FEDHA zilizotengwa na Rais John Magufuli kwa ajili ya kugharimia
elimu ya bure nchini, zimeanza kutafunwa baada ya kubaini kuwapo kwa
udanganyifu unaofanywa na walimu wakuu kwa kuongeza idadi ya wanafunzi
hewa ili kupata fedha zaidi.
Kutokana na hali hiyo, wilaya ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam na
Manispaa ya Arusha, zimebaini udanganyifu huo na kuchukua hatua za awali
kwa kusimamisha walimu wakuu wa shule husika na pia kuziagiza mamlaka
husika kuwavua uongozi walimu hao.
Hivi karibuni, Rais Magufuli aliwaagiza wakuu wa wilaya zote,
kushughulikia udanganyifu unaofanywa na walimu wakuu wanaotafuna fedha
kwa kuweka wanafunzi hewa katika suala la elimu bure baada ya serikali
kuanza kutoa elimu bure Januari mwaka huu, ikitenga Sh bilioni 18.7 kila
mwezi.
Wanafunzi hewa Kinondoni
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi aliwaambia waandishi wa habari
jana Dar es Salaam kuwa kubainika kwa wanafunzi hao kumekuja baada ya
kuagiza mkurugenzi na watendaji kufanya uhakiki shule kwa shule ili
kubaini wanafunzi hewa, waliowekwa na walimu wakuu wasiokuwa na uzalendo
na kujipatia fedha kinyume cha sheria.
“Hadi kufikia leo (jana) tumebaini wanafunzi hewa 3,462 kutoka shule
68 za msingi na wanafunzi 2,534 kutoka shule 22 za sekondari ambao
wameingizwa, ni jambo la kusikitisha fedha za serikali zinapotea kwa
sababu ya walimu wakuu wasio waaminifu,” alisema Hapi.
Alizitaja baadhi ya shule za msingi zilizokutwa na wanafunzi hewa ni
Msisiri B, Msewe, Golani, Kibangu, Kimara Baruti, Ubungo Kisiwani,
Shekilango, Tandale, Makoka, Mbezi Luis, Kijitonyama, Kinondoni,
Mburahati, Makumbusho, Makongo, Kawe A na Ubungo Plaza.
Shule za sekondari ni Boko, Bunju A, Kambangwa, Kawe Ukwamani,
Kigogo, Kiluvya, Mbweni, Matosa, Maramba Mawili, Mburahati, Salma
Kikwete, Saranga, Temboni, Mabibo, Makoka, Luguruni na Mtakuja.
Hapi alisema baada ya kubainika mambo yote hayo, hatua mbalimbali
zimechukuliwa ikiwemo kumuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa manispaa hiyo,
kuwavua vyeo walimu wakuu 68 wa shule za msingi kwa tuhuma za
udanganyifu wa takwimu juu ya elimu bure.
“Licha ya kumuagiza hilo nimemuagiza pia mkurugenzi nafasi hizo 68 za
walimu hao wapewe vijana wanaokidhi sifa na wenye uwezo wa kuendana na
kasi ya serikali ya awamu ya tano, tunataka tuwaondoe watumishi wote
wenye madaraka ambao bado wanafanya kazi kwa mazoea,” aliongeza.
Aliongeza kuwa, kwa kuwa walimu wa shule za Sekondari, wapo chini ya
Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa tayari wamemuandikia katibu huyo barua na
kuwaomba awavue vyeo walimu wakuu 22 wa shule za sekondari, waliopeleka
takwimu za uongo na kusababisha zaidi ya Sh milioni 70 kwenda kinyume
cha matarajio.
Aliongeza kuwa, kila mwalimu mkuu aliyehusika kusababisha ubadhirifu
huo wa fedha, atatakiwa kulipa fedha zote kutoka katika mshahara wake.
“Kwanza anashushwa cheo na kuwa mwalimu wa kawaida pili atachukuliwa
hatua nyingine kutoka Tume ya Utumishi wa Walimu lakini tatu atalipa
fedha zote zilizopelekwa katika shule yake kinyume na utaratibu kutokana
na udanganyifu alioufanya,” alisisitiza Hapi.
Pia Hapi alisema wameshamuandikia barua Mkurugenzi wa Tume ya
Utumishi ya Walimu, kuhakikisha hatua nyingine kali za kisheria
zinachukuliwa dhidi ya walimu hao.
Wanafunzi hewa
Arusha Mkoani Arusha, walimu wakuu wa shule za msingi 11 na sekondari
12 wamesimamishwa kazi na Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji la Arusha,
Athuman Kihamia kwa sababu ya kuongeza idadi ya wanafunzi hewa ili
kupata fedha nyingi katika mgawo wa fedha za elimu bure.
Aidha, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Mrisho Gambo ameunda timu maalumu
kwa ajili ya kuhakiki tena kwa mara ya pili, idadi ya wanafunzi hewa
katika shule mbalimbali za serikali walioisababishia serikali hasara ya
zaidi ya Sh milioni 26.12.
Kihamia alisema uchunguzi walioufanya awali kupitia waratibu wa
elimu, wenyeviti na wajumbe wa Bodi na kamati za shule, wakuu wa shule
zote za sekondari, wamebaini kuwa shule 11 za msingi zimeongezewa
wanafunzi hewa 907.
Alisema wanafunzi hao hewa wameisababishia serikali hasara ya Sh
milioni 23.3 kwa shule za sekondari katika kipindi cha Januari hadi
Julai mwaka huu na uchunguzi bado unaendelea ili kubaini shule hizo 11
zilizozidishiwa wanafunzi 907.
“Shule za sekondari idadi imeongezewa jumla ya 942 jambo ambalo
halikubaliki hata kidogo na Rais alishasema,” alisema Kihamia na
kuzitaja sekondari zilizoongeza idadi ya wanafunzi ni Arusha Day, Baraa,
Kaloleni, Kimaseki, Kinana, Morona, Moshono, Naura, Ngarenaro,
Oloirieni na Suye.
“Tumegundua wanafunzi hao hewa na hakuna fedha ya serikali
itakayoachwa iende kwenye mikono ya watu kiholela holela hapana hivyo
nimechukua hatua ya kuwasimamisha kazi na wanahojiwa hao wakuu wa shule
pamoja na waratibu wa elimu kata, ikithibitika wamekula hela hizo hatua
stahiki zitachukuliwa, kwa nini serikali ikose mapato na hela zipo,”
alisema mkurugenzi huyo.
Kwa upande wake, DC Gambo alisema amepokea taarifa za shule za msingi
za serikali 11 zenye wanafunzi ambao hawapo shuleni kulingana na hali
halisi ya wanafunzi waliopo darasani na kwamba wanafunzi 907
wanapelekewa fedha wakati hawapo shuleni.
Alitaja shule hizo kuwa ni Azimio, Kimandolu, Magereza, Maweni,
Moshono, Naura, Njiro Hill, Olkeryani, Salei, Sokon 1, Terrat na Wema na
kwa shule hizo za msingi wameisababishia serikali hasara ya Sh
3,940,008.
Gambo alimwagiza Mkurugenzi wa Jiji kuwachukulia hatua walimu hao,
akiwemo Ofisa Elimu Msingi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Hussein
Mghewa kujieleza kwa Mkurugenzi amechukua hatua gani kabla ya timu hiyo
kuundwa. Pia alisisitiza timu maalumu ya Kamati ya Ulinzi na Usalama,
imeundwa ili kubaini wanafunzi wengine hewa.
Imeandikwa na Sophia Mwambe, Dar na Veronica Mheta, Arusha.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)


0 comments:
Post a Comment