Amewataka makandarasi hao pia kuweka mbele uzalendo, badala ya tamaa ya kujipatia faida zaidi, hasa inapotoka miradi mikubwa kutoka serikalini, ili waweze kupatiwa upendeleo. Rais Magufuli aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati alipofungua mkutano wa siku mbili wa mashauriano wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi wa mwaka huu.
Alisema endapo itatokea mtendaji wa serikali akaomba makandarasi hao rushwa, wawasilishe taarifa zao kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wakamatwe na kuchukuliwa hatua za kisheria. “Mimi niwaombe makandarasi, msikubali kutoa rushwa, na muwafichue watendaji wanaoomba rushwa, atakapokuomba wewe rushwa hujui amewaomba wangapi…” “…
Na utakapotoa rushwa huna hakika kama ile zabuni utaipata, wengine wameishia kutoa rushwa hapa, rushwa hapa, rushwa hapa mpaka anafilisika, kazi huipati na rushwa umeitoa,” alisisitiza. Aliwatambulisha makandarasi hao wapatao 100 waliohudhuria mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Valentino Mlowola na kuwataka kuwasilisha taarifa zote za watendaji waombaji rushwa kwa mkurugenzi huyo.
“Ninamuamini sana Mlowola na ninajua hamjamualika hapa, lakini nimekuja naye kwa sababu nafahamu tatizo kubwa la rushwa lililopo katika sekta ya ujenzi. Kama mnaona hamtawaamini maofisa wengine wa Takukuru, basi nendeni moja kwa moja kwa mkurugenzi atachukua hatua,” alisema.
Alisisitiza kuwa tatizo la rushwa ni kikwazo kikubwa kwenye sekta ya ujenzi hali inayowafanya vijana wengi kuikimbia taaluma ya ujenzi; na hivyo kusababisha Tanzania kuwa na idadi ndogo ya makandarasi ikilinganishwa na mataifa mengine. Alisema kwa sasa wastani wa makandarasi ikilinganishwa na idadi ya Watanzania ni mkandarasi mmoja kwa watanzania 6,000 wakati katika nchi kama vile Japan wastani ni mkandarasi mmoja, Wajapani 50.
Aliahidi kuajiri vijana wengi zaidi katika serikali yake, watakaoonesha kwa vitendo kwamba wanaichukia rushwa. “Nimegundua kuna mafanikio makubwa mahali ambako kuna vijana kwa sababu wengi wao hawapendi rushwa. Sisi wazee ndio tunaoliharibu taifa,” alisema. Rais Magufuli aliapa kupambana na tatizo la rushwa nchini na kubainisha kuwa katika miezi kadhaa aliyoshikilia madaraka, kumekuwa na ongezeko la wawekezaji wa kimataifa nchini.
Miongoni mwao, yumo mwekezaji kutoka Ujerumani anayekuja kuwekeza katika kiwanda cha mbolea Kilwa, kitakachokuwa kiwanda kikubwa Afrika Mashariki na Kati. “Tayari nimeanza kuona mabadiliko na nawahakikishia sitaacha kupambana na rushwa…wale wanaofikiri kuwa nitalegeza msimamo watashangaa kwani huu ni mwanzo tu…” “…Ni kwa sababu ya mapenzi ya Mungu ndio maana ni rais wa Tanzania (yeye) na si mapenzi ya mtu yeyote hivyo sitamuogopa mtu.
Niko tayari kujitolea maisha yangu kwa ajili ya wananchi wa Tanzania,” alisisitiza Dk Magufuli. Aidha aliwahadharisha makandarasi wazalendo, kuacha tamaa kwa kuandika maombi yenye gharama kubwa za ujenzi kuliko uwezo wa serikali, hali ambayo ndio kikwazo kwao cha kupatiwa upendeleo wa miradi iliyo chini ya Serikali.
Alisema Serikali ya Awamu ya Tano, iko tayari kuwapa kipaumbele makandarasi wa Tanzania, pale inapotangaza zabuni za miradi ya ujenzi, endapo watajirekebisha kwa kupanga viwango vinavyostahili vya gharama za ujenzi wa miradi hiyo ambavyo Serikali itaridhika. Alitoa mfano wa Idara ya Mahakama iliyotangaza kujenga Mahakama za Mwanzo na Wilaya huku ikiwa na bajeti ya Sh bilioni 24 na makadirio ya kitaalamu yanayoonesha kuwa kila jengo lisizidi Sh milioni 200.
“Lakini makandarasi wazalendo walipoomba zabuni za ujenzi wa mahakama hizi, katika nyaraka zao wametaka jengo moja lijengwe kwa gharama ya Shilingi bilioni1.4, nyingine Sh milioni 670, sasa nakuuliza Mheshimiwa Mwenyekiti na ndugu makandarasi, hata kama una upendeleo, upendeleo huo utapasua moyo sasa,” alisema Rais Magufuli.
Alisema pamoja na nia nzuri ya Serikali ya kutaka kuwasaidia makandarasi wazalendo, ni lazima makandarasi hao kwanza na wao wawe na nia njema ya kuisaidia nchi yao. Pamoja na hayo, Rais Magufuli aliwaahidi makandarasi hao kuwa ataziagiza wizara zote katika Serikali yake, kutoa kipaumbele kwa makandarasi wazalendo katika miradi ya umma huku akiwasisitiza kuhakikisha kuwa wanatimiza masharti yaliyoainishwa.
“Nitaagiza wizara zote kufanya kama ambavyo Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano inavyofanya…na kuhakikisha asilimia kubwa ya miradi ya maendeleo ya umma inatekelezwa na makandarasi wazalendo lakini lazima na nyie mjadiliane vikwazo vinavyosababisha mshindwe kushinda zabuni za miradi hii,” alisisitiza.
Alisema kuna changamoto nyingi zinazoikabili sekta ya ujenzi lakini changamoto nyingi zinasababishwa na makandarasi wenyewe ikiwemo kitendo chao cha kushindwa kushirikiana katika ushindani wa miradi mikubwa ya Serikali.
Rais Magufuli alitoa mwito kwa makandarasi hao, kujipanga ipasavyo waweze kupata zabuni katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya ujenzi itakayofanywa hapa nchini ikiwemo ujenzi wa bomba la mafuta la kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga hapa Tanzania, Ujenzi wa Reli ya Kati na Ujenzi wa Viwanda. “Sina uhakika kwamba mmejipangaje makandarasi wa Tanzania katika kuhakikisha hiyo kazi mnaipata ya kujenga bomba kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga.
Alisema atasikitika sana endapo kilometa zote 1,410 zitajengwa bila kuwepo mkandarasi hata mmoja kutoka Tanzania. Alisema pamoja na mradi huo, pia Serikali imejipanga kujenga Reli ya Kati kwenye bajeti ya mwaka ujao wa 2016/17 kwa kuanza na kilometa 100 ambapo pia kuna fedha zitakazotolewa na Serikali ya China kwa ajili ya kujenga kilometa zaidi ya 1,200 za reli zitakazounganisha nchi za Mwanza, Kigoma, Burundi na Rwanda.
“Wenzetu wanajipanga, na ninavyoona makandarasi wa Tanzania wameendelea sana, lakini nashindwa kuelewa kuna tatizo gani linatufanya kutojua changamoto zinazotukabili, hivi makandarasi wa Tanzania mmejipangaje kushiriki katika miradi hii?” Alihoji Rais Magufuli. Akizungumzia ucheleweshwaji wa malipo ya makandarasi, Dk Magufuli alisema katika Serikali ya Awamu ya Tano, kwa sasa tatizo hilo limeshakuwa historia.
“Serikali yangu imeshaanza kulipa madeni yote inayodaiwa na kampuni za makandarasi. Tumeshalipa mpaka sasa Sh milioni 650 na nyingine Sh milioni 460 kutoka kwa Mfuko wa Barabara na tunawahakikishia tutamaliza madeni yote yanayodaiwa ndani ya sekta hii,” alisema.
Kwa upande wake, Mlowola alisema taasisi hiyo ipo tayari kukabiliana na rushwa iliyopo katika sekta ya ujenzi, ambayo ni miongoni mwa sekta zenye rushwa kubwa na ametaka makandarasi watoe ushirikiano kukomesha tatizo hilo. Naye Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, aliwaahidi makandarasi hao kuwa miradi yote ya umma, itapatiwa makandarasi wazalendo watakaotimiza vigezo na kufuata masharti ya ujenzi wa miradi hiyo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Makandarasi, Consolata Mgimwa, alimshukuru Dk Magufuli na Serikali yake kwa hatua ya kuanza kulipa madeni ya makandarasi , ambayo serikali ilikuwa inadaiwa kwa muda mrefu.
Aidha alisema mkandarasi mzalendo atakayepatiwa mradi wa ujenzi uliopo chini ya Serikali, atautekeleza kinyume na masharti ya mradi huo, atachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufungwa na kufutiwa usajili. “Tutawasilisha mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ili hatua kali ziweze kuchukuliwa dhidi ya makandarasi wasiofuata maadili ya taaluma zao,” alisisitiza.
0 comments:
Post a Comment