KIONGOZI
wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Askofu Josephat Gwajima, amefunguka kwa
kuelezea safari yake aliyoifanya nje ya nchi hivi karibuni, baada ya
taarifa mbalimbali kudai kuwa alilikimbia Jeshi la Polisi.
Akiongoza
ibada kanisani kwake, Ubungo, jijini Dar es Salaam jana, Askofu Gwajima
alisema aliondoka nchini kwenda Japan Juni 15, mwaka huu, kwa ndege ya
Emirates.
Akitoa mahubiri katika ibada jana, Gwajima alisema alifika
mjini Osaka Juni 16 na kuanza mkutano wa kuhubiri injili na siku
zilizofuata alikwenda katika miji mbalimbali.
Askofu Gwajima ambaye
aliingia kanisani hapo saa 5:00 asubuhi na kuanza kuhubiri dakika 15
baadaye, asubuhi alitumia muda wa saa tatu hadi saa 8:20 kumaliza
mahubiri yake.
Baada ya kuanza kuhubiri, alielezea safari hiyo kwa
kutaja miji aliyekwenda ikiwamo Nagoya alikohubiri kwa siku mbili,
Karuizawa, Ibaraki, Hiloshima na Yanakochi.
“Safari yangu ilikuwa ya
mafanikio sana. Tulisafiri salama na kuzunguka miji mbalimbali na
tulirudi Jumatatu ya wiki iliyopita,” alisema Askofu Gwajima.
Kadhalika,
katika mahubiri hayo, Gwajima aliwakumbusha waumini wa kanisa hilo
kuhusu kuhama kwa kanisa hilo, kwa kuwatajia siku ya mwisho ya kumalizia
michango kwa ajili ya ujenzi wa kanisa jipya kuwa ni Julai 30, bila ya
kutaja sehemu ambayo kanisa hilo litahamia.
Hata hivyo, Askofu Gwajima wakati wote wa mahubiri, hakuzungumzia suala la kuhojiwa kwake na Jeshi la Polisi.
Wakati
huo huo, mwandishi alizungumza na Msaidizi wa Askofu Gwajima, Yekonia
Bihagaze, kuhusu tetesi za kufungiwa kwa kanisa hilo na kusema taarifa
hizo si za kweli bali ni maneno ya mitaani.
“Hayo maneno si ya kweli.
Si umeona ibada imeendelea kama kawaida na Askofu amehubiri? Maneno ya
mtaani usiyalete kanisani,” alisema Bihagaze.
Julai 12, mwaka huu,
Kikosi cha Polisi cha Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA)
kilimkamata Askofu Gwajima wakati akitokea Japan kwa kutumia ndege ya
Shirika la Ndege la Kenya.
Baada ya kukamatwa, alipelekwa moja kwa
moja Kituo Kikuu cha Polisi kwa ajili ya kuhojiwa, akidaiwa alitoa
maneno ya uchochezi mwezi uliopita.
Jeshi la Polisi lilikuwa
likimtafuta Askofu Gwajima baada ya kusambazwa mkanda kwenye mitandao ya
kijamii unaodhaniwa una sauti yake.
Katika mkanda huo, Gwajima
anapendekeza Rais mstaafu Jakaya Kikwete afikishwe mahakamani kwa yote
yaliyofanyika wakati wa utawala wake, ambayo kwa sasa Rais Magufuli
anayashughulika kwa staili ya utumbuaji majipu.
Pia Gwajima alisikika
akimshauri Rais John Magufuli, kuhama Chama Cha Mapinduzi (CCM) iwapo
watakataa kumkabidhi uenyekiti na kwamba apeleke muswada bungeni,
kuondoa kinga ili rais ashtakiwe kwa makosa aliyoyafanya akiwa
madarakani.
Tangu kusambaa kwa mkanda huo, Jeshi la Polisi lilikuwa
likipiga kambi katika moja ya nyumba za Askofu Gwajima, iliyoko Mbezi
Salasala jijini Dar es Salaam.
Pamoja na kupiga kambi, jeshi hilo halikufanikiwa kumkamata na baadaye ilielezwa kuwa amekwenda nje ya nchi kuhubiri.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment