KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad,
amekataa kusalimiana kwa kushikana mkono na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali
Mohamed Shein.
Tukio hilo lilitokea jana mchana wakati wa mazishi ya Rais wa pili wa
Zanzibar, Aboud Jumbe Mwinyi, aliyezikwa jana katika makaburi yaliyoko
maeneo ya Migombani visiwani hapa.
Katika Uchaguzi Mkuu mwaka jana, Maalim Seif alishindana Dk. Shein
ambaye aliibuka mshindi katika uchaguzi wa marudio wa Machi 20, mwaka
huu.
Hata hivyo, Maalim Seif alilalamikia ushindi wa Dk. Shein kwa kile
alichosema haukuwa halali kwa kuwa alifanyiwa hujuma na kuporwa ushindi
wake uliopatikana Oktoba 25 mwaka jana.
Mazishi ya marehemu Jumbe yalifanyika jana saa saba mchana kisiwani
Unguja, ambapo Dk. Shein aliwaongoza mamia ya watu waliofika msibani
hapo.
Wakati akiwa makaburini, Dk. Shein alisalimiana na waombolezaji
mbalimbali kwa kuwashika mikono, lakini alipopeleka mkono kwa Maalim
Seif, mwanasiasa huyo mkongwe aliukataa mkono huo na kuwashangaza
waombolezaji.
Msiba huo ulihudhuriwa na viongozi na watu mbalimbali wa Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja Serikali ya Zanzibar.
Viongozi waliohudhuria ni pamoja na marais wastaafu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania akiwamo Benjamin Mkapa na Ali Hassan Mwinyi.
Mbali na hao, pia alikuwapo Makamu wa Rais mstaafu, Dk. Mohammed
Gharib Bilal, Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa na Rais mstaafu wa
Zanzibar, Amani Abeid Karume.
Wengine ni Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa na aliyekuwa Kadhi Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Habib Ali Kombo.
Akisoma risala kwa niaba ya Serikali zote mbili, Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohammed Aboud Mohammed,
alisema kifo cha Jumbe ni pigo kwa Watanzania.
“Enzi za uhai wake, mzee Jumbe alifanikiwa kuazisha mfumo wa
kuandikwa kwa Katiba ya Zanzibar pamoja na kuwakusanya wanasheria na
kutaka nchi kuendeshwa kwa mujibu wa sheria,” alisema.
Aboud alisema Serikali kwa kushirikiana na familia ya marehemu,
wametekeleza wosia ulioachwa na marehemu, aliyesema siku akifariki
asipigiwe mizinga na asizikwe kijeshi.
“Tumefanya mazishi haya kwa kutekeleza yale marehemu aliyoyaandika na
Serikali imeshirikiana kikamilifu na watoto wake ili kuhakikisha yale
yote aliyoyausia ndio tunayatekeleza.
“Tunashukuru tumekwenda vizuri tokea mwanzo hadi mwisho bila ya misukosuko yoyote,” aliongeza Aboud.
Katika mazishi hayo hakukuwapo na mizinga kama yanavyofanyika mazishi
mengine ya viongozi wakuu wa Serikali na jeneza lake lilibebwa kwa
kufunikwa kitambaa cha kawaida na si bendera ya taifa wala ya chama.
Wakati huo huo, Lowassa alipokuwa akimzungumzia marehemu Jumbe,
alisema Watanzania wamepata pigo kwa kuondokewa na kiongozi ambaye
alikuwa anajiamini.
“Watanzania tunatakiwa tujifunze kujiamini kutoka kwa marehemu wetu
huyu kwani alikuwa tayari kwa lolote katika mambo yake anayoyataka
katika uongozi wake.
“Ujasiri aliokuwa nao marehemu Alhaji Jumbe ni wa kipekee, kwa hiyo
Watanzania wanapaswa kumkumbuka kwa ushupavu wake,” alisema Lowassa.
Naye Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye,
alisema Tanzania imepoteza mwandishi wa siasa kwani enzi za uhai wake
aliandika vitabu vingi vyenye mwelekeo wa siasa.
“Watanzania hatuna utaratibu wa kusoma vitabu, lakini nakuombeni
tuvisome vitabu vya Alihaji Jumbe ili tuweze kujifunza kutoka kwake.
“Umahiri aliokuwanao katika kuandika vitabu vyake hasa vile vya
kisiasa ni nguzo kwa uongozi wa Tanzania na wananchi kama watavisoma na
kuvifanyia kazi,” alisema.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)

0 comments:
Post a Comment