SERIKALI
inatarajia kukusanya sh. bilioni 200 kwa mwaka, ikiwa ni mapato ya kodi
baada ya kukamilika kwa ujenzi wa kiwanda cha kimataifa cha Kiluwa
Steel Group kitakachokuwa na uwezo wa kuzalisha tani 3,000 za nondo kwa
siku.
Awamu ya kwanza ya ujenzi wa kiwanda hicho kinachomilikiwa na
mwekezaji mzawa kwa kushirikiana na Wachina, inatarajiwa kukamilika
Oktoba, mwaka huu ambapo fedha hizo zitapatikana baada ya kukamilika
awamu tatu za ujenzi wake.
Akizungumza mbele ya Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa aliyetembelea kiwanda hicho jana (Jumanne, Julai 12, 2016),
Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda hicho, Bw. Mohammed Kiluwa alisema ujenzi
huo utasaidia kuimarisha uchumi.
“Kukamilika kwa mradi huo,
kutaongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wa nchi, upatikanaji wa ajira pamoja
na kufanikisha azma ya serikali ya awamu ya tano ya kuifanya Tanzania
kuwa nchi ya maendeleo ya viwanda,” alisema.
Alisema kiwanda hicho
kitazalisha nondo kwa matumizi ya ujenzi pamoja na vifaa vingine
vinavyohusiana na bidhaa za chuma. “Lengo ni kuweza kuuza malighafi hizo
kwenye viwanda vingine vya chuma nchini na nchi jirani kwa kuzingatia
ubora unaokidhi mahitaji ya soko la kimataifa,” alisisitiza.
“Katika
awamu ya kwanza ya ujenzi, tunatarajia kutumia dola milioni 40; awamu ya
pili tutatumia dola milioni 50 na dola milioni 200 zitatumika kwenye
awamu ya tatu ili kukamilishia ujenzi wa kiwanda hiki,” alisema.
Kiluwa
alisema, awamu ya kwanza inatarajiwa kukamilika Oktoba mwaka huu,
ambapo awamu ya tatu itakamilika Februari mwakani. Kikikamilika,
kinatarajiwa kuajiri vijana zaidi ya 500 wa Kitanzania.
Kwa upande
wake, Waziri Mkuu alisema lengo la ziara hiyo ni kukagua maendeleo ya
ujenzi wa kiwanda hicho kikubwa cha kwanza kinachojengwa na mwekezaji
mzawa.
“Uwekezaji sio lazima ufanywe na watu wa nje, Watanzania wana
nafasi ya kuwekeza katika sekta mbalimbali, Kiluwa amefungua njia hivyo
wengine wafuate nyayo zake. Uwezo tunao na sababu ya kuwekeza tunayo,
kwani tunataka tuzalishe bidhaa mbalimbali sisi wenyewe,” alisema.
Aliongeza
kuwa uwepo wa kiwanda hicho katika eneo la Disunyara, Mlandizi mkoani
Pwani, utawezesha kuboresha hali ya uchumi kwa wakazi wa eneo hilo na
Taifa kwa ujumla.
Waziri Mkuu alitolea mfano kwa wakazi wa Mtwara,
ambao wamenufaika kutokana na ujenzi wa kiwanda cha saruji cha Dangote
ambapo awali walikuwa wakinunua saruji kwa sh. 17,000, lakini hivi sasa
wanainunua kwa sh. 7,000.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu
alilitaka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) lipeleke umeme mapema
kwenye eneo hilo ili kuharakisha shughuli za uwekezaji.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)

0 comments:
Post a Comment