Image
Image

Chenge awazidi kete Polisi,akaidi agizo la mikutano ya hadhara.

Agizo la Jeshi la Polisi nchini la kusitisha kufanyika kwa mikutano ya hadhara ya kisiasa imeonekana kutoathiri ratiba za Mbunge wa Bariadi, John Chenge ambaye ameendelea na mikutano ya hadhara jimboni kwake.
Taarifa kutoka jimboni humo zimeeleza kuwa Chenge amekuwa akifanya mikutano ya hadhara katika vijiji mbalimbali na Alhamisi iliyopita alianza na eneo la Buchani, mkutano uliomalizika salama bila kuwepo kizuizi chochote.
Katika mikutano hiyo, Mtemi Chenge ameendelea kuwasisitiza wananchi wake kupuuza kauli za kisiasa zinazotolewa na wapinzani wake bali waangalie namna anavyotekeleza ahadi alizozitoa kwenye kampeni za uchaguzi mkuu.
Mikutano hiyo ya Chenge hutanguliwa na matangazo yanayofanywa kwa kutumia magari yenye vipaza sauti katika eneo husika.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Onesmo Lyanga alipotafutwa kwa njia ya simu alisema kuwa yeye hahusiki kutoa vibali vya mikutano na kwamba mhusika ni Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD). Hata hivyo, OCD hakupatikana kwa wakati.
Hali hiyo imedaiwa kuzua manung’uniko kwa vyama vya upinzani mkoani humo ambavyo vimeshindwa kufanya mikutano ya hadhara kutokana na kuwepo kwa zuio la Mikutano hiyo nchi nzima.
Mwezi uliopita, Kamishna wa Jeshi la Polisi, Operesheni ya Mafunzo, Nsato Msanzya alitangaza kupiga marufuku kufanyika kwa mikutano ya kisiasa kwa sababu za kiusalama.
“Polisi kupitia vyanzo vyake mbalimbali, imebaini kuwea mikutano hiyo ina lengo la kuwahamasisha wananchi kutotii sheria za nchi,” alisema Kamishna Nsato.
Kufuatia agizo hilo, Jeshi la Polisi lilizuia kufanyika kwa mikutano iliyokuwa imepangwa na Chadema na ACT-Wazalendo
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment