Koplo Mbango alikumbana na tukio hilo baada ya dereva wa mke
huyo wa waziri kusimama kwenye alama za kuruhusu watembea kwa mguu kuvuka
barabara na alilazimika kupiga simu kituoni kupata maelekezo baada ya mama huyo
kujitambulisha kuwa ni mke wa waziri.
Akizungumza katika ufunguzi wa kikao cha kazi cha makamanda
wa polisi wa mikoa, mawakili wafawidhi wa Serikali, na wakuu wa upelelezi wa
mikoa na vikosi, kilichofanyika mjini Dodoma, Rais Magufuli bila kumtaja jina
alisema amemwonya waziri huyo na mkewe.
“Ebo! Yule trafiki anajua kazi, mpandishe cheo. Na huyo
waziri na mke wake nimeshamwambia,” alisema Rais Magufuli, kwa mujibu wa
taarifa ya habari ya TBC1.
Licha ya polisi na Rais Magufuli kutotaja jina la waziri
huyo, mazungumzo kwa njia ya simu ambayo yamesambaa yanaonyesha mwanamke huyo
aliyekamatwa akijitambulisha kwa jina la waziri mmoja mpya katika Serikali ya
Awamu ya Tano.
Majibizano ya polisi na mama huyo yanaonyesha kuwa dereva
wake alikamatwa baada ya kusimama katikati ya mistari ya pundamilia, ambayo ni
ishara ya kuvukia waendao kwa miguu.
Mazungumzo hayo yaliyorekodiwa yanaanza wakati Koplo
Deogratius alipompigia simu kamanda wa trafiki wa Kinondoni, Mrakibu Msaidizi
wa Polisi, Awadh Haji na kumueleza tukio lililokuwa mbele yake.
Kadhalika Koplo Deogratius alimueleza RTO Haji kuwa wakati
anataka kumuandikia faini, dereva huyo alitaka kuondoa gari na mama huyo
akamtukana.
“Huyu mama akawa ananitukana… anasema yeye ni mke wa waziri.
Nikamuambia hilo ni kosa la dereva, hivyo sitaruhusu aondoke bali nitampeleka
kituoni. Wakati namuamuru dereva aende kituoni, akataka aondoke,
nikamnyang’anya funguo ili nimpeleke kituoni,” alisema Koplo Deogratius.
“Ameniita mimi mshenzi, sina akili. Anasema yeye ni mke wa
waziri gani?.. Anasema yeye sijui mke wa waziri (anamtaja jina).”
Baadaye Kamanda Haji anataka aongee na mama huyo ambaye
mazungumzo yanaonyesha anakanusha kumtukana askari huyo, akisema alikuwa
akimuomba amuelimishe dereva kwa kuwa kosa alilofanya ni dogo.
“Mimi sikumtukana, wala sikumwambia maneno hayo namshangaa
sijui leo ameamkaje. Kitu nilichomuambia kwamba huyu kijana (dereva) alikuwa
anakwenda moja kwa moja, mimi nilikuwa na vihela kidogo nilikuwa nataka
kuchenji ili nimpe fundi,” alisema mke huyo wa waziri.
“Nikauliza kosa gani, akasema eti kosa lake ni kusimama
kwenye zebra crossing. Nikamuambia sawa, hilo ni kosa la kuelimishwa, lakini
sasa wewe unamuandikia kwa kosa kama hilo? Hilo ni kosa dogo, very minor la
kuweza kumuandikia? Lakini kama unamuandikia andika.”
Kupitia maongezi hayo, RTO Haji alisema kosa hilo ni kubwa
na lina adhabu kali.
“Nikusaidie kitu kimoja, katika makosa mabaya sana mojawapo
ni dereva kutoheshimu zebra crossing. Mahakama inapomkuta mtu na hatia ya
kugonga kwenye zebra crossing, adhabu yake ni jela miezi sita. Haina hata
faini, hiyo tunaita dangerous driving (uendeshaji wa hatari),”alisema Haji na
kumtaka Koplo Deogratius kumuadhibu dereva kwa kosa lake.
Alipotafutwa kuzungumzia tukio hilo, Koplo Deogratius
alikiri kupambana na mke huyo wa waziri, lakini hakutaka kuingia kwa undani
akisema yeye si msemaji wa Jeshi la Polisi.
“Ni kweli nilimkamata huyo mama lakini, kwanza tuelewane.
Mimi siyo msemaji wa polisi. Kama unataka kesho uje pale kituoni, umuone RTO.
Kama akiruhusu mimi nitaeleza kila kitu,” alisema Deogratius akiwa maeneo ya
Namanga.
Naye Kamanda Haji alithibitisha tukio hilo, lakini
akamuelekeza mwandishi kumuuliza kamanda wa polisi mkoani Kinondoni,
Christopher Fuime.
Kamanda Fuime alisemai kuwa Rais Magufuli ameagiza koplo
huyo apandishwe cheo kutokana na kusimamia sheria na kwamba agizo hilo
linafanyiwa kazi.
“Mimi ndiyo natoka Dodoma kwenye hicho kikao cha Rais na
maofisa wa polisi. Hilo ni agizo, sasa unataka tulipinge? Hayo ni mambo ya
utawala, wataangalia wenyewe kama apewe cheo gani. Kwa sasa yeye ni Koplo, kwa
hiyo watajua wenyewe wampe nini. Afande IGP ndiyo anajua,” alisema Fuime.
0 comments:
Post a Comment