HALI si shwari ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kutokana na
mchakato unaoendelea wa kumkabidhi Rais Dk. John Magufuli uenyekiti wa
chama hicho, kukumbwa na sintofahamu.
Taarifa kutoka ndani kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa
(CC), kilichofanyika juzi Ikulu ya Chamwino, mkoani hapa,
zimethibitisha kutokea mgawanyiko wa vigogo ndani ya chama hicho.
Hali hiyo imekuja baada ya kutokea kwa mvutano juu ya tarehe rasmi ya
kufanyika kwa mkutano mkuu maalumu uliopangwa Juni mwaka huu, ambao
pamoja na mambo mengine Mwenyekiti wa chama hicho taifa, Rais mstaafu
Jakaya Kikwete atakabidhi kijiti kwa Rais Magufuli.
Chanzo cha kuaminika ndani ya kikao hicho kililidokeza gazeti hili
kuwa, kabla kilifanyika kikao kidogo kilichokuwa na wajumbe wanne ambao
pamoja na mambo mengine walijadili ajenda muhimu ikiwamo ya kupanga
tarehe kwa ajili ya mkutano huo.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, kikao hicho kidogo kilishirikisha
viongozi wanne akiwemo Mwenyekiti wa chama hicho Jakaya Kikwete, Rais
Dk. John Magufuli, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Katibu Mkuu wa
CCM, Abdulrahman Kinana.
Habari hizo zinaeleza kuwa, katika kikao hicho kidogo viongozi hao
walikubaliana wakatangaze tarehe rasmi, lakini baada ya kikao cha Kamati
Kuu kuanza, Kikwete alikataa kuruhusu hoja hiyo ijadiliwe, hatua
iliyozua mfarakano.
“Baada ya kumalizika kwa kikao kile viongozi hao wanne waliingia
ndani ya kikao cha CC ambacho kilikuwa na ajenda kadhaa ikiwemo ya
mkutano mkuu maalumu ambapo mwenyekiti alirusha na kutaka hoja ya tarehe
isijadiliwe,” kilisema chanzo hicho.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, ilipofika ajenda ya tatu ambayo
iliwasilishwa na Katibu Mkuu, Kinana kuhusu kutangazwa kwa tarehe ya
mkutano mkuu maalumu, Kikwete aligoma isijadiliwe na badala yake
aliahirisha kikao na kutoka nje.
Chanzo hicho kilisema, uamuzi wa Mwenyekiti Kikwete wa kuahirisha
kikao ulijikita katika suala la gharama za mkutano ambazo zinakadiriwa
kuwa ni zaidi ya Sh bilioni mbili, hivyo aliwataka wajumbe waahirishe
kikao ili kutoa fursa ya kutafuta fedha.
Taarifa hizo zilieleza kuwa, kutokana na hali hiyo yaliibuka makundi
mawili, moja linalomuunga mkono Kikwete na jingine linalopingana na hoja
hiyo, likidai kuwa fedha si tatizo kwa chama hicho kwa kwani kina
miradi, ruzuku na marafiki wengi.
“Wanaompinga mwenyekiti walishangazwa na hoja hiyo wakisema kuwa,
suala la fedha ni la watendaji wa chama na si la mwenyekiti, kitendo
ambacho wamekitafsiri kwamba mwenyekiti hana dhamira ya dhati ya
kukabidhi chama kwa sasa,” kilisema chanzo hicho.
Chanzo hicho kiliendelea kutoa taarifa kuwa, baada ya Kikwete kugoma
kujadili tarehe alisimama mjumbe Jenista Mhagama, ambaye alipipinga
uamuzi huo, huku akisema suala hilo ni lazima lijadiliwe kwa kina na
tarehe ya mkutano mkuu itangazwe.
“Kauli ya mwenyekiti inaonekana iliwaudhi baadhi ya wajumbe, lakini
Jenista alizungumza vizuri sana na kumhoji mwenyekiti inakuaje hataki
kusema lini utafanyika mkutano mkuu maalumu ili akabidhi chama.
“Maana suala la makabidhiano ni la utamaduni wa ndani ya CCM, Jenista
alisema aliyekaa muda mrefu alikuwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius
Nyerere pekee lakini na yeye alikabidhi kwa mzee Mwinyi (Ali Hassan) na
pia ilipofika wakati kama huu mzee Mwinyi naye alikabidhi kwa mzee
Mkapa.
“Si hilo tu hata mzee Mkapa naye alikabidhi chama kwake (Jakaya
Kikwete), sasa inakuwaje yeye leo hataki kufuata utaratibu huo ambao ni
wa kawaida ndani ya chama?,” kilihoji chanzo hicho.
Chanzo kingine cha habari kilisema kuwa baada ya mwenyekiti huyo wa
CCM taifa kuahirisha kikao hicho juzi, aliondoka na kurejea jijini Dar
es Salaam kwa gari tofauti na ratiba iliyokuwa imepangwa.
“Ratiba ya chama ilikuwa baada ya kikao cha jana (juzi) mwenyekiti
angelala Dodoma na badala yake alipoahirisha kikao kwa utata alipanda
kwenye gari na kuondoa hali ya kuwa alitakiwa kurejea Dar leo (jana).
“Baada ya kikao hicho alitoka mzee Kinana akiwa amekasirika sana,
tena huku akiwa amekunja sura, unajua siku zote mzee Kinana anaamini
kwamba kile kilichokuwa kinapiganiwa na chama hivi sasa ndicho
kinachotekelezwa na Rais Magufuli tena kwa vitendo tofauti na huko
nyuma,” kilisema chanzo chetu.
Baraza la Wazee kukutana
Taarifa nyingine ambazo MTANZANIA ilizipata ni kwamba, kutokana na
hali hiyo Baraza la Wazee la CCM linaloundwa na viongozi wastaafu,
linatarajiwa kukutana kati ya leo na kesho kwa lengo la kujadili hali
hiyo ili kuondoa mtanziko huo uliojitokeza.
“Ninachotaka kukuambia katika kipindi cha siku mbili baraza la
ushauri la wazee litakutana na kujadili hali hii na baada ya hapo
watakwenda kwa mwenyekiti kumshauri juu ya uamuzi wake na autafakari kwa
kina.
“Tunajua tunakwenda vizuri katika hili na hakuna kitakachoharibika na
wazee wetu watamshauri vema mwenyekiti ili kupata mwafaka wa kudumu na
mkutano mkuu utafanyika mwezi uliopangwa,” chanzo hicho kilisema.
Baraza la Ushauri la Wazee wa CCM, linaongozwa na Rais mstaafu wa
awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi (Mwenyekiti), Pius Msekwa (Katibu) na
wajumbe ni Rais mstaafu Benjamin Mkapa pamoja na Makamu Mwenyekiti wa
CCM mstaafu (Bara), John Malecela.
Jenista alonga
Kutokana na hali hiyo MTANZANIA ilimtafuta Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Waziri Mkuu, Uratibu, Bunge, Kazi na Walemavu, Jenista Mhagama, ambapo
alisema hawezi kuzungumzia suala hilo huku akitaka atafutwe msemaji wa
chama hicho, Christopher Ole Sendeka ndiye mwenye majibu ya kina.
Mazungumzo kati ya Jenista na mwandishi yalikuwa hivi; MTANZANIA: Mheshimiwa nasikia kwenye Kamati Kuu kulikuwa hapatoshi.
Jenista: Mimi siwezi kuzungumzia hilo mtafuteni
msemaji wa chama Ole Sendeka yeye ndiyo msemaji wetu wa vikao vya chama
lakini si mimi ndugu zangu.
MTANZANIA: Mbona kuna taarifa zinaeleza kwamba wewe
umemkabili Mwenyekiti kwenye kikao kuhusu tarehe ya mkutano mkuu maalumu
juu ya Rais Magufuli kukabidhiwa chama?
Jenista: (kicheko) jamani mimi hilo sijui mtafute Sendeka ndiye anaweza kuzungumzia masuala yote ya chama.
Pamoja na majibu hayo alipotafutwa Msemaji wa CCM, Christopher Ole
Sendeka kuhusu kikao cha Baraza la Ushauri la Wazee, alisema hana
taarifa ya kiko hicho.
“Sina taarifa hizo na wala sijasikia chochote labda wazee wao wenyewe
wana ratiba zao, kwani si lazima kila wanapokutana watoe taarifa kwa
chama,” alisema Sendeka.
Home
News
Slider
Mchakato wa kumkabidhi Rais.Magufuli uenyekiti wa CCM Ngoma nzito*Mwinyi, Mkapa, Malecela, Msekwa kujadili.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment