Image
Image

Manji achefuka ajiuzulu yanga na 75% zake mfukoni.

MWENYEKITI wa Yanga, Yusuf Manji amejiuzulu wadhifa huo ndani ya klabu hiyo alioutumikia kwa takriban miezi miwili tangu aingie madarakani katika uchaguzi mkuu uliofanyika Juni 25 mwaka huu. Mbali na kujiuzulu uenyekiti, Manji pia amesitisha mpango wake wa kutaka kuikodi timu kwa miaka 10 kama alivyowaahidi wanachama katika mkutano wa dharura, takriban wiki mbili zilizopita.
Si Manji wala Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka Deusdedit aliyekuwa tayari kuzungumza na gazeti hili juu ya hilo mapema mchana jana, lakini walisikika wakizungumza kwenye kipindi cha michezo cha Radio E ambapo Baraka alisema mwenyekiti wao yupo safari huku Manji akigoma kuzungumza.
“Mwenyekiti yupo safari nje ya nchi lakini wanachama wajue tu kwamba mwenyekiti wa Yanga mpaka sasa ni Manji".
Kuhusu Manji alizungumza na redio hiyo na kugoma kutaja sababu za kujiuzulu zaidi ya kusisitiza kwamba hataki kuzungumza na yeyote.
Habari za uhakika kutoka kwa mmoja wa viongozi wa Yanga ambaye si msemaji wa klabu zinasema ni kweli mwenyekiti huyo ameamua kujiuzulu.
“Habari za mwenyekiti wetu ndio kama ulivyozisikia, hapa sasa sisi wenyewe (viongozi) hatuelewi la kufanya maana zimekuwa taarifa za ghafla mno kwetu,” alisema kiongozi mmoja ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini. “Tumeshangaa tu asubuhi kupata taarifa zake za kujiuzulu, na mpaka sasa hatujakutana naye, tumemfuata ofisini kwake hatukufanikiwa kumuona, tumempigia simu yake ya mkononi hataki kupokea, ameacha maagizo tu kwamba aachwe,” alisema mtoa habari hiyo.
Taarifa za Manji kujiuzulu zilianza kuzagaa tangu asubuhi ya jana na mwandishi wa gazeti hili alifika ofisini kwake Quality Plaza bila mafanikio.
“Bosi hayupo, ameondoka hapa tangu saa saba mchana na hata ukimsubiri huwezi kumuona maana kwanza leo hataki kuonana na yeyote,” alisema mmoja wa wahudumu wa ofisini kwa Manji kumjibu mwandishi aliyeomba kuonana na Manji baada ya kumpigia simu yake ya mkononi bila majibu.
Hata hivyo, taarifa zaidi zinasema kuwa Manji amefikia uamuzi huo kwa kile kinachodaiwa ni kuingiliwa mpango wake wa kutaka kukodi timu. Katika mkutano wake wa dharura na wanachama, Manji aliomba akodishiwe timu na nembo ya Yanga kwa miaka kumi na kwamba atatoa asilimia 25 ya faida kwa klabu na asilimia 75 atachukua yeye huku akisisitiza akipata hasara itakuwa yake.
Jambo ambalo lilikubaliwa na wanachama waliofika kwenye mkutano huo, huku mjumbe wa baraza la wadhamini la Yanga Francis Kifukwe akiahidi kulifikisha kwa viongozi wenzake kwa ajili ya kulijadili na kulitolea maamuzi.
“Sisi wenyewe tunasikia ameamua kuondoka uenyekiti na kusikitisha kukodisha timu baada ya watu kuingilia mpango huo halafu sasa linazungumzwa vibaya, nasikia baada ya baadhi ya viongozi wa serikali kulizungumzia hilo suala ndio ameamua kukaa pembeni,” alisema mtoa habari wetu ambaye ni mmoja wa viongozi wa Yanga.
Kitendo cha Manji kuondoka Yanga ni pigo kubwa kwa klabu hiyo hasa kipindi hiki ambacho inakwenda kwenye mabadiliko pamoja na mpinzani wake Simba inayotaka kumuuzia hisa mfanyabiashara Mohamed Dewji ‘Mo’.
Mo anataka kununua hisa asilimia 51 kwa Sh bilioni 20, hata hivyo suala hilo bado linajadiliwa na uongozi endapo apewe hisa hizo ama apunguziwe. Tayari wanachama wa Simba wameshaanza kuingia darasani kufundishwa jinsi soko la hisa lilivyo.
Hii si mara ya kwanza kwa Manji kusema anajiweka pembeni Yanga na kisha anarudi baada ya kuombwa na wanachama, takriban miaka mitatu iliyopita aliwahi kufanya hivyo, lakini alirudi baada ya wazee wa klabu hiyo kumuomba. Manji aliingia Yanga tangu mwaka 2006 kama mfadhili kabla ya kushika wadhifa wa mwenyekiti tangu mwaka 2012.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment