ALIYEKUWA
Mkurugenzi Mtendaji wa wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Ephraim
Mgawe,ameshangaa kutoshtakiwa kwa aliyekuwa Waziri wa Fedha katika
Serikali ya awamu ya nne, Mustapha Mkulo pamoja na Waziri wa Uchukuzi
Omary Nundu kwa sababu walishiriki makubaliano ya ujenzi wa gati namba
13 na 14 katika Bandari ya Dar es Salaam.
Mgawe aliyasema hayo jana
wakati akitoa ushahidi wake katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele
ya Hakimu Mfawidhi, Cyprian Mkeha katika kesi inayomkabili, Mgawe
alidai kuwa katika kipindi hicho, hakuvunja Sheria ya Ununuzi wa Umma
kwa vile alisaini mkataba wa makubaliano ya biashara na Kampuni ya
China Communication Construction Company Limited (CCCCL) kutokana na
masharti ya mkopo kutoka Benki ya Exim ya China.
Mgawe na aliyekuwa
Naibu wake, Hamad Koshuma, wanakabiliwa na kesi ya matumizi mabaya ya
madaraka, kwa kutoa zabuni kwa kampuni ya CCCCL kwa ajili ya ujenzi wa
Gati 13 na 14 katika Bandari ya Dar es Salaam.
Huku akiongozwa na
wakili wake, Frank Mwalongo, Mgawe alieleza kwamba TPA ilitangaza zabuni
ya kutafuta kampuni ambayo ingefanya kazi ya upembuzi yakinifu kwa
ajili ya ujenzi wa gati hizo na katika mchakato wa awali Kampuni ya CPCS
ya Canada ilishinda zabuni hiyo.
Alidai kampuni hiyo baada ya
kufanya upembuzi yakinifu ilibaini kwamba ujenzi wa gati hizo
ungegharimu Dola za Marekani milioni 321 (sawa na Sh bilioni 67.2) na
kupendekeza ujenzi huo uwe wa ubia na kwamba TPA inatakiwa kugharamia
uchimbaji wa gati hizo.
Alidai baada ya ripoti hiyo ya upembuzi
yakinifu kutolewa,TPA haikuwa na fedha za ujenzi na ndipo ikaanza
kutafuta fedha katika benki mbalimbali na kupatikana Kampuni ya CCCCL
ambayo ilisema ingewezesha kufanikisha upatikanaji wa Mkopo huo.
Alieleza
kwamba katika upembuzi yakinifu uliofanywa na Kampuni ya CCCCL
ilibainika kwamba gati hizo mbili zingejengwa kwa gharama ya dola za
Marekani milioni 500 (sawa na Sh billion 10.2) na kwamba mkopo huo
ungepatikana katika Benki ya Exim ya China.
“Ripoti hiyo pia ilieleza
kwamba lazima mkopo huo upate dhamana ya serikali na serikali kupitia
Hazina walitueleza kwamba wapo tayari kutudhamini na Septemba 2011
Wizara ya Uchukuzi ilituruhusu tufuatilie mkopo katika Benki hiyo,”
alidai Mgawe.
Alidai mwishoni mwa Novemba 2011 wakiwa na aliyekua
Waziri wa Uchukuzi, walikwenda China kwa ajili ya kuonana na uongozi wa
Benki ya Exim kufuatilia mkopo huo ambako walikutana na Makamu
Mwenyekiti wa benki hiyo ambaye aliwahakikishia mkopo wa Dola za
Marekani 500 kwa ajili ya ujenzi wa gati hizo.
Alidai walipofika
nchini humo, walitakiwa kuandika barua rasmi ya kuomba mkopo huo ambao
ungedhaminiwa na serikali, ndipo ilipofika mwaka 2012 aliyekua Waziri wa
Fedha, Mustapha Mkulo aliandika barua hiyo na kuambatanisha na barua ya
makubaliano ya kibiashara kati ya TPA na kampuni ya CCCCL.
Alidai
baada ya kuandikwa kwa barua hiyo, alisaini makubaliano ya kibiashara
na CCCCL kutokana na matakwa ya Benki ya Exim kwa sababu ndiyo kampuni
iliyofanya upembuzi yakinifu wa ujenzi wa gati hizo mbili na mkataba
huo unatambua mkopo kati ya benki ya Exim ya China na Serikali ya
Tanzania,” alidai Mgawe.
Alifafanua zaidi, Mgawe aliieleza mahakama
hiyo kuwa katika kipindi hicho, TPA ilikuwa haina fedha za ujenzi, hivyo
walilazimika kutafuta mkopo kuhakikisha kazi hiyo inafanyika.
Aliiomba
mahakama hiyo kumwachia huru kwa madai kuwa, hajavunja sheria ya
manunuzi na kwamba mchakato huo ulihusisha viongozi mbalimbali wa
serikali wakiwamo mawaziri hao.Source:MTANZANIA.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment