HATIMA
ya nani atakuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ipo mikonini
mwa mwenyekiti mtarajiwa Rais Dk. John Magufuli, ambaye sasa yupo mbioni
kukabidhiwa mikoba ya chama hicho.
Nafasi hiyo kwa sasa inashikiliwa
na Katibu Mkuu anayemaliza muda wake, Abdulrahman Kinana, ambaye
ameshika nafasi hiyo tangu Novemba, 2012.
Jana Msemaji wa CCM,
Christopher ole Sendeka, alisema hadi sasa maandalizi yanakwenda vizuri
na tayari wajumbe wataanza kuwasili mjini Dodoma mapema wiki hii, kwa
ajili ya Mkutano Mkuu utakaofanyika Julai 23, mwaka huu.
“Suala la
nani ni Katibu Mkuu litaamuliwa na mwenyekiti mpya Dk. John Magufuli,
baada ya kukabidhiwa chama na Rais mstaafu Jakaya Kikwete. Tunataraji
wajumbe 2,465 watahudhuria na hata wakipungua basi ni kidogo,” alisema
Msemaji
huyo wa CCM alisema kuwa baada ya Julai 23, kutakuwa na kikao cha
Halmashauri Kuu ambacho ndicho kitaamua juu ya mapendekezo ya mwenyekiti
mpya kama anabadili sekretarieti au laa.
“Kwa sasa Katibu Mkuu bado
ni Kinana hivyo sasa hapo ndipo kuna kitandawili ambacho kitateguliwa na
mwenyewe Rais Magufuli kama ataendelea na aliyepo sasa au atakuja na
mtu mwingine,” alisema Sendeka.
Alipoulizwa kuhusu kuibuka kwa kundi
la watu wanaompinga Rais Magufuli, asipigiwe kura kwa ajili ya
kukabidhiwa chama, alisema hakuna kitu kama hicho zaidi ya taarifa hizo
kuenezwa kwenye mitandao ya kijamii.
“Suala la kuwepo kwa watu
kumpinga Rais Magufuli asikabidhiwe chama si geni, ingawa hadi sasa
hatujaweza kumfahamu mwanachama yeote anayeendesha mpango huu.
“Mambo
haya nahisi kuna kikundi cha watu kinajifurahisha katika mitandao ya
kijamii hivi inawezakana vipi wajumbe walewale waliomchagua Magufuli awe
mgombea wa CCM eti leo hii wageuke na kumpinga?
“… hili si kweli na
si geni kama unakumbuka hata mwaka 2002 wakati mzee Benjamin Mkapa
anawania uenyekiti kwa mara ya pili mambo kama haya yalijitokeza na wale
waliokuwa wanatajwa walikanusha na haohao ndiyo wakawa mstari wa mbele
kuhakikisha wanatafuta kura za kutosha,” alisema Sendeka.
Hata hivyo
hadi sasa bado Kinana amekuwa akipewa nafasi ya kuendelea kuwa katibu
mkuu ingawa mwenyewe amekuwa akitajwa na watu wake karibu kuwa anahitaji
kupumzika.
Polisi wachimba mkwara
Akizungumza kwa niaba ya
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa, Mrakibu Mwandamizi
wa jeshi hilo mkoani hapa Mayala Towo, alisema polisi wamejipanga
kuufanya Mkoa wa Dodoma kuwa kisima cha amani wakati wote na baada ya
Mkutano Mkuu wa CCM.
“Amani itakuwepo wana Dodoma na Watanzania
wasiwe na wasiwasi ukija na nia mbaya tutakachokufanya utawasimulia
wenzako kwani kwetu amani ni wajibu wetu,” alisema Mayala.
Alitoa
angalizo kwa wale watakaopokea na kuwaweka wageni katika nyumba zao
ambao lengo lao ni kufanya fujo kuwa jeshi hilo litawachukulia hatua
kali za kisheria.
“Usiwe sehemu ya tatizo, kama unampokea mtu na
kumweka kwako ili aje afanye vurugu wa kwanza kuchukuliwa hatua utakuwa
wewe mwenye nyumba,” alisema.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment