupingwa kwa nguvu
zote, kwani inawanyima wanachi haki yao ya msingi ya kupata habari moja
kwa moja bila kuhaririwa wala kuchujwa. Wananchi wana haki ya kujua ni
nini wawakilishi wao (wao) waliowachagua wanafanya na namna
wanavyowawakilisha Bungeni.
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu
kinatambua umuhimu wa vyombo vya habari katika kukuza na kuhimiza
utekelezwaji wa haki za binadamu. Vyombo vya habari vimekua ni wadau
wakubwa katika kusambaza elimu na hali ya haki za binadamu Tanzania, na
Kituo kimekuwa kikifanya navyo kazi kwa karibu katika hilo.
Uhuru wa
vyombo vya habari umeendelea kupata changamoto kwa kutokuwepo kwa sheria
inayoongoza vyombo vya habari. Sote tunajua kuwa mchakato wa
upatikanaji wa sheria hizi umekwama wa muda mrefu sasa.
Hivyo basi,
kwa kutambua umuhimu wa vyombo vya habari kwa mustakabali wa taifa letu
la Tanzania, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinapendekeza
yafuatayo:
1. Kituo kinatambua na kupongeza juhudi za serikali ya
awamu ya tano katika kupambana na ufisadi, rushwa na matumizi mabaya ya
ofisi. Vyombo vya habari vinaweza kusaidia sana katika mapambano haya
iwapo havitaminywa na sheria na mazingira. Hivyo serekali haina budi
kurekebisha sheria na kufuta vifungu kandamizi vyenye kuminya uhuru wa
habari na wanahabari na kuwapa wanahabari uwanja mpana wa kutafuta na
kutoa habari kwa uhuru, kama; Sheria ya Magazeti, Sheria ya Usalama wa
Taifa, Sheria ya Utumishi na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma
2.
Sheria za makosa ya mitandao na takwimu ni vizuri sheria hizi
zikaangaliwa upya na kurekebishwa ili kutoathiri haki za msingi za
binadamu na utendaji kazi wa vyombo vya habari na asasi za kiraia. Kituo
kinatoa wito kwa serikali kuimarisha nguvu ya vyombo hivi na asasi za
kiraia kufanya tafiti na kutoa taarifa ambazo zitasaidia kuongeza
uwajibikaji na uheshimuji wa haki za binadamu na sheria.
3.
Serikali kuanzisha upya mchakato wa kupata Sheria ya Vyombo vya Habari,
wanahabari na haki ya kupata habari ili tuweze kupata sheria nzuri na
zinazoenda na wakati zitakazolinda na kusimamia uhuru wa vyombo vya
habari na wanahabari.
4. Pia Kituo kinatoa rai wa wanahabari na
vyombo vya habari kuzingatia uweledi na maadili ya kazi yao kwa kutoa
taarifa sahihi, zenye uchunguzi na zenye lengo la kuelimisha, kuendeleza
na kujenga jamii yenye kuheshimu haki za binadamu, utawala bora na
utawala wa sheria nchini.
Mwisho, Watanzania wana haki ya kupata
taarifa mbalimbali, kutoa na kupokea maoni mbali mbali na mbadala kuhusu
mambo yote yanayo wahusu. Hivyo uhuru wa vyombo vya habara ni msingi
muhimu wa kujenga jamii ya kidemokrasia, yenye kuheshimu haki za
binadamu, utawala wa sheria na kwa maendeleo endelevu yetu sote.
Imetolewa na;
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu
Helen Kijo-Bisimba
Mkurugenzi Mtendaji.
Home
News
Slider
LHRC:Sheria ya Takwimu inaminya uhuru wa vyombo vya habari na asasi za utafiti kutoa taarifa kwa umma.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment