Image
Image

Wapinzani: Hatushiriki vikao hata kama tukinyimwa posho






SIKU moja baada ya Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, kutangaza kutowalipa posho wabunge wanaosusa kushiriki vikao vya Bunge, wabunge wa upinzani wamesema hawatasitisha utaratibu wao wa kutoshiriki vikao anavyoviongoza.
Akijibu mwongozo uliokuwa umeombwa na Mbunge wa Nkasi (CCM), Ally Keissy, kuhusu kususa kwa wabunge wa upinzani kushiriki vikao vya Bunge huku Bunge likiendelea kuwalipa posho, Dk. Ackson aliagiza bungeni mjini hapa juzi kuwa wabunge wenye tabia hiyo wasilipwe posho.
Kiongozi huyo alisema uamuzi wake huo umetokana na uamuzi uliowahi kutolewa bungeni miaka iliyopita dhidi ya wabunge wa Chama cha Wananchi (CUF).
Hata hivyo, katika mahojiano na Nipashe kwa nyakati tofauti kwenye viwanja vya Bunge jana, wabunge wanaotoka vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), walipinga kitendo hicho huku baadhi yao wakidai "huenda Kiongozi huyo wa Bunge amepata shinikizo la wakubwa wake wa kazi."
MWITA WAITARA
Mbunge wa Ukonga (Chadema), Mwita Waitara, alisema Naibu Spika amekosea kutoa uamuzi huo kwa sababu chanzo cha wabunge wa upinzani kususa vikao vya Bunge ni yeye mwenyewe.

"Ukawa hawezi kutishiwa posho tunapokuwa na hoja na mawazo ya msingi. Hoja yetu hapa si posho, kuna mambo ambayo anayafanya (Naibu Spika) hayaendi sawa na si ya kawaida. Hoja ya posho akawatishie watoto, sisi ni watu wazima.
Tumekuja hapa tuna utashi mkubwa," alisema Waitara.
"Kama suala ni kuwanyima watu posho, hatutarudi humo kwa sababu ya posho. Naibu Spika amekuwa akifokeafokea watu anapokaa kwenye Kiti cha Spika. Mambo ya msingi anayazima kwa manufaa yake na serikali," alisema.
"Pia, Naibu Spika ni mwanasheria, yeye tuna ugomvi naye, tunamtuhumu kwa mambo ya msingi ya utawala bora ameyakiuka. Sasa kama ni mtuhumiwa, anapata wapi uhalali wa kukaa kwenye Kiti cha Spika na kutoa uamuzi dhidi yetu? 'This is very unfair' (hii si haki).
Alipaswa kumtuma hata Mwenyekiri wa Bunge akasema uamuzi huo wa kufuta posho. Yeye ni mtuhumiwa, hawezi kumhukumu mtuhumiwa mwenzake."
Aidha, Waitara alidai kuna wabunge wa CCM wanamaliza miaka mitano hawajachangia chochote bungeni, lakini wanalipwa posho.
"Kuna wabunge wa CCM, kazi yao ndani ya Bunge ni kupiga makofi na kusema 'NDIYO', lakini wanalipwa posho. Naibu Spika alipaswa kuanza na hili kabla ya kufanya uamuzi dhidi ya Ukawa," alisema.
JAMES MBATIA
Mbunge wa Vunjo (NCCR-Mageuzi), James Mbatia, alisema ameshangazwa na uamuzi huo wa Naibu Spika huku akiuita ni wa jazba.

"Mimi nimekuwa kwenye siasa kwa miaka zaidi ya 25. Kilichofanywa na Naibu Spika sasa ni kudhalilisha wabunge, ionekane sasa eti tupo hapa kwa ajili ya kulipwa posho. Tupo hapa kwa ajili ya kutoa huduma kwa Watanzania. Kina Tulia wakiwa Shule ya Msingi, sisi tunapambana bila kulipwa posho na mtu yeyote," alisema Mbatia.
DK. ALLY YUSUF SULEIMAN
Mbunge wa Mgogoni (CUF), Dk. Ally Yusuf Suleiman, alisema uamuzi wa Dk. Ackson una tatizo kwa sababu "anaonekana kujichanganya."

"Awali alisema Bunge litalazimika kubadili kanuni za malipo ya posho ili ziruhusu kutowalipa wabunge wanaosaini mahudhurio bila kushiriki vikao, lakini jana (juzi) kaja na uamuzi mwingine. Sijui uamuzi huo kautoa wapi," alisema.
Mbunge huyo alidai kuwa wabunge wa CCM ndiyo wanaoongoza kwa kukacha vikao vya Bunge, hivyo kuna haja ya kuziboresha zaidi kanuni za malipo ya posho za wabunge kwa kuwa wabunge wengi wa chama hicho tawala hawashiriki kikamilifu vikao vya Bunge hilo.
"Bado mimi nalaumu hata Ofisi ya Spika kutowaita viongozi wa Ukawa na kulimaliza hili suala kwa busara. Ninachokiona hapa Naibu Spika sasa anatumia mabavu tu," alisema.
SUSAN LYIMO
Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Susan Lyimo, alisema wataendelea kutoshiriki vikao vyote vinavyoongozwa na Dk. Ackson hadi pale haki itakapopatikana.

"Hoja yetu si posho. Posho zao hata hazitubabaishi, tutasimamia msimamo wetu, akiwapo Naibu Spika tutatoka ndani ya Ukumbi wa Bunge bila kuziangalia hizo posho," alisema.
LUCIA MLOWE
Mbunge mwingine wa Viti Maalum (Chadema), Lucia Mlowe alisema: "Tuliacha posho ya Sh. milioni 30 ya Bunge la Katiba, hoja hapa si posho. Tunataka utawala bora ndani ya Bunge."

DAVID SILINDE
Mbunge wa Momba (Chadema), David Silinde, alisema uamuzi uliofanywa na Naibu Spika uko kinyume cha Kanuni za Kudumu za Bunge toleo la Januari 2016.

Mbunge huyo alisema Kanuni za Kudumu za Bunge zinasema Mbunge aliyesaini mahudhurio bungeni, anapaswa kulipwa posho.
"Hata wasipotulipa, hatutarudi nyuma katika uamuzi wetu. Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, alitangaza Jumatatu ya wiki iliyopita kuwa kuwa upinzani hauna imani na Naibu Spika na hautakuwa tayari kushiriki vikao anavyoviongoza hadi haki itakapopatikana.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment