NAIBU Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk
Hamis Kigwangalla amesisitiza kuwa huduma zote za afya za magonjwa
anayowapa watoto wenye umri chini ya miaka mitano nchini ni bure.
Alisema ikitokea mwenye mgonjwa anatakiwa kulipia, mhusika atoe taarifa mahali panapohusika.
Dk Kigwangalla alisema hayo jana jijini Dares Salaam wakati
akizungumza katika uzinduzi wa ripoti inayohusu upatikanaji wa huduma za
afya na wahudumu kuongezeka kwa mwaka 2015. Ripoti hiyo ilitokana na
utafiti ulioandaliwa na mradi wa sauti za wananchi chini ya Taasisi ya
Twaweza.
Alisema kupitia Sera ya Afya nchini, watoto ni moja ya kundi la
wahitaji wa matibabu bure, wengine wakiwa ni wazee zaidi ya miaka 60 na
wote wenye kipato cha chini ambao hawapaswi kutozwa gharama.
Kuhusu madai ya kuwepo kwa uhaba wa upatikanaji wa dawa za wanaoishi
na virusi vya Ukimwi, Dk Kigwangalla alisema taarifa hizo si za kweli
kwani upo uhakika kuwa ipo akiba ya dawa kwa miezi sita kwenda mbele kwa
Jiji la Dar es Salaam huku katika mikoa mingine uhakika wa upatikanaji
wa dawa hizo ukiwa ni wa miezi mitatu mbele.
Alisema kinachoweza kukosekana ni dawa za magonjwa nyemelezi lakini
serikali imekuwa makini sana kufuatilia uwepo wa dawa hizo pamoja na za
magonjwa mengine ambayo ni magonjwa sugu.
Kuhusu kuwepo kwa makundi yanayolipia huduma hizo ilhali zinatolewa
bure, Dk Kigwangalla alisema Sera ya Afya Tanzania iko wazi kwamba
magonjwa mbalimbali ambayo ni sugu yako katika msamaha wa kulipiwa.
Alisema kinachojitokeza ni baadhi ya vifaa vinavyotakiwa kuwepo katika
stoo za vituo vya huduma za afya kutokuwepo kwa wakati.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)


0 comments:
Post a Comment