CHAMA
Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kwamba Mkutano Mkuu Maalumu wa chama
hicho, utakaofanyika mwishoni mwa wiki hii si wa kupokezana vijiti, kwa
sababu nafasi za Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti unapofika wakati wa
uchaguzi haziombwi, bali yanapendekezwa majina ya watu wanaofaa kushika
nyadhifa huo.
Aidha, kimesema maandalizi ya mkutano huo utakaofanyika
Jumamosi wiki hii, yamekamilika na unatarajiwa kushirikisha wajumbe
2,456 na mpaka sasa wamekodi hoteli 306 ambazo zitawalaza zaidi ya watu
3,331 mjini Dodoma.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari jana,
Msemaji wa CCM, Christopher ole Sendeka alisema Mkutano Mkuu Maalumu wa
Taifa utamchagua Mwenyekiti wa CCM Taifa baada ya Mwenyekiti wa sasa,
Jakaya Kikwete kung’atuka na kutoa nafasi hiyo kwa Rais John Magufuli
kugombea.
Alisema Rais Magufuli atakuwa Mwenyekiti wa CCM wa tano
baada ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Ali Hassan Mwinyi,
Benjamin Mkapa na Kikwete.
“Kwa mujibu wa Katiba ya CCM, nafasi ya
Mwenyekiti wa CCM na Makamu Mwenyekiti wawili unapofikia wakati wa
uchaguzi nafasi hizi haziombwi isipokuwa Kamati Kuu inafikiria na
kupendekeza majina na kuyawasilisha kwa Halmashauri Kuu ya Taifa ambayo
humteua,” alisema Sendeka.
Alisema kisha Mkutano Mkuu wa Taifa
unamchagua kwa kumpigia kura. Alisema wanaopendekezwa hawajazi fomu za
kugombea nafasi hizo na katika mchakato huo kinachofanyika si kupokezana
kijiti, kama wengi wanavyopenda kuita, bali ni uchaguzi wa kumpata
mwenyekiti wa CCM.
Alisema katika uchaguzi huo itapigwa kura ya
‘ndio’ au ‘hapana’ ili kupata mwenyekiti na lazima apate nusu ya kura na
akipata chini ya nusu mapendekezo yataanza upya.
“Tuna imani wajumbe
wote watampa mwenyekiti mpya kura zote za ‘ndio’ ili achukue nafasi ya
kuongoza kitaifa,” alisema na kuongeza kuwa akipatikana mwenyekiti
ataunda ‘jeshi’ lake, kwani hiyo ni desturi ya chama na walio katika
Sektetarieti, watapisha ili mwenyekiti mpya aunde jeshi lake.
Rais
Magufuli anatarajiwa kufanya mabadiliko makubwa ya uongozi ndani ya CCM
baada ya kukabidhiwa uenyekiti wa Taifa, kwa kupanga upya safu yake ya
viongozi, ambao anaamini anaweza kufanya kazi nao kwa ajili ya kuleta
mabadiliko ndani ya Chama.
Viongozi watakaojiuzulu ili kupisha Dk
Magufuli kupanga safu hiyo ni Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana,
manaibu katibu mkuu wawili na watendaji wengine.
Wajumbe wa
Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa ni pamoja na Katibu Mkuu, Naibu
Katibu Mkuu Bara, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Katibu wa Oganaizesheni,
Katibu wa Siasa na Uhusiano ya Kimataifa, Katibu wa Uchumi na Fedha na
wa Itikadi na Uenezi.
“Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana
atakabidhi barua yake kwa mwenyekiti wa chama kupisha Rais Magufuli
aweze kuunda safu yake ya watu atakaofanya nao kazi,” alieleza Sendeka
na kuongeza kuwa anaamini Magufuli ataunda safu nzuri itakayoleta
mabadiliko.
“Chama madhubuti huzaa serikali madhubuti na chama
legelege huzaa serikali legelege,” aliongeza na kubainisha kuwa
maandalizi kwa ajili ya mkutano huo, yamekamilika na tayari fedha
zimetumwa mikoani ili kuwezesha wajumbe wote kufika; na magari
yatakodishwa kuwaleta mjini hapa.
Alisema jumla ya wajumbe 2,456
watahudhuria mkutano huo, lakini pia wanajitahidi kuweka hesabu vizuri
kwa kuondoa wajumbe wenye kofia mbili. Alisema wamekodi hoteli 306.
Akizungumzia hali ya usalama alisema wamejipanga kuhakikisha mkutano huo
unafanyika kwa amani.
“Dodoma ni shwari na salama watu wasiwe na
hofu na tuna imani mkutano utamalizika vizuri,” alifafanua na kuongeza
kuwa wajumbe wa NEC watawasili Alhamisi tayari kwa kikao cha Ijumaa na
wajumbe wengine watawasili Ijumaa.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment