RAIS
John Magufuli ameibua wizi wa mabilioni ya fedha za sare za Jeshi la
Polisi, unaodaiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka jana na ameagiza wahusika
washughulikiwe mara moja na kufikishwa katika vyombo vya dola.
Aidha,
amemuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali wa Polisi
(IGP) Ernest Mangu kuorodhesha majina ya watumishi raia katika jeshi
hilo na kuwarejesha Utumishi, akieleza kuwa baadhi yao wanachafua jeshi
hilo kwa wizi na ubadhirifu na kutaka wakapangiwe kazi nyingine.
Kuhusu
wizi, Magufuli amesema kuna minong’ono inayoendelea katika jeshi hilo
kwamba kati ya Sh bilioni 20 hadi 60, zinatajwa kutolewa katika kipindi
hicho kwa ajili ya sare za polisi, lakini mpaka sasa hakuna sare yoyote
iliyonunuliwa, jambo alilodai kama ni kweli, na kwamba watu hao
wanapaswa kufikishwa mbele ya sheria.
Rais alisema hayo Ikulu, Dar es
Salaam jana, alipokaribishwa kuzungumza katika hafla ya kula Kiapo cha
Uadilifu kwa Viongozi wa Umma kwa makamishna 58 kati ya 60 wa Jeshi la
Polisi, aliowapandisha vyeo Julai 16, mwaka huu.
Makamishna hao
waliapishwa na Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma,
Jaji mstaafu Salome Kaganda wakiwamo manaibu Kamishna wa Polisi (DCP) 23
na Makamishna Wasaidizi Waandamizi wa Polisi (SACP) 35 huku wawili
wakiwa nje ya nchi kwa mafunzo mafupi.
Mhasibu na watumishi hewa
Akitolea
mfano, Mhasibu Mkuu wa Jeshi hilo, Frank Msaki anayetuhumiwa kufanya
malipo ya posho kwa watumishi hewa wasio askari wa jeshi hilo, Rais
Magufuli alisema inashangaza kuona Polisi wanakamata wezi wa kuku
mtaani, lakini wezi ndani ya Jeshi hilo wanashindwa kuwakamata.
Alisema,
aliagiza hatua stahiki zichukuliwe kwa mhasibu huyo na watu wengine kwa
kufikishwa mbele ya sheria, kwani watu kama hao ndio wanaochafua jeshi
hilo.
Alitoa mwito kwa makamishna walioapishwa kushughulikia suala la
watumishi hewa katika maeneo yao ya kazi ili kuzuia ubadhirifu wa fedha
na mali za umma.
Raia waondolewe
Rais Magufuli akisisitiza mfano
wa mhasibu huyo, alisema ikiwa katika jeshi hilo tatizo ni raia ndio
wanaochafua jeshi, IGP Mangu aorodheshe majina ya watumishi raia wote
ndani ya jeshi hilo na kuwapeleka Utumishi, wakapangiwe kazi nyingine.
“Kama raia ndio chanzo, wahamisheni wapelekwe Utumishi wapangiwe kazi nyingine za kiraia maana wataendelea kuwachafua,” alisema.
Alihoji
ikiwa hakuna askari polisi waliosomea uhasibu, rasilimali watu na kazi
nyingine wanaoweza kuzifanya kazi hizo mpaka raia wazifanye na
kusisitiza kuwa matatizo mengine katika jeshi hilo, wanayataka wenyewe
kwa kuchanganya kware na njiwa pamoja.
“IGP kachambue vizuri raia
wanaochafua jeshi wapelekwe Utumishi wakapangiwe kazi za uraia. Naona
raia wa jeshini hashughulikiwi ila wa nje anashughulikiwa,” alisema
Magufuli akisisitiza utekelezaji wa majukumu bila upendeleo na kwa
kuzingatia sheria. Wizi wa mabilioni Magufuli alisema, “Kuna minong’ono
kuwa ‘billions of money’ (mabilioni ya fedha) yamelipwa kwa ajili ya
uniform (sare) za Polisi mwishoni mwa 2015, na waziri anajua, IGP (Mkuu
wa Polisi) anajua, Katibu Mkuu anajua na makamishna.
Kuna wanaosema
zilitoka shilingi bilioni 40, wengine 60 na wengine 20 ndani ya wiki
moja. “Natumaini siku hawa watafikishwa mbele ya sheria. Magari ya
polisi yamekwama bandarini kwa kukosa fedha na mabilioni yameliwa, msema
kweli ni mpenzi wa Mungu, kama ni kweli, mkasimamie hili, fedha zirudi,
mkakomboe magari,” alisisitiza Magufuli huku akimuuliza Waziri wa Mambo
ya Ndani, Mwigulu Nchemba kuwa ni magari mangapi yamekwama bandarini na
kueleza kuwa ni 77.
Agizo la Rais amelitoa huku Jeshi la Polisi,
likikabiliwa na kashfa ya mkataba wenye utata wa zaidi ya Sh bilioni 30
wa Kampuni ya Lugumi Enterprises Ltd inayomilikiwa na mfanyabiashara
Said Lugumi na Polisi wa mwaka 2011.
Mkataba huo unadaiwa kuitaka
kampuni hiyo kufunga mitambo ya kuchukua alama za vidole katika vituo
108 vya polisi nchini; na mpaka sasa inadaiwa vituo 14 pekee vimefungwa
mitambo hiyo.
Juzi IGP Mangu alisema suala hilo linashughulikiwa na
Bunge. Vituo vya Polisi kutovamiwa Pamoja na agizo hilo, Rais Magufuli
pia alilipongeza Jeshi la Polisi kwa kusimamia uwajibikaji, ulinzi na
usalama, hali iliyorejesha amani na kupunguza uvamizi katika vituo vya
polisi na uhalifu mwingine.
Alisema ana imani na Polisi na ameona kwa
kipindi kifupi Jeshi hilo, limemuelewa kuhusu kuhakikisha vituo vya
polisi havivamiwi na askari hawaporwi silaha. “Kipindi cha sasa naona
mmeanza kunielewa.
Sijaona kituo kimevamiwa wala wale jamaa
kunyang’anya silaha badala yake naona wao wananyang’anywa silaha zao.
Endelezeni hiyo, safi.
Ndio maana sikuwa na wasiwasi kuwapandisha
vyeo. Hata hivyo, alisema wapo wachache wanaoharibu sifa hiyo nzuri ama
kwa makusudi na nia yao mbaya na aliagiza wakaambiwe wajirekebishe ama
waondolewe kabisa ili mambo wanayofanya yenye ukakasi yasiendelee
kuchafua jeshi hilo.
Viongozi wenye magari
Katika kusisitiza
uadilifu na uwajibikaji, Rais aliwataka makamishna walioapishwa na
viongozi wengine wa Polisi, kufanya kazi bila woga na kuzingatia sheria
huku akionya baadhi wanaotumia nafasi zao, kutishia askari wa chini
wasiguswe pindi wanapokamatwa.
Akitoa mfano, alisema kuna mabasi
(akitaja Buffalo na Happy Nation) ya watu wanaodaiwa kuwa ni wakubwa,
yakiguswa yanapobainika kuwa na makosa, inakuwa shida.
Aliagiza kuwa askari wa chini akishika hata gari la rais, IGP, waziri au kiongozi yeyote, aachwe atekeleze wajibu wake.
“Sheria
ni msumeno, tusiwavunje moyo askari wa chini kutekeleza majukumu yao
wala tusiwavunje moyo, vyeo vyetu tuweke pembeni, tuwape mamlaka
tunaowasimamia kutekeleza sheria. Kuna asilimia ndogo ya wachache
ukiwagusa tu wafa, mimi napokea message (ujumbe) kweli kweli, sitapenda
kuona mtu anazuiwa kutekeleza sheria,” alisema Rais.
Maduka ya bidhaa majeshini
Kuhusu
kuondolewa kwa punguzo la kodi kwa maduka ya bidhaa katika kambi za
majeshi, rais alifafanua kuwa uamuzi huo umefikiwa baada ya kuona kuwa
wanufaika wengi si walengwa.
Alisema badala yake, serikali imeamua
katika mwaka huu wa fedha, fedha zilizokuwa zikipunguzwa katika bidhaa
hizo ziwekwe katika mishahara ya askari na kuongeza makazi bora kwao.
“Niwahakikishie
kuwa makusanyo ya mapato yanaongezeka, tutafika tu,” alisema Magufuli.
VAT kwa watalii, meli bandarini Alisema kumekuwa na maneno kuwa meli
zimepungua bandarini; na kueleza kuwa ni heri kuwa na meli chache,
zinazoingia nchini na kulipa kodi kuliko utitiri wa meli zinazokwepa
kodi na kuisababisha serikali hasara. “Tunataka anayekuja alipe kodi.
Yapungue tu, hata yaache kuja yaende wasikolipa kodi,” alisema.
Kuhusu
watalii kulipa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika huduma za
utalii, Magufuli alisema ni heri kuwa na watalii 500,000 wanaolipa kodi
kuliko watalii milioni mbili wasiolipa kodi.
Alisema katika kipindi
hiki alichokiita cha mpito, watanzania watasikia mengi kwa kuwa wako
waliozoea kupata fedha za bure, sasa hawazipati.
Hoteli tupu, safari za Dubai
Alisema
watu wachache wamekuwa wakineemeka isivyo halali na kuongeza kuwa ana
taarifa kuwa baadhi waliwapangia watu hoteli zaidi ya tatu na kufanya
safari za kustarehe Dubai na wengi wao ni watumishi wa umma.
“Kuna
waliokuwa wakipanga na kupangia watu hoteli hii, na hii na hii. Nchi hii
ni yetu sote, hakuna aliyeumbwa kupata shida na mwingine astarehe. Nchi
hii imeliwa, watu wanakula mabilioni ya fedha, mkafanye kazi kwani
mliopandishwa vyeo mnastahili,” alisema Rais na kusifia Jeshi hilo kuwa
wanafanya kazi nzuri.
Aliahidi kuyalinda, kuyazingatia na kuboresha
maslahi ya Polisi na askari wa vyombo vyote vya usalama akieleza kuwa
changamoto na matatizo yao yanafanana na anayafahamu.
Polisi Jamii
Rais
alionesha kushangazwa na kile alichosema baadhi ya polisi, kufanya
mazungumzo na wahalifu wakiwemo majambazi na kueleza kuwa dhana ya
Polisi Jamii, aliipinga tangu awali akiwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo
na Uvuvi. Alisema haiwezekani askari ameshika silaha (akitaja SMG) na
jambazi anamnyang’anya huku watu wakieleza ni polisi jamii.
“Kule
Chato (kijijini kwake) wananchi walivamia kituo cha polisi. Vituo
vinavamiwa sisi tunasema polisi jamii, hawa watu wanapaswa kulala pema
hata kama ni ndugu yangu. Naomba katika utendaji wenu mtangulizeni Mungu
mbele na usalama wa raia na mali zao,” alisisitiza Rais.
Uadilifu Polisi
Akizungumzia
uadilifu katika Jeshi la Polisi, Magufuli alisisitiza askari wa chini
wathaminiwe na kutaka viongozi wa jeshi hilo, wajitathimini kila mmoja
kwa nafasi yake katika uadilifu.
Alisema wapo baadhi ya viongozi
wanaotumia nafasi zao vibaya kwa kuwakwamisha askari wa chini
wanapokamata wahalifu na wao kuagiza waachiliwe.
Magufuli alisema
katika kuwapandisha vyeo, wapo waliokwama baada ya majina yao
kutorejeshwa kuwa wamepanda vyeo na aliwatuma makamishna waliokula
kiapo, kuwaeleza waliobaki wasitafute mchawi bali wajipange na
kurekebisha wasikofanya vizuri.
“Mchakato ulichukua miezi mitatu,
minne, mitano hivi iliyopita, nilimwagiza IGP (Mangu) sababu nilijua
kazi nzuri inayofanywa na Polisi. Nilipokea majina ya makamishna
wasaidizi waandamizi 46 waliopendekezwa wakabaki 35 na manaibu 31
wamebaki 25. Msitafute mchawi, mchawi ni mimi, watumie muda
kujirekebisha."
Kamishna Jaji
Kaganda Awali, akitoa maelezo ya
kiapo hicho cha ahadi ya uadilifu kabla ya makamishna hao kula kiapo,
Kamishna Jaji Kaganda alionya baadhi ya viongozi wa polisi kuwa sababu
ya askari wa chini kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa kuhusika
kuwaachia wahalifu na kuwataka wawe sababu ya kurejesha maadili katika
jeshi hilo.
“Mkumbuke ahadi hii ni nyenzo ya kutekeleza utii kwa
serikali na kuweka mbele uzalendo, muitunze ahadi hii ofisini kila
mnapoingia muone na wananchi waone kile mnachopaswa kutekeleza. Huu ni
mkataba,” alisema Jaji Kaganda.
Alisema ahadi hiyo ni tamko rasmi na bayana la kuunga mkono mapambano dhidi ya rushwa, matumizi mabaya ya madaraka na rushwa.
Aliwataka
kusimamia hayo. Jaji Kaganda aliagiza makamishna hao kuunda Kamati za
Maadili katika maeneo yao ya kazi ili kero za askari na watumishi wa
chini zishughulikiwe katika ngazi husika kabla ya kufika ngazi za juu.
Alisema IGP Mangu amekuwa akipokea malalamiko ya askari wa chini, ambayo yangetatuliwa na viongozi wa chini.
Mwigulu, AG
Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba akitoa salamu baada ya kiapo
hicho, aliwataka makamishna hao kuzingatia kasi ya serikali ya Rais
Magufuli katika kuwatumikia wananchi kwa uadilifu na kuhakikisha watu
hawakosi imani na jeshi hilo.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment