Image
Image

Majaliwa aigeukia wizara ya maliasili.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa, ameiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kujipanga vizuri na kufanya mapitio ya idara zake hususan ya misitu na nyuki, kutokana na kubainika kuwapo matatizo makubwa.
Majaliwa alitoa agizo hilo juzi alipokutana na watumishi wa wizara hiyo, jijini Dar es Salaam na kusisitiza kwamba hakuna sababu ya serikali kuendelea kuwa na watumishi wasio waaminifu, waadilifu na uwajibikaji.
“Eneo la misitu limekuwa na matatizo makubwa, watendaji wengi si waaminifu na sura ya wizara si nzuri miti mingi inakatwa na fedha haiingii serikalini. Huu ni mgogoro mpya,” alisema.
Alisema lengo la mkutano huo ni kukutana na watumishi kusikiliza changamoto zao, kukumbushana wajibu, pamoja na kutoa maagizo ili yatekelezwe kwa utaratibu unaokubalika kisheria.
Alisema mtumishi ambaye atabainika kuwa haitendei haki nafasi yake kwa kutokutimiza majukumu ipasavyo hana sababu ya kuwepo kwa sababu serikali inapoteza fedha nyingi kuwalipa watu wasio na tija.
Waziri Mkuu alisema sababu inayoikosesha serikali mapato ni uwapo wa watumishi wasio waadilifu kwenye ofisi za serikali ikiwemo Wizara ya Maliasili na Utalii hivyo kuna umuhimu wa kuzisafisha.
Alisema kuna uvunaji mkubwa wa misitu kuliko upandaji huku asilimia 50 ya mapato yatokanayo na uvunaji huo yanapotea na kuisababishia Serikali hasara ambapo alihoji sababu ya wizara kushindwa kusimamia jambo hilo.
Katika hatua nyingine; Waziri Mkuu aliitaka wizara hiyo kupunguza idadi ya vizuizi vya ukaguzi wa mazao ya
misitu kwenye barababara mbalimbali baada ya kukosa tija kutokana na upotevu wa misitu unaotokea kila siku.

Alitoa mfano wa barabara ya kwenda mikoa ya kusini kuanzia Dar es Salaam ambapo alisema ina vizuizi visivyopungua sita na kila kizuizi kinatumika kwa ajili ya kukagua mazao ya misitu na maliasili inayotoka kuvunwa.
“Vizuizi vya katikati ya safari havina umuhimu na badala yake kuwe na vizuizi mwanzo na mwisho ili rasilimali zingine zitumike kuongeza nguvu na umakini wa ukaguzi kwenye vituo vichache vitakavyosalia.
“Kwa mfano ukitokea Ikwiriri kuja Dar, kuna vituo vya ukaguzi wa maliasili visivyopungua sita, kuna Ikwiriri, Kibiti, Jaribu Mpakani,Mkuranga, Vikindu kote huku wanakagua lakini linapofika kituo cha mwisho cha Mbagala linakutwa na makosa kwenye mzigo kwa nini?
“Yule mkaguzi wa kwanza alifanya kazi gani? Kuna tatizo la uadilifu na ninyi ni mashahidi, sasa naagiza ongezeni nguvu kwenye vituo vikuu vya ukaguzi yaani mwanzo na mwisho,” alisema.
Aidha alisema ni muhimu kukawa na mabadiliko kwenye mfumo wa mauzo ya misitu kutoka wa sasa (kuuza kwa eneo) na kuhamia kwenye mfumo wa mnada ambao utaongeza mapato ya Taifa na utaweka uwazi.
Pia aliwataka watumie mashine za malipo za kielektroniki (EFD),wanapofanya mauzo ya mazao ya misitu ili
kuepusha matumizi ya daftari na risiti bandia ambazo hazitambuliwi na wizara.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment