Image
Image

Mzindakaya amtaka Magufuli kuwatoa mkuku wanafiki CCM baada ya kukabidhiwa kijiti.

WANASIASA mkongwe, Dk. Chrisant Mzindakaya, amemtaka Rais John Magufuli kuwanondoa wanafiki ndani ya CCM baada ya kupewa hatamu za uongozi wa chama hicho.
Sambamba na hilo, amewananga baadhi ya wanasiasa wanaoiponda serikali ya awamu ya nne, chini ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete, na kuwaelezea kuwa ni wanafiki na kwamba Magufuli anapaswa kuepukana nao.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mzindakaya alisema ana imani kwamba Rais Magufuli ayenatarajiwa kukabidhiwa uenyekiti wa chama mwishoni mwa wiki hii, atakirejesha katika heshima yake.
“Imani yangu ni kubwa sana kwamba Magufuli atakirejesha chama katika nafasi yake na kupata heshima yake kama ilivyokuwa zamani. Pamoja na imani yangu, ninashauri aondokane na wanafiki kwani hao ni sumu kwa maendeleo ya chama na serikali," alisema Mzindakaya ambaye amepata kuwa mbunge, Naibu Waziri na Mkuu wa Mkoa.
“Ninawashangaa baadhi ya wanasiasa wanaodai kuwa (Rais) Magufuli hajawahi kuwa hata mwenyekiti wa tawi ndani ya CCM. Hicho si kigezo kwa sababu ameonyesha uwezo mkubwa katika nafasi ya urais hivyo na chama atakiweza.
"Kama anafaa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM basi apewe chama nako ataweza.”

Dk. Mzindakaya alisema ana imani kwamba Magufuli atasafisha rushwa na atatimiza dhamira yake ya kuhakikisha mtu mmoja hajilimbikizii vyeo hali ambayo husababisha kuwapo kwa ufanisi hafifu.
Kutokana na imani hiyo, aliwasihi wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa CCM kumpa kura za kishindo za ndiyo ili atekeleze azma yake ya kusafisha rushwa, ufisadi na uovu uliojaa ndani ya chama hicho.
Kuhusu wanaoohofia kuenguliwa baada ya Magufuli kushika uenyekiti wa CCM, Mzindakaya alisema watu hao wanaogopa vivuli vyao kutokana na mambo mabaya waliyoyafanya.
“Mtu mwema siku zote haogopi mabadiliko na ukiona mtu ana hofu ujue ana kasoro au madhambi na watu wa aina hii wasivumiliwe hata kidogo kwa sababu ni sumu kwa maendeleo ya chama na taifa kwa ujumla.”
AWANANGA WANAFIKI
Pamoja na kutoa ushauri kwa Rais, Dk. Mzindakaya ambaye aliwahi kushika nafasi za naibu waziri (waziri mdogo enzi hizo), ukuu wa mkoa na ubunge, aliwananga baadhi ya wanasiasa ambao wamekuwa wakibeza serikali iliyopita, chini ya Kikwete kuwa ilifanya vibaya.

Mzindakaya alisema ameshangazwa kwamba baadhi yao walikuwa mawaziri katika serikali hiyo na kuwaita ni wanafiki wanaopaswa kuogopwa kama ukoma.
“Hawa watu wengine walikuwa mawaziri katika serikali ya awamu ya nne chini ya Jakaya Kikwete. Walikuwa wapi wasimshauri juu ya hayo mambo wanayoyasema sasa? Watu hawa ni wanafiki na hawastahili kupewa nafasi kabisa.
“Unafiki ni kitu kibaya sana na ni aibu kuwa na wanafiki katika jamii. Kwa sababu ya unafiki wao baadhi yao wameanza kulipwa mshahara kutokana na hilo,” alisema bila kuwataja watu hao.
Alitoa mfano wakati wa utawala wa awamu ya kwanza chini ya Mwalimu Julius Nyerere, akisema wajumbe wa kamati kuu ya chama walikosoa mipango ya maendeleo.
Katika ushauri wake, alisema aliandika kijitabu cha “Wawindaji 10 tusigombanie sungura mmoja” hoja ambayo Nyerere aliikubali na kuwataka wapanue mawazo kubuni mipango ya maendeleo.
Pia Mzindakaya aliwaponda baadhi ya watu wanaobeza uteuzi wa Rais alioufanya kwa wakuu wa mikoa, wilaya, makatibu tawala wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri na kusema umezingatia sifa na vigezo.
Hata hivyo, alisema wateule hao wanapaswa kuonyesha kwa vitendo kuwa wana sifa na uwezo katika nafasi walizopewa ili aliyewaamini aendelee kuwaamini na hata kuwapa nafasi za juu zaidi.
ANG’ATUKA NDC
Wakati huo huo, mwanasiasa mkongwe, Dk. Chrisant Mzindakaya jana alitangaza kuachia uenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la maendeleo la Taifa (NDC), nafasi ambayo ameitumikia kwa zaidi ya vipindi viwili vya miaka mitatu kila kimoja.

Mzindakaya ambaye aliteuliwa kushika wadhifa huo kwa mara ya kwanza mwaka 2007, kipindi chake cha tatu kilitarajiwa kumalizika Julai, mwakani.
Alkisema amemwandikia Rais Magufuli barua ya kujiuzulu kwake.
Alisema ameamua kupumzika katika nafasi hiyo kutokana na umri, kwa kuwa mwezi ujao anatarajiwa kufikisha miaka 76.
“Nimefikia uamuzi huu nikiwa ninafurahia mafanikio yaliyopatikana ndani ya shirika ikiwamo miradi ya makaa ya mawe ya Mchuchuma ambao utakapokamilika utazalisha megawati 600 za umeme na wa chuma Liganga ambao utazalisha tani milioni moja," alisema.
Sambamba na miradi hiyo, alitaja mafanikio mengine kuwa ni ujenzi wa kiwanda cha viuadudu Kibaha, mkoani Pwani ambacho ni kikubwa kwa Afrika na kitakapoanza kazi kitasaidia kupunguza tatizo la malaria nchini.
Alisema katika kuchukua uamuzi huo, amezingatia misingi aliyojiwekea katika maisha kuwa ni lazima afike mahali na kung’atuka katika nafasi aliyo nayo na kwamba amekuwa akifanya hivyo mara kwa mara.
Mwaka 1995, alisema, baada ya uchaguzi mkuu alimfuata Rais mstaafu Benjamin Mkapa na kumwomba asimfikirie katika safu yake kwa kuwa alikuwa ameamua kuwa mbunge na mkulima baada ya kuwa mkuu wa Mkoa kwa miaka 23.
Pia alisema baada ya kuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) kwa miaka 15, aliamua kung’atuka mwaka 2007 na pia aliamua kuachia ngazi ubunge wa Kwela mwaka 2010 baada ya kuwa kwenye nafasi hiyo kwa miaka 44 .
“Hata nafasi hii nimeona ning’atuke baada ya kuishika kwa zaidi ya vipindi viwili. Nimpongeze Rais (mstaafu) Kikwete kwa kuniamini pamoja na Rais Magufuli kuendelea kuniamini baada ya kuingia madarakani,” alisema.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment