Waziri
Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anaendelea na kile anachokiita ziara
ya kihistoria Barani Afrika, katika mpango wake wa kuimarisha mahusiano
ya kibiashara na kiusalama na Bara hilo.
Jana Jumatatu Waziri Mkuu
Netanyahu alihudhuria maadhimisho ya miaka 40, baada ya kuokolewa kwa
mateka nchini Uganda, ambapo kaka yake mwenyewe aliyeongoza operesheni
hiyo aliuawa.
Mchana huu, tayari Netanyahu yuko jijini Nairobi,
nchini Kenya akikutana na mwenyeji wake, Rais Uhuru Kenyatta. Mwenyewe
Kenyatta alikuwa ziarani Israel hivi karibuni. Alipozungumza hapo jana,
mjini Entebbe, Uganda, karibu na uwanja wa ndege ambapo operesheni hiyo
ilifanyika, wakati mateka takriban 100 walipokuwa wakiokolewa mnamo
mwaka 1976, Netanyahu amesema tukio hili linapotea taratibu na kufungua
ukurasa mpya wa mahusiano ya karibu zaidi na Afrika.
"Miaka 40
iliyopita, askari wa Israel waliendesha operesheni ya kihistoria hapa
Entebbe", alisema Netanyahu ambaye amekuwa waziri mkuu wa kwanza wa
Israel kufanya ziara ya kwanza katika Ukanda wa Kusini mwa Bara la
Afrika, baada ya miongo mingi.
Taarifa zinasema kuwa, Israel imetoa
msaada wa dola za Kimarekani bilioni 13 za kuwezesha kuimarisha
mahusiano ya kiuchumi na nchi za Afrika. Nchi hiyo pia inatarajia kutoa
mafunzo ya namna ya kuboresha usalama wa ndani na afya.
Baada ya
mkutano wa kihistoria uliokutanisha viongozi saba wa Afrika uliofanyika
nchini Uganda, Netanyahu ambaye ameongozana na wafanyabiashara 80
wanaowakilisha makampuni 50 ya biashara, alielekea Kenya hivi leo, huku
pia wakitarajia kuzuru Ethiopia na Rwanda.
Machafuko kati ya nchi za
Kiarabu na Israel yalichangia hali ya kutengamana kati ya nchi za Afrika
na mataifa ya Kiyahudi tangu miaka ya 1960. Kutokana na vita kati ya
Israel na majirani zake kati ya mwaka 1967 na 1973, mataifa yaliyopo
Kaskazini mwa Afrika yaliyoongozwa na Misri yalishinikiza nchi zilizopo
Kusini mwa jangwa la Sahara kukata mahusiano yake na Israel, ambapo
mengi yaliitikia shinikizo hilo.
Kando na mahusiano ya kidiplomasia
na biashara, ziara hiyo ina maana binafsi kwa Netanyahu. Mwaka 1976,
kaka yake Jonatan, aliyejulikana kwa jina la utani, "Yoni" aliuwawa
wakati huo akiwa komandoo aliyeongoza mashambulizi ya ghafla mjini
Entebbe nchini Uganda katika kuwaokoa abiria waliokuwa kwenye ndege ya
shirika la ndege la Ufaransa, "Air France" iliyotekwa na Wapalestina
wawili na Wajerumani wawili.
"Nimejifunza kutoka kwa kaka yangu
kwamba mnahitaji vitu viwili katika kukabiliana na ugaidi, uwazi na
ujasiri", Netanyahu alisema. Alipozungumza katika maadhimisho hayo,
alisema vita dhidi ya ugaidi vitaendelea. Alisema, iwapo magaidi
wanafanikiwa eneo moja, hujisogeza na maeneo mengine, na iwapo ugaidi
utadhibitiwa mahala popote, utakuwa unapunguzwa nguvu hata maeneo
mengine.
Mahusiano kati ya Israel na Afrika kibiashara hivi sasa ni
asilimia 2 tu, ingawa bado kunaoneka kuwepo na ongezeko la mahitaji.
Lakini pia Israel inaliona Bara la Afrika kama mshirika wake muhimu,
hususan ndani ya Umoja wa Mataifa na taasisi za kimataifa, ambazo mara
nyingi zimeitupia lawama ya kulikalia eneo la Ukingo wa Magharibi na
kuweka kizuizi katika ukanda wa Gaza.
Baadhi ya nchi za Afrika
zimeonyesha utayari wa kujifunza teknolojia ya kilimo na maji kutoka
nchini Israel, ambazo nchi hiyo imekuwa ikizipigia debe. Ziara hii ya
Netanyahu, inafuatia mikakati ya mida mrefu ya kuboresha mahusiano na
Afrika.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment