VIONGOZI wastaafu nchini wametakiwa kujitokeza kuwashauri viongozi
waliopo madarakani, kuhakikisha wanailinda na kuisimamia Katiba ya nchi
ili isivunjwe.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana,
Mwenyekiti wa Taasisi ya Wazalendo, Khamis Mgeja, alisema hivi sasa
Taifa linapita kwenye wakati mgumu tofauti na miaka 30 iliyopita, hivyo
ni muda mwafaka kwa marais wastaafu na viongozi mbalimbali kujitokeza
kukemea viashiria vya uvunjwaji wa Katiba.
Alisema kuna mambo yanaonesha Rais Dk. John Magufuli anakiuka Katiba,
hivyo ni wakati mwafaka kwa viongozi wastaafu kukemea jambo hilo,
vinginevyo Taifa litaelekea kubaya.
“Tulitegemea Rais Dk. Magufuli, ataisimamia Katiba ipasavyo na
kuilinda kama alivyoapa lakini kuna mambo anayafanya yanakiuka Katiba
huku akitambua hakuna aliye juu ya sheria. Jambo hili linahitaji
viongozi wastaafu kukemea kabla halijaota mizizi,” alisema Mgeja.
Alisema migogoro baina ya baadhi ya vyama vya siasa na Serikali ni
viashiria vibaya kwani wananchi wakishindwa kudai haki kwa mazungumzo,
wataandamana.
“ Tunaomba marais wastaafu akina Benjamin Mkapa, Ally Hassan Mwinyi,
Dk. Jakaya Kikwete na viongozi mbalimbali wastaafu na wa kidini
wahakikishe wanajitokeza kuisimamia Katiba ili isivunjwe vingine
historia itawahukumu kwa kushindwa kusimamia Katiba ikiwemo suala la
kuwaonya viongozi wanaoikiuka ,”alisema Mgeja.
Alisema ni vyema viongozi wastaafu wakaacha kusubiri mambo yaharibike
ndipo wajitokeze kinachotakiwa ni kushauri haki itendeke na
wasimfurahishe mtu kwa ukimya wao.
“ Nakumbuka Juni 14, mwaka 1995 Hayati baba wa Taifa Mwalimu Julius
Nyerere aliwahi kutamka kuna nyufa inahitajika kuzibwa ya kuchezea
Katiba na sheria ya vyama vya siasa kwa gharama yoyote ushirikiano
unahitajika huku akisisitiza rais aliyeapa kuilinda Katiba hiyo anapaswa
kuilinda na si kuionea aibu,” alisema Mgeja.
Alisema kiongozi yeyote atakayeona aibu kukemea vitendo vya uvunjwaji
sheria hafai kuwepo madarakani hivyo ni muda muafaka kwa viongozi
wastaafu kuiga mfano wa Nyerere.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)

0 comments:
Post a Comment