WAZIRI
wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, ProfesaJoyce
Ndalichako, amesema operesheni ya uhakiki wa wanafunzi hewa wanaopatiwa
mikopo imeanza na kuonesha mafanikio, kwani wanafunzi hewa wameanza
kubainika.
Akizungumza baada ya kufungua Maonesho ya 11 ya Elimu ya
Juu, Sayansi na Teknolojia yaliyoandaliwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania
(TCU) jana, alisema uchunguzi wa awali umebaini wanafunzi hewa 139
katika vyuo vitano vilivyofanyiwa uhakiki.
“Tunaendelea kuhakiki na
tayari tumehakiki vyuo vitano ambapo wanafunzi hewa 139 walibainika kati
yao wamo marehemu, walioacha shule, waliosimamishwa shule na
waliohamishwa,” alisema bila kuvitaja vyuo hivyo kwa maelezo kuwa,
taarifa haijawa kamili.
Aidha, alisema katika jitihada za kuboresha
elimu inayotolewa nchini wizara hiyo inafanya mapitio ya Sheria ya Vyuo
Vikuu ili itoe fursa kuchukulia hatua vyuo vya kitapeli. Alisema kupitia
sheria hiyo, serikali itaanzisha mfumo wa kuratibu na kudhibiti
uanzishwaji wa vyuo kwa lengo la kuwabana wanaoanzisha vyuo kwa lengo la
utapeli.
Hivi karibuni, Rais John Magufuli aliwasimamisha kazi
watendaji wakuu wa Kamisheni ya Tume vya Vyuo Vikuu (TCU) baada ya
kubainika kamisheni hiyo inadahili wanafunzi wasio na sifa, wakiwemo
wenye ufaulu wa daraja la nne, kujiunga na vyuo vikuu na kuwapatia
mikopo.
Serikali pia ilibaini uwepo wa wanafunzi hewa wanaotafuna
mikopo ya elimu ya juu, jambo lililosababisha Profesa Ndalichako
kutangaza vita dhidi yao na kuanza operesheni ya uhakiki katika vyuo
vyote vikuu nchini.
Aliungwa mkono na Rais John Magufuli aliyetangaza
kuwa serikali yake imejipanga kumaliza makosa yote yaliyojitokeza huko
nyuma, ikiwemo tatizo la watumishi na wanafunzi hewa lililoibuka hivi
karibuni.
Profesa Ndalichako alianza kuchukua hatua kwa kusimamisha
kazi viongozi wanne waandamizi kwa tuhuma za kudahili wanafunzi wasio na
sifa.
Aidha, Mwenyekiti wa Bodi ya TCU, Awadh Mawenya naye
alisimamishwa kazi kwa kosa la kushindwa kuwachukulia hatua watumishi
waliodahili wanafunzi hao wasio na sifa.
Profesa Ndalichako alichukua
hatua hizo baada ya TCU kudahili wanafunzi 489 waliopata daraja la 4.32
katika mitihani yao ya kidato cha nne lakini walijiunga na chuo kikuu
na kupatiwa mikopo yenye thamani ya Sh milioni 784.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment