Image
Image

Safari ya kupata viwanda 5 vya ‘SU’ kwa mtaji wa EFD.

WIKI hii imekuwa na upekee kwa kutoa mwelekeo wa uchumi wa Tanzania. Kila jambo lililokuwa dodoso au ubashiri, sasa una ufafanuzi kamili. Kilichobaki ni kushuhudia uchambuzi na utekezaji wa maono hayo.
Mjini Dodoma katika siku mbili zilizopita, kuliwasilishwa mambo makuu matatu. Mosi ni Mpango wa Taifa wa Maendeleo ya Taifa wa Miaka Mitano ijayo hadi kufikia mwaka 2021.
Siku moja baadaye, ambayo ni juzi bungeni asubuhi kuliwasilishwa Mwelekeo wa Hali ya Uchumi wa Taifa na jioni ikawa bajeti ya serikali kwa mwaka mmoja ujao wa fedha.
Wakati anaingia madarakani miezi saba ilyopita, Rais Dk. John Magufuli alisisitiza hoja yake ya kuanzisha Tanzania ya Viwanda, huku akiweka msisitizo katika ujenzi wa kurejesha viwanda mikononi mwa umma, viwanda vilivyobinafsishwa na kurejeshwa mkononi mwa umma.
Tayari utekelezaji wa azma hiyo unajitokeza katika sura kadhaa. Moja ni kupitia kauli ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, aliyeeleza katika mawasilisho ya Mpango wa Maendeleo ujao kwamba imetengwa Sh. trilioni 107 kwa ajili ya kujenga viwanda vipya vya umma.
Alieleza mchakato wa kupata fedha hizo, kila mwaka serikali itatenga Sh. trilioni 11.8 za kutekeleza azma hiyo na kiasi kingine Sh. trilioni 9.6 kitapatikana kutoka kwa wadau wa maendeleo.
Kimsingi, dhamira kuu ya serikali katika eneo hilo ni kuonyesha njia na kuhakikisha inashikilia baadhi ya viwanda nyeti.
Ili kuvutia sekta binafsi, hapo ndipo kwenye mahitaji makuu ya sera ya ushirikiano baina ya Sekta Binafsi na Umma (PPP), iliyokwishatungiwa sheria maalum ya kusimamia.
Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), ndio kinabeba jukumu kubwa la kuvutia uwekezaji na inawajibika na uratibu wote wa shughuli hiyo ya uwekezaji, hasa kutoka kwa wageni.
Mikakati ya serikali ni kuipatia balozi mbalimbali za Tanzania nje ya nchi, kutangaza fursa za uwekezaji kupitia Diplomasia ya Uchumi.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa anasema kuna viwanda 39 vilivyoanishwa na viko mbioni kurejeshwa katika umiliki wa umma.
Katika hilo, Waziri wa Fedha Dk. Philip Mpango, anaenda mbali kupitia hotuba yake ya bajeti juzi kuwa, serikali inafanya tathmini ya viwanda vilivyobinafishwa kuangalia ufanisi wake na serikali itachukua hatua kali dhidi ya watakaokiuka.
Ubinafisishaji nchini ulifanyika kuanzia mwanzoni mwa miaka ya 1990, chini ya Tume ya Rais ya Kurekebisha Mashirika ya Umma (PSRC) na kupitia hatua mbalimbali na kuhusisha zaidi ya mashirika ya umma 400, ili kuviweka mikononi mwa wawekezaji waliotarajiwa kuviendesha kwa ufanisi.
Mkakati uliotumika kubinafisha taasisi hizo za umma ambazo katika sehemu kubwa ni zilikuwa viwanda ina sura kuu nne.
Njia ya kwanza ni kuuzwa kwa asilimia 100 taasisi inayoendeshwa kwa hasara, ili kuiweka mkononi mwa mwekezaji atakayoiendesha kwa tija.
Pili ni kiwanda kinabinafsishwa kwa asilimia zaidi ya 50 kupewa mwekezaji na hisa iliyobaki zinabaki kwa serikali na wananchi au vinginevyo serikali itakavyiamua juu ya hisa zake.
Sura ya tatu, umiliki wote wa kampuni au taasisi kuhamishiwa kwa wafanyakazi. Ni Utaratibu ambao ni maarufu kwa jina la Mebo (Management by Ownership).
Hilo lilifanyika kwa Kiwahda cha Uchapaji cha Taifa (Kiuta) na Kampuni ya Saana za Mikono (Handico) ambayo imeshatoweka.
Njia ya nne ya ubinafsishaji ni kukodisha kampuni kwa mkataba wa muda maalum, ambao ulifanyika kwa iliyokuwa Shirika la Reli Tanzania (TRC), ambayo baada ya ubinafsishaji iliunda kampuni kadhaa.
Hizo ni Shirika la Umiliki wa Huduma za Reli (RAHCO) na Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) ambayo ilimiliki vyombo vya usafiri tu, kwa masharti maalum, ikiwamo kuwajibikia baadhi ya huduma ambayo si sehemu ya miliki yake.
Hata hivyo, kampuni a Rites kutoka India walioikodi TRL kwa mkataba wa miaka 20, ilishindwa kutimiza masharti ya mkataba na wakanyang’anywa kandarasi hiyo na umiliki umerejeshwa kwa serikali kupitia RAHCO.
Dk. Mpango anasema hivi sasa katika kuvutia miradi mipya ya uwekezaji ikiwamo viwanda, inajenga mazingira bora ya uwekezaji kama vile upatikanaji mikopo kwa Watanzania kupitia Benki ya Rasilimali (TIB) na urafiki kwa wawekezaji wa kigeni walioko nchini, ili wawe mabalozi wazuri kwa wenzao walioko mbali.
Anataja mfano mmojawapo wa kuvutia wawekezaji ni kuboresha huduma za upatikanaji umeme na kujenga urafiki wa kuvutia uwekezaji kupitia ubalozi katika mataifa kama vile Brazil, Uingereza, Afrika Kusini na China.
Dk. Mpango anasema kuwa, pia Watanzania walioko nje ya nchi (Diaspora) wanaendelea kuhamasishwa kuja kuwekeza nchini.
Hata hivyo, dira na ndoto hiyo ya Dk. Magufuli ambayo amekuwa akiihubiri tangu akiwa kwenye kampeni za uchaguzi na sasa ana zaidi ya miezi saba mdarakani, mtihani wake ulikuwa atapata wapo mtaji wa kuwekeza katika viwanda hivyo?
MTAJI WA VIWANDA
Hatua ya kwanza iliyoshuhudiwa kwa sehemu ya utendaji wake wa awali, ni katika maboresho ya makusanyo ya kodi yaliyojidhirisha kuwa na mafanikio makubwa kwa kuvuka malengo.

Kupitia mawasilisho ya bajeti juzi bungeni, Dk. Mpango alitaja maboresho mengi yanayolenga kuhakikisha pato la serikali halipotei kirahisi na wakati huo huo inaongeza vyanzo vyake.
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inaonekana kuaminiwa sana hivi sasa na katika mabadiliko ya serikali imebebeshwa jukumu la kukusanya mapato yote ya serikali, ikiwamo yasiyo ya kodi.
Na ili kufanikisha hilo, kumekuwapo msisitizo maalum wa kutumia mashine ya kielektroniki (EFD), huku kukiongezwa kanuni nyingi za kisheria za kuhakikisha pato la taifa halipotei.
Dk. Mpango anasema matumizi ya EFD yanawalenga wafanyabiashara wakubwa na wa kati wanaotakiwa na kisheria kuzitumia.
Tayari Rais Dk. Magufuli alishaagiza kutolewa bure EFD, ili zisambae kwa wafanyabiashara wengi, jambo litakaloisaidia serikali kukusanya kodi kirahisi.
Mwana- uchumi Profesa Ibrahim Lipumba, akizungumza muda mfupi baada ya kuwasilishwa bajeti juzi jioni, anakosoa kuwa matumizi ya EFD kitaifa ni hayatekelezeki kirahisi, kwani usambazaji wake umekuwa mgumu jijini Dar es Salaam, kabla ya hata kufika mikoa mingine.
Hata hivyo, Dk. Mpango katika mkakati wake wa kuhimiza makusanyo ya serikali, alitoa mkakati mmojawapo wa serikali ni kwamba malipo yote ya serikali, ni lazima risiti zake ziwe za mashine ya EFD.
Pia, vituo vyote vya mafuta nchini vimepewa muda hadi mwisho wa mwaka huu, mfumo wao wa malipo uwe umeunganishwa na EFD.
Mwanazuoni mwandamizi wa uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Haji Semboja anasema kufanikisha matumizi ya mashine hizo pia inaendana na elimu ya kutosha.
Anasema wananchi wenye uelewa ndiyo wanaokuwa na utashi wa kulipa kodi na kuwekeza ndio wanaoweza kufanikisha azma ya serikali ya kuinua uwekeza katika viwanda nchini.
Dk. Semboja anafafanua kunahitajika utashi wa wananchi kuwekeza kwenye viwanda vidogo, ikiienda sambamba na alichokiita ‘dozi’ ya mwananchi kuwa na elimu na taarifa za kutosha.
Mtaalamu huyo anasema, hatua inayofuata ni kwa wafanyabiashara kuendesha shughuli zao katika mfumo rasmi na unaotambuliwa na serikali, ili waweze kukopesheka benki na kupata huduma muhimu za serikali .
DK. MPANGO NA NDOTO YA VIWANDA
Akiwasilisha hotuba ya bajeti yake jana, Dk. Mpango alisema:”Serikali itatekeleza azma ya kuendeleza viwanda ambavyo ndiyo msingi wa uchumi endelevu utakaowezesha taifa letu kufikia hadhi ya kipato cha kati na hali bora ya maisha ya wananchi walio wengi ifikapo mwaka 2025.

“Bajeti ya serikali ya mwaka 2016/17 inalenga kuimarisha miundombinu ya msingi kama vile ya maji, umeme na usafirishaji, kwa ajili ya kuhakikisha maendeleo ya viwanda nchini na vile vile kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo yanayotumika kama malighafi viwandani.
“Ili kufanikisha hilo, mkazo mkubwa utawekwa kwenye ukusanyaji wa mapato ya ndani pamoja na ugawaji wa rasilimali hizo katika maeneo muhimu ya kuvutia uwekezaji kwenye sekta ya viwanda.
“Jitihada kubwa zitaelekezwa katika kuziba mianya ya ukwepaji kodi, kuibua vyanzo vipya vya mapato na kuhimiza matumizi ya mashine za kielektroniki - EFD ili kuongeza makusanyo na vile vile kudhibiti matumizi yasiyokuwa na tija.
“Hivyo, kaulimbiu ya bajeti za nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa mwaka 2016/17 ni “kuongeza uzalishaji viwandani ili kupanua fursa za ajira.”
“Kwa msingi huo, bajeti ya maendeleo kwa mwaka 2016/17 imeongezwa kwa kiasi kikubwa na kufikia asilimia 40 ya bajeti yote, tofauti na miaka yote ya nyuma ilikuwa wastani wa asilimia 25.
“Bajeti hii inalenga kujenga mazingira mazuri ya kufanya biashara na kuwekeza, ili kuvutia ushiriki wa wawekezaji wa ndani na nje katika kuendeleza viwanda na kilimo,” anatamka Dk. Mpango na kuongeza:
“Serikali itatekeleza azma ya kuendeleza viwanda ambavyo ndiyo msingi wa uchumi endelevu utakaowezesha taifa kufikia hadhi ya kipato cha kati na hali bora ya maisha ya wananchi walio wengi ifikapo mwaka 2025.”
MABORESHO YA MAZINGIRA
Dk. Mpango anasema ili kuboresha mazingira bora ya kuwa na ‘Tanzania yenye viwanda,’ bajeti inayotarajiwa kutekelezwa katika mwaka ujao wa fedha, inalenga kuimarisha miundombinu muhimu katika kuhuisha sekta hiyo kama inavyohubiriwa na Rais Dk. Magufuli, katika mikakati yake ya kitaifa.
Ili kufanikisja hilo, Dk. Mpango anaeleza umuhimu wa kuboresha huduma muhimu kwa jamii na maendeleo ya viwanda.
Anataja baadhi ya huduma hizo kuwa ni maji, umeme na usafirishaji na anafafanua kwamba: “Kwa ajili ya kuhakikisha maendeleo ya viwanda nchini na vile vile kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo yanayotumika kama malighafi viwandani.
“Ili kufanikisha hilo, mkazo mkubwa utawekwa kwenye ukusanyaji wa mapato ya ndani pamoja na ugawaji wa rasilimali hizo katika maeneo muhimu ya kuvutia uwekezaji kwenye sekta ya viwanda.
Katika suala hilo la ukusanyaji mapato, Profesa Lipumba, aliyeshawahi kuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muugano wa Tanzania mara kadhaa, anaeleza hofu yake katika matumizi ya EFD kama yatafika sehemu zote za nchi ndani ya kipindi kifupi.
Msomi huyo pia alishawahi kuwa mwanatalamu wa Taasisi ya Utafiti wa Uchumi wa UDSM.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment