MATOKEO
ya Utafiti wa Utumikishwaji wa Watoto wa mwaka 2014 (2014 NCL),
Tanzania Bara yameonesha kuwa, kati ya watoto milioni 15 wenye umri kati
ya miaka 5 -17, watoto milioni 4.2 sawa na asilimia 28.8 wanatumikishwa
katika kazi mbalimbali za kiuchumi.
Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya
Taifa ya Takwimu, Dk Albina Chuwa aliyasema hayo jana jijini Dar es
Salaam wakati wa uzinduzi wa ripoti ya matokeo ya utafiti huo
unaofanyika kila baada ya miaka mitano na utafiti wa mwisho ulifanyika
mwaka 2006/2007.
Alisema sekta ya kilimo, misitu na uvuvi imeendelea
kuongoza kwa kuajiri watoto, ikiwa na kiwango cha asilimia 92.1 ya
watoto wote wanaojihusisha na shughuli za kiuchumi na wengi wao wanaishi
vijijini.
“Matokeo haya yameonesha kuwa watoto hutumia zaidi ya nusu
ya muda wao wa siku yaani asilimia 58.8 kwa shughuli za kujihudumia na
usafi binafsi, huku wasichana wakionekana kutumia muda mrefu zaidi kwa
shughuli hizo, kwa kiwango cha asilimia 59.2 ikilinganishwa na wavulana
wanaotumia asilimia 58.3,” alisema.
Aidha, alisema shughuli za
kujisomea kwa watoto zilichukua nafasi ya pili kwa matumizi ya muda kwa
kiwango cha asilimia 15.5 ambapo wavulana walitumia muda mrefu zaidi
kujisomea ambao ni asilimia 16.4 ikilinganishwa na wasichana waliotumia
wastani wa asilimia 14.6.
Alisema hali hiyo haiendani na kaulimbiu ya
Serikali ya Awamu ya Tano ya “Hapa Kazi Tu” kwa watoto kutumia muda
mwingi katika starehe badala ya kusoma.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment