MKUU
wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali, Ernest Mangu amefunguka kuhusu
mambo juu ya utendaji wa jeshi hilo na kueleza kuwa wakati wowote
litamburuza mahakamani Katibu Mkuu wa Taifa wa Chama cha Wananchi (CUF),
Maalim Seif Shariff Hamad kwa kuhamasisha uchochezi visiwani Zanzibar
Amebainisha
kuwa jeshi hilo, kamwe halikandamizi wala kuonea chama chochote cha
siasa, kwani limekuwa likitekeleza wajibu wake kwa kufuata sheria na
taratibu zilizopo.
Akizungumza katika mahojiano yaliyofanyika kwenye
kipindi cha Funguka, kinachorushwa na Kituo cha Televisheni ya Azam
jana, IGP Mangu alisema hali ya siasa Zanzibar ilikuwa shwari katika
chaguzi zote mbili na kwamba machafuko na vurugu vilianza kutokea baada
ya uchaguzi wa pili.
Alisema vurugu hizo zilianza baada ya kubainika
kuwa Maalim Seif, alikuwa akifanya mikutano ya ndani na mingine ya chini
kwa chini na wafuasi wake katika maeneo ya Kaskazini na Kusini.
“Kwa
sababu ilikuwa ni mikutano ya ndani, Polisi hatukuona tatizo na wala
hatukumzuia, tuliona ni mwananchi anataka kuzungumza na wafuasi wake,
tukasema mwache aongee nao tu,” alisema IGP Mangu.
Alisema baadaye
jeshi hilo liligundua kuwa kiongozi huyo wa CUF, alikuwa anawachochea
wananchi waichukie serikali iliyopo madarakani na wapinzani wao ambao ni
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuwafanyia uhalifu.
Alisema baada ya
vikao hivyo vya Maalim Seif, visiwani humo kukaanza kuibuka matukio ya
vurugu kama vile mashamba kuchomwa moto na mazao kung’olewa.
“Haya mambo hayakutokea kabla ya vikao vya Seif, yalitokea baada ya vikao vyake,” alifafanua mkuu wa polisi.
Alisema
wafuasi hao walichochewa, kiasi cha kususa hadi shughuli za kijamii,
kama vile misiba na wakati mwingine ilifikia hatua ya kususa kuwauzia
bidhaa wafuasi wa CCM.
“Tukasema kama wameona kugeuza biashara zao
siasa, basi waendelee tu. Biashara inadumu kwa sababu unatengeneza
faida, sasa kama umeamua kuchagua wa kumuuzia ni shauri yako. Hawa
tuliwaacha kwa sababu tuliona hawana makosa,” alisema.
Hata hivyo,
alisema jeshi hilo kamwe halikuwanyamazia wahalifu waliochoma na kung’oa
mazao kwenye mashamba ya wenzao, eti tu kwa kigezo cha ufuasi wa chama
au siasa.
“Hawa tuliwakamata na wapo wengine tunaendelea kuwatafuta,
watakapoacha ndio hatutawatafuta. Wale wahalifu ndio tunaowatafuta.
Pengine kwa sababu ya siasa wanadhani Polisi tunawaonea wananchi
tunawakamata bila sababu. Sasa hawa watu tunawaoneaje wakati
tunawapeleka mahakamani?” Alihoji.
Maalim Seif kuhojiwa
Alisema
kutokana na matukio hayo, tayari Maalim Seif amehojiwa na jalada lake
halijaamuliwa, lipo kwa Mwendesha Mashtaka wa Serikali (DPP) Zanzibar.
“Lakini pia tunataka tumpeleke mahakamani kumshitaki kwa makosa
aliyofanya ya kuchochea fujo,” alieleza.
Alisema kazi kubwa ya Polisi
kwa sasa si kujiingiza kwenye siasa au kupatanisha pande mbili
zinapokwaruzana, bali kazi yake ni kuhakikisha inadhibiti na kuwakamata
wahalifu.
Alisema endapo vyama viwili vinavyolumbana visiwani
Zanzibar, vitaamua kuchukua hatua za kisheria kumaliza tofauti zao,
polisi haina tatizo, lakini endapo vyama hivyo vitachukua hatua za
kijinai au kukomoana, jeshi hilo halitokaa kimya.
“Kazi ya polisi iko
wazi, tunakamata tunapeleleza na kupeleka mahakamani umma unatuona
tunachofanya hatuna cha kuficha,” alisisitiza.
Maandamano na mikutano
Akizungumzia
madai ya jeshi hilo kukandamiza demokrasia na wapinzani kwa kudhibiti
shughuli za siasa nchini, IGP Mangu alisema hakuna mwanasiasa au chama
chochote, kilichozuiwa kufanya shughuli zake, ikiwemo mikutano.
Alisema
kinachotakiwa ni kwa mwanasiasa au chama hicho, kupeleka maombi yake
Polisi kwa mujibu wa sheria na baada ya jeshi hilo kufanyia tathmini
maombi hayo, endapo yataonekana hayana tatizo yataruhusiwa kuendelea.
Alisema
endapo jeshi hilo linazuia shughuli za kisiasa, hutokana na uchunguzi
au tathmini lililofanya na kujiridhisha kuwa shughuli husika si salama
na inatishia usalama wa raia.
“Unajua unapozungumzia masuala hayo
tuwe makini kidogo, kwa sababu hapa kuna watu wa aina mbili kuna
wanaofanya siasa na sisi watendaji tunaotekeleza sheria. Ila sisi pia
hatuko juu ya sheria, kama kuna mahali tunakiuka upo utaratibu wa
kutushughulikia,” alisisitiza.
Alisema hata katika suala la kuzuia
shughuli za kisiasa, kama vile mikutano na maandamano endapo, kuna chama
au mwanasiasa anahisi kuwa jeshi hilo, halikutenda haki au limeenda nje
ya mstari, taratibu zinamruhusu kukata rufaa kwa Waziri wa Mambo ya
Ndani ya Nchi, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Rais na Mahakama.
Hata
hivyo, alisema jeshi hilo halifanyi jambo lolote nje utaratibu wa
kisheria, akifafanua, “lakini sisi hatuwezi kujiingiza kwenye siasa kwa
sababu sisi sio wanasiasa, pia hatuwezi kuzuia wanasiasa kulumbana kwa
sababu ni uwanja wao wa kulumbana. Sasa kama tulitoa maelekezo fulani
basi ujue tulikuwa tunatekeleza sheria na utaratibu uliopo.”
“Sidhani
kama sisi tunakandamiza upinzani, tunachofanya sisi ni kufuata sheria
na taratibu zilizowekwa na watu wako huru kama wanafikiri tumeenda nje
ya mipaka yetu wakatuchukulie hatua,” alisisitiza.
Alitoa mfano wa
matukio yaliyozuiwa na Polisi kwa sababu za kiusalama kuwa ni pamoja na
mkutano wa mahafali wa Dodoma, ambao ulifanyika siku moja na mkutano wa
mahafali uliofanyika Ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam ambao wenyewe
haukuzuiwa. Yote ilikuwa mikutano ya wanafunzi wafuasi wa Chadema.
“Kama
sisi tuna sera ya kuzuia, mbona wa Karimjee hatukuuzuia? Dodoma
kulikuwa na sababu na imeelezwa na viongozi wa Dodoma. Hii si sera yetu,
usichukulie mkutano mmoja kuzuiwa basi ndio yote nchi nzima imezuiliwa.
Haiwezekani,” alifafanua.
Alisema sheria inazungumzia wanaohitaji
kufanya mkutano au kufanya maandamano, wanatoa taarifa kwa mkuu wa
polisi wa hilo eneo, na mkuu huyo ataangalia kama mazingira yanaonesha
hakuna tatizo, mkutano utaendelea, kama kuna tatizo atauzuia.
“Sasa
ni wapi sisi tumefanya kitu ambacho ni kinyume na tunaonekana
tunakandamiza upinzani? Na ikumbukwe kuwa kuna mikutano baadhi iliombwa
tukaizuia kwa sababu kipindi hicho kulikuwa na kelele za mauaji Mwanza,
Sengerema, Tanga mpaka tunahojiwa Polisi mko wapi,” alisema.
Alisema wakati Polisi ikihojiwa kuhusu dawa ya mauaji, baadhi ya vyama viliwasilisha maombi ya maandamano.
“Hivi
kweli? Kwanza mauaji yenyewe mtindo wake ni mpya unajuaje kama
wanaoomba wangeenda nao kuvamiwa? Lazima tuchukue tahadhari,” alisema na
kuongeza kuwa Polisi imepewa jukumu la kisheria kuhakikisha panakuwepo
na amani.
“Sasa tunapochukua hatua kuhakikisha kuna amani, naomba
tuvumiliane. Msione kuna amani, basi mkajua ipo tu na ni ya kudumu, mjue
kuna wengine wameumia kuhakikisha hiyo amani inakuwepo. Lazima iwe
hivyo ndio utaratibu wa kuongoza nchi, sisi hatubagui wala kukandamiza
chama chochote,” alieleza IGP Mangu.
Matumizi ya nguvu
IGP Mangu
alisema si kweli jeshi hilo limekuwa likitumia zaidi nguvu katika
kudhibiti vurugu na kubainisha kuwa nguvu hutumika, pale tu inapobainika
kuwa upande wa pili unaodhibitiwa nao unatumia nguvu.
Hata hivyo,
alisisitiza kuwa Polisi nchini imekuwa ikitekeleza wajibu wake vyema
bila kukandamiza wala kutumia nguvu, kwani hata taasisi ya kimataifa
iliyofanya tathmini juu ya utendaji wa jeshi hilo katika uchaguzi mkuu
nchini ilibainisha kuwa jeshi hilo lilifanya vyema.
Polisi na rushwa
Akizungumzia
tuhuma zinazorushiwa Jeshi la Polisi kwamba kuna baadhi ya askari wake,
wanatuhumiwa kwa rushwa, alisema askari hawana mamlaka ya kula rushwa
na kujilimbikizia mali halafu wasiguswe na mtu.
“Hili haliwezekani.
Kwa hiyo nasema bado wananchi wanaweza wakasaidia kama kweli wanazo
taarifa za Polisi na zitafanyiwa kazi. Kama hawaamini kama sisi wenyewe
hatuwezi kudhibitiana, vipo vyombo vingine vinaweza kufanya hivyo,”
alisema.
Hata hivyo, alisema wapo askari Polisi wenye maisha mzuri
kwa maana ya nyumba na magari, ambao wamepata mali hizo kupitia taasisi
mbalimbali za mikopo ikiwemo Saccos ya Polisi, ambayo ndio kubwa nchini.
“Askari
polisi kumiliki gari nzuri si kosa, la msingi amepataje hilo gari, kama
kuna polisi ana mali au gari isiyo na maelezo tuleeteni, polisi
hazuiliwi kuwa na gari nzuri. Siku hizi kuna taasisi nyingi zinakopesha
anaweza kukopa,” alisisitiza.
Kashfa ya Lugumi
Akizungumzia suala
la kashfa ya mkataba tata wa Kampuni ya Lugumi Enterprises Ltd
inayomilikiwa na mfanyabiashara Said Lugumi, IGP Mangu alisema suala
hilo lilichukuliwa na Bunge na kufanyiwa uchunguzi hivyo, matokeo ya
uchunguzi hawezi kuyazungumzia.
Alisema anachoweza kukizungumzia ni
maelekezo ambayo jeshi hilo limepatiwa na Bunge, ambayo ni kukamilisha
yale ambayo hayajakamilishwa.
“Tunaendelea kuchukua hatua za
kukamilisha.Kuhusu uchunguzi kazi ilifanywa na Bunge kwa anayetaka
anaweza kuwasiliana na Bunge na kupatiwa matokeo kwa kuwa naamini Bunge
linawakilisha wananchi, taarifa zao ziko wazi,” alisema.
Home
News
Slider
Jeshi la Polisi Tanzania Kumburuza Maalim Seif Mahakamani Muda wowote kuanzia sasa.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment