UBADHIRIFU
wa fedha na ukiukwaji wa taratibu na sheria katika usimamizi wa miradi
kadhaa ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), vimeelezwa kuwa
miongoni mwa sababu za kusimamishwa kazi wakurugenzi sita na mameneja
watano wa shirika hilo.
Vigogo hao walisimamishwa kazi juzi na Bodi
ya Wadhamni ya NSSF inayoongozwa na mwenyekiti wake, Profesa Samwel
Wangwe, kupisha uchunguzi kuhusu tuhuma za ubadhirifu, matumizi mabaya
ya ofisi na kutofuata kanuni, sheria na taratibu katika uwekezaji,
usimamizi wa miradi, ununuzi wa ardhi na ajira katika shirika hilo.
Waliosimamishwa
ni Mkurugenzi wa Mipango, Uwekezaji na Miradi, Yacoub Kidula,
Mkurugenzi wa Fedha, Ludovick Mrosso, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na
Utawala, Chiku Matessa na Mkurugenzi wa Udhibiti, Hadhra na Majanga,
Said Shemliwa.
Wengine ni Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Hesabu za Ndani, Pauline Mtunda na Mkurugenzi wa Uendeshaji, Cresentius Magori.
Mameneja waliosimamishwa ni Meneja Utawala, Amina Abdallah, Meneja wa Uwekezaji, Abdallah Mseli na Meneja wa Miradi, John Msemo.
Wengine ni Mhasibu Mkuu, John Davis Kalanje, Meneja Kiongozi Mkoa wa Temeke, Wakili Chedrick Komba na Meneja Miradi, John Ndazi.
Inaelezwa
kuwa baadhi ya ubadhirifu huo ulifanywa kupitia miradi ya usimamizi wa
nyumba za kuuza zilizopo Mtoni Kijichi, Dar es Salaam, unaokadiriwa
kufikia Sh bilioni 137.7.
Katika ripoti ya mwaka ya Mkaguzi na
Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kuhusu ukaguzi wa mashirika
ya umma kwa mwaka wa fedha 2014/2015, imebainika kuwa ulikuwapo
ukiukwaji mkubwa wa taratibu katika miradi hiyo.
Taarifa hiyo ya CAG
inaeleza katika ukurasa wa 165 na 166 kuwa Juni 30 mwaka 2015, Sh
bilioni 79 za shirika hilo zilitumika katika ujenzi wa nyumba hizo
ambazo ziliamuriwa kuuzwa ndani.
Uamuzi huo ulitolewa badala ya
kufuata maelekezo ya wasimamizi kwa kutumia benki au makampuni ya mikopo
kama ilivyoelekezwa katika kanuni namba 13 ya Mamlaka ya Udhibiti wa
Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) na mwongozo wa uwekezaji wa Benki Kuu
ya Tanzania (BoT).
Katika maoni yake kuhusu mradi huo, ofisi ya CAG
iliishauri menejimenti ya NSSF kuzingatia sheria, kanuni na maelekezo
yanayotolewa na wasimamizi wake.
“Kitendo chochote cha kutofuata
maagizo kinatakiwa kuwasilishwa kwa maandishi kwa mdhibiti wa sekta na
kukubaliana muda uliopangwa kwa ajili ya kufuatwa,” ilisema sehemu ya
ripoti hiyo.
Ukiukwaji mwingine wa sheria na taratibu unaotajwa
kufanywa na vigogo hao, ni ununuzi wa ardhi bila ushindani kutoka kwa
muuzaji mmoja, kwa gharama ya Sh bilioni 15.16.
Taarifa hiyo ya CAG
inaeleza kuwa NSSF ilipanga bajeti ya Sh bilioni 1.6 kwa ajili ya
ununuzi wa kiwanja kupitia zabuni za ushindani.
“Hata hivyo, ilitumia
chanzo kimoja katika ununuzi wa kiwanja kilichogharimu Sh bilioni
15.16. Nimegundua kwamba Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma
haikujulishwa, kinyume cha kanuni namba 87 ya mwaka 2013 ya mamlaka hiyo
inayohitaji kuwasilishwa taarifa za mkataba wa tuzo kwake, ndani ya
siku saba kuhusu mchakato wa ununuzi endapo chanzo kimoja kilitumika,”
inasomeka sehemu ya ripoti hiyo ya CAG.
CAG aliishauri menejimenti ya
NSSF kuzingatia mpango wake wa bajeti na kanuni za ununuzi wa umma za
mwaka 2013, kuhakikisha ununuzi unafanyika katika ushindani ili kupata
huduma kwa bei nafuu.
Kutokana na hali hiyo, katika ripoti hiyo ya
ukaguzi, CAG alieleza namna NSSF lilivyoingia ubia na Kampuni ya Azimio
Housing Estate kuanzisha kampuni maalumu kwa jina la Hifadhi Bulders
Limited.
Katika mkataba huo, Azimio Housing Estate inatakiwa
kuendeleza ekari 20,000 za ardhi zilizopo Kigamboni ambapo kwa hatua ya
awamu itaaanza na ekari 300.
“Katika ubia huu, Shirika la Taifa la
Hifadhi ya Jamii linamiliki asilimia 45 ya hisa wakati Azimio Housing
Estate inamiliki asilimia 55. Jumla ya gharama za mradi ni dola za
Marekani milioni 653.3.44.
“Ukaguzi wa hatimiliki umeonyesha kuwa
Azimio Housing Estate inamiliki viwanja viwili, kiwanja chenye
hatimiliki namba 81828 chenye ukubwa wa hekta 1.98 na chenye hatimiliki
namba 105091 chenye ukubwa wa hekta 114.11 ambavyo vyote vinapatikana
katika eneo la Rasi Dege,” ilieleza taarifa ya CAG.
Pamoja na hali
hiyo, CAG alisema kuwa hajaweza kupatiwa hatimiliki za ardhi ambayo
Azimio iliahidi kutoa kama uchangiaji wa mtaji hali ambayo NSSF ililipa
asilimia 20 ya fedha kama mtaji ambazo zilikuwa kwenye hatari ya
kupotea.
Licha ya kuibuliwa kwa hili, CAG alieleza kuwa Menejimenti
ya NSSF ina udhaifu katika mifumo ya kifedha na kiuhasibu. Kwamba wana
mfumo mkuu wa usimamizi wa rasilimali ambao unaweza kuunganishwa na
mfumo wa usimamizi wa fedha ambao unakosa moduli ya uhasibu kwa ajili ya
kuhifadhi taarifa za kifedha.
DENI LA BIL 723.22
Katika taarifa
hiyo ya CAG, inaelezwa kuwa NSSF iliikopesha Serikali katika miradi yake
mbalimbali, lakini hata hivyo imekuwa hailipi madeni yake kwa muda
mrefu.
Kwamba hali hiyo imekuwa ikisababisha kuongezeka kwa limbikizo
la riba na adhabu hadi kufikia asilimia 39 ya salio la Sh bilioni
729.22 kufikia Juni 2014.
WAFANYAKAZI NA MADENI
Shirika hilo lina
utaratibu wa ndani wa kutoa mikopo kwa wafanyakazi wake, na ukaguzi
umeonyesha kiasi cha Sh milioni 827.98 bado kinadaiwa kwa wafanyakazi
ambao si waajiriwa tena wa NSSF.
Mwanzoni mwa mwaka huu, Rais John
Magufuli alitengua uteuzi wa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Dk.
Ramadhani Dau na kumteua kuwa balozi ingawa hadi sasa hajapangiwa nchi
ya kwenda.
Vilevile, mwanzoni mwa Machi mwaka huu, mrithi wa Dk. Dau,
Dk. Carine Wangwe ambaye aliteuliwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri
Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista
Mhagama, uteuzi wake ulitenguliwa na Ofisi ya Rais Ikulu katika kile
kilichoelezwa kuwa ulikiuka taratibu.
KUHOJIWA TAKUKURU
Wakati
huohuo, taarifa zilizoifikia MTANZANIA jana, zilisema vigogo hao
wameanza kuhojiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru)
kuhusu suala hilo.
Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Valentino Mlowola,
alipotafutwa kuzungumzia suala hilo, alisema yuko nje ya ofisi na
akashauri atafutwe msemaji wa taasisi hiyo, Mussa Misalaba.
Hata hivyo, Misalaba alipoulizwa, alisema hana taarifa na jambo hilo kwa sababu hakuwa ofisini.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment