Ni imani yetu kuwa, kwa kuzingatia sheria, mambo yanayofanywa sasa na baadhi ya wafanyabiashara wa sukari wasio waaminifu yasingetokea. Watanzania, bila sababu za msingi wamejikuta wakiingizwa katika harakati ya kusaka sukari huku walionayo wakiitoa kidogo kidogo kuonesha kwamba kuna uhaba, wakati uhalisia hauko hivyo.
Wateja wa sukari wa rejareja ambao zaidi huitumia kwa matumizi ya nyumbani, wamejikuta wakilazimika kuinunua kwa kupangiwa kiasi na bei ya juu, kwa sababu tu wafanyabiashara wakubwa wameificha.
Tunampongeza Rais John Magufuli kwa msimamo wake wa kutaka wafanyabiashara wanaojihusisha na hujuma ya sukari kwa kufanya bidhaa hiyo ionekane adimu nchini, wachukuliwe hatua stahiki.
Msimamo huo, pamoja na hatua za kisheria zitakazochukuliwa dhidi ya wahusika, zitakuwa ni fundisho litakalowakumbusha wengine umuhimu wa kutii sheria za nchi, hata kama wana mitaji mikubwa kiasi gani.
Nidhamu ya kibiashara nayo itaongezeka kwa wafanyabiashara wengi kama si wote, huku wananchi nao wakipata moyo wa kuwafichua wanaozichezea sheria wakati wakiendesha biashara zao.
Hatua hizo ni faida, kwa sababu wanapofichuliwa, kukamatwa na kuchukuliwa hatua zinazostahili, wenye mpango wa kuiga matendo yao yasiyofaa huingia hofu na kuacha kuthubutu kuyatenda, hivyo kuliacha soko liendelee kama inavyotakiwa.
Kinachofanywa na baadhi ya wauzaji wakubwa wa sukari nchini ni aibu inayoonesha wazi kuwa wameshindwa kuheshimu sheria za Tanzania, wakati wakiendesha biashara zao. Ni jambo lisilofaa kuvumiliwa kwamba wauza sukari waliopewa vibali vya kuendesha biashara ya sukari wanahusika kuhujumu upatikanaji wa bidhaa hiyo kwa sababu wanazozijua wao, bila kumjali mtumiaji.
Kama haitoshi, wameendesha uvunjaji wa sheria kwa kuficha sukari kwenye maghala yao hata baada ya Rais kukataza mchezo huo mchafu. Tunajiuliza, vitendo hivyo vibaya vimelenga kuwanufaisha pekee au kuonesha kuwa wana nguvu wanayoitegemea nje ya sheria?
Huu ndio wakati wananchi tunapaswa kusimama kidete kumuunga mkono Rais kuhakikisha tunamaliza hujuma zozote katika soko la sukari kwa kuwafichua wanaojihusisha nazo. Kama ilivyoelezwa, kuficha bidhaa muhimu kama sukari, inayohitajiwa na wananchi karibu wote ni kuhujumu uchumi waziwazi.
Tayari vinara wa kuficha sukari wameanza kujulikana na mamlaka zinazohusika kushughulikia masuala yao zimeanza kufanyia kazi hujuma yao. Wito wetu kwa mamlaka hizo na wananchi ni kuhakikisha vita dhidi ya wanaosababisha kukosekana kwa sukari ya kutosha sokoni hawapati mwanya wa kutumia rushwa na kujuana, kujiondoa kwenye mkono wa sheria.
Vilevile, tunatoa rai kwa watumiaji ambao ni wateja wa sukari kutohofia kuwaripoti kwenye vyombo husika, wafanyabiashara wanaoendelea kuiuza kwa bei zaidi ya iliyoelekezwa, Sh 1800. Kiburi cha waficha sukari kilianza baada ya Rais kupiga marufuku uingizaji bidhaa hiyo kutoka nje.
0 comments:
Post a Comment