YANGA
imejisogeza jirani na ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya
kuifunga Toto Africans mabao 2-1 Uwanja wa CCM, Kirumba Mwanza. Ushindi
huo umeiwezesha timu hiyo kufikisha pointi 65 katika msimamo wa Ligi Kuu
Tanzania Bara baada ya kucheza mechi 26, ikifuatiwa na Azam yenye
pointi 58 na Simba yenye pointi 57.
Hata hivyo Simba na Azam
zimezidiwa mechi moja na Yanga na zinachuana leo zenyewe Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam. Toto Africans ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika
ya 39 mfungaji akiwa William Kimanzi, akiunganisha krosi ya Abdallah
Seseme.
Timu hizo zilishambuliana kwa zamu, lakini umaliziaji haukuwa
mzuri, huku washambuliaji Donald Ngoma, Amis Tambwe na Deus Kaseke wa
Yanga wakipoteza nafasi nyingi. Nao wachezaji wa Toto Africans
wakiongozwa na Seseme na Kimanzi nao walikaribia lango la Yanga, lakini
walipiga mashuti dhaifu ama kushindwa kulenga lango.
Yanga ambayo
mchezo wake uliopita dhidi ya Mgambo Shooting, ambao pia ilianza
kufungwa bao kabla ya kusawazisha na kuibuka na ushindi kama wa jana,
ilisawazisha bao dakika ya 50 mfungaji akiwa Kaseke kutokana na pasi ya
Tambwe.
Dakika ya 76 Yanga ilipachika bao la pili mfungaji akiwa Juma
Abdul aliyemalizia mpira wa Simon Msuva na kuibua shangwe kwa mashabiki
wa Yanga. Yanga; Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Kelvin
Yondan, Vincent Bossou, Haruna Niyonzima/Thabani Kamusoko, Salum Telela,
Simon Msuva, Amissi Tambwe/Malimi Busungu, Donald Ngoma na Deus
Kaseke/Matheo Anthony.
Toto Africans; Mussa Mohamed, Eric Muliro,
Hassan Khatibu, Salum Chukwu, Carlos Protus, Jamal Soud, Abdallah
Seseme, Waziri Junior, William Kimanzi na Edward Christopher. Wakati
huohuo Mwandishi Wetu anaripoti kutoka Tanga kuwa Coastal Union jana
ilijisogeza karibu zaidi na shimo la kushuka daraja baada ya kukubali
kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa African Sports.
Bao hilo pekee
lilifungwa na Mohammed Mtindi, ambapo limeiacha Coastal ikishika nafasi
ya 16 kati ya timu 16 zinazoshiriki ligi hiyo ikiwa na pointi 22, wakati
African Sports ikichupa kutoka nafasi ya 15 hadi ya 13 ikiwa na pointi
25.
Timu zote hizo zimebakisha mechi mbili kumaliza ligi. Coastal
Union ili ibaki Ligi Kuu inaziombea mabaya timu za African Sports,
Mgambo, JKT Ruvu na Kagera Sugar ambazo zina pointi chini ya 26 zifanye
vibaya na yenyewe ishinde mechi zake mbili zilizosalia na kufikisha
pointi 28.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment