BENKI
ya Exim ya China imekubali kutoa mkopo wenye masharti nafuu wa Dola za
Marekani bilioni 7.6 sawa na zaidi ya Sh trilioni 16 kwa ajili ya
kugharamia ujenzi wa mradi mkubwa wa Reli ya Kati nchini kwa kiwango cha
kisasa (standard gauge) unaotarajiwa kuanza mwaka huu wa fedha.
Rais
wa Benki ya Exim ya China, Liu Liang amemueleza Rais John Magufuli jana
Ikulu ndogo ya Chamwino mjini Dodoma, kuwa pamoja na kutoa fedha hizo
zitakazofanikisha ujenzi wa kilometa 2,190 za Reli ya Kati, benki hiyo
itashirikiana na Tanzania katika kubadilishana uzoefu na utaalamu katika
ujenzi na uendeshaji wa reli.
Pamoja na kukubali kutoa fedha hizo,
Rais huyo wa Benki ya Exim ya China amempongeza Rais Magufuli na
serikali yake kwa dhamira ya dhati ya kuiletea nchi maendeleo, ikiwemo
kuharakisha ujenzi wa Reli ya Kati na ameahidi kuwa benki yake itatoa
ushirikiano wa karibu katika kufanikisha mradi huo na miradi mingine ya
maendeleo.
“Kuhusu huu mradi wa Reli ya Kati tuna mtazamo chanya,
tunauona ni mradi mzuri na tutatoa ushirikiano wowote utakaohitajika.
Tunaamini kuwa kwa ushirikiano na Serikali ya Tanzania mchakato wa
utekelezaji wa mradi huu utafanyika kwa mafanikio na kwa kuzingatia
muda,” alisema rais huyo wa Benki ya Exim.
Kwa upande wake, Rais
Magufuli amemshukuru Rais wa Benki ya Exim ya China kwa kukubali kutoa
fedha hizo na amemhakikishia kuwa Tanzania imedhamiria kutekeleza mradi
huo ambao tayari ujenzi wake umepangwa kuanza katika mwaka huu wa fedha
kwa kutumia fedha za ndani kiasi cha Sh trilioni moja zilizotengwa
katika bajeti.
Rais Magufuli amebainisha kuwa kutekelezwa kwa mradi
huo kutasaidia kuinua uchumi wa Tanzania na nchi jirani zisizopakana na
bahari zikiwemo Uganda, Rwanda, Burundi, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Congo (DRC).
“Kwa hiyo kukubali kwao ambako ilikuwa ni kitu kikubwa,
inaonesha kwamba juhudi za Tanzania kwenda haraka haraka zinakubalika
kimataifa, na wenzetu hawa Wachina wana pesa nyingi. Na kule kuaminika
kwamba tunakopeshwa kwa masharti nafuu, riba yake ni ndogo na huku kwetu
ni mafanikio makubwa, kwa hiyo mizigo mingi tutakuwa tunaisafirisha,
tutaendeleza reli yetu na bandari zetu,” alisema Rais Magufuli.
Mradi
wa ujenzi wa Reli ya Kati utahusisha ujenzi wa reli kwa kiwango cha
kisasa (Standard Gauge) kutoka Dar es Salaam – Tabora –Isaka - Mwanza,
Tabora – Mpanda -Kalemela, Tabora – Uvinza – Kigoma na Isaka – Keza –
Msongati.
Mazungumzo kati ya Rais Magufuli na Rais wa Benki ya Exim
ya China yamehudhuriwa na Balozi wa China nchini, Dk Lu Youqing, Waziri
wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, Waziri wa
Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Suzan Kolimba.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment