Image
Image

Mhezo Mwema Kwenu Taifa Stars.

TIMU ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) leo inashuka kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam kucheza na Misri katika mchezo wa kuwania kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zitakazofanyika Gabon mwakani.
Mchezo huu ni muhimu sana kwani kwa mara ya mwisho Tanzania ilicheza fainali za Mataifa ya Afrika mwaka 1980 nchini Nigeria, ikiwa ni miaka 36 imepita tangu wakati huo.
Taifa Stars leo inatakiwa kucheza kwa kujituma sana ili kuhakikisha inashinda kwa mabao mengi ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kufuzu kwa fainali hizo za Gabon.
Pamoja na Taifa Stars kuwa na pointi moja na kushika mkia, lakini timu hiyo inaweza kupenya kama itaifunga Misri kwa mabao mengi na kufanya kweli katika mchezo wake wa mwisho dhidi ya Nigeria Septemba.
Tayari Nigeria imeshatolewa katika mbio hizo za kusaka nafasi ya kucheza katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika nchini Gabon na mbio zimebaki kwa Taifa Stars na Misri. Misri nao wamebakisha mchezo mmoja tu na wanahitaji pointi moja tu ili waweze kufuzu, hivyo ni kazi kwa Taifa Stars kuizuia Misri kushinda au kutoka sare.
Ni matarajio ya wengi kuwa wachezaji wa Taifa Stars watacheza kwa kujituma kupigania taifa lao liweze kufikia rekodi ya mwaka 1980 ya kucheza fainali za Mataifa ya Afrika. Wadau na wapenzi wa soka wa Tanzania wamechoka kuziangalia timu za nchi nyingine katika luninga na sasa wanataka kuwaona wachezaji wao wakipambana katika mashindano hayo makubwa ya timu za taifa barani Afrika.
Pamoja na ugumu wa mchezo huo wa leo kwani hakuna asiyeijua timu ya Misri kwa ubora wake, lakini katika soka hakuna lisilowezekana, hivyo Taifa Stars wanaweza kushinda na kuweka hai matumaini ya kutinga fainali hizo.
Katika soka hakuna lisilowezekana na kama Taifa Stars walifungwa mabao 3-0 Misri, iweje Taifa Stars ishindwe kuwafunga Misri tena kwa mabao mengi? Wapenzi wa soka wanatakiwa kuiunga mkono Taifa Stars wakati wote wa mchezo kwa kuishangilia kwa nguvu ili kuwakatisha tamaa Misri, ambao wana uwezo mkubwa kisoka.
Umoja ni nguvu na utengano ni udaifu, hivyo wadau wote wa michezo hasa soka wanatakiwa kuwa pamoja kuisapoti Taifa Stars ili kuhakikisha Misri hawatoki `salama’ uwanjani na badala yake wanapokea kipigo cha mbwa mwizi.
Kila la heri Taifa Stars katika mchezo wa leo dhidi ya wapinzani hao wa Misri na Inshallah mtashinda na kuweka hai matumaini ya kwenda Gabon mwakani. Mungu Ibariki Taifa Stars. Mungu Ibariki Tanzania.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment