Na. Mtatiro J 1. Akidi ilitimia pande zote, Bara na Zanzibar
na mkutano ulimchagua Ndugu. Julius Mtatiro kwa kura takribani 500 kuwa
Mwenyekiti wa Kikao, alifuatiwa na Ndugu. Ridhiwani wa Morogoro
aliyekuwa na kura takribani 170 na hivyo ndugu Mtatiro alipitishwa rasmi
kuongoza mkutano.
2. Mkutano Mkuu kwa kauli moja ulipitisha
ajenda mbili: Moja ni Taarifa ya Barua ya Kujiuzulu kwa Prof. Lipumba na
mbili ni Uchaguzi wa Kujaza nafasi wazi za Mwenyekiti Taifa, Makamu
Mwenyekiti Taifa na Wajumbe wanne wa Baraza Kuu.
3. Mkutano Mkuu
ulianza ajenda ya kwanza chini ya Uenyekiti wa ndugu Mtatiro ambapo
Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad alipewa ruhusa ya kueleza
taarifa ya kujiuzulu kwa Prof. Lipumba na alieleza jambo hilo kwa kina,
hatua kwa hatua.
4. Baadhi ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CUF
wapatao 10 kutoka Tanzania Bara walitoa hoja zao kwa kutaka Kikao
kimuite Prof. Lipumba ili aje ajieleze kuhusu kujiuzulu kwake jambo
ambalo lilipingwa na wajumbe wengine. Mwenyekiti wa kikao aliwataka
wajumbe wanaotaka Lipumba aletwe waweze kueleza kifungu cha katiba au
kanuni kinachotaka Kiongozi aliyejiuzulu yeye mwenyewe aitwe kujieleza,
wajumbe hao walishindwa kutoa mamlaka ya kikatiba au kikanuni. Wajumbe
waliokataa Prof. Lipumba kuja mkutanoni walinukuu ibara ya 117(2) ambayo
inataka taarifa ya kujiuzulu kwake ndiyo ipelekwe kwenye mkutano mkuu
na siyo yeye mwenyewe. Mwenyekiti wa kikao aliujulisha mkutano kuwa
Prof. Lipumba si mjumbe wa kikao kwa hiyo hawezi kuitwa kwa sababu
yoyote ile na kwamba mkutano ujadili barua zake na ufanye maamuzi ya
kumrudisha au kutomrudisha.
5. Baadhi ya wajumbe wa mkutano mkuu
wa CUF kutoka Tanzania Bara walikataa Mkutano Mkuu usifanye maamuzi
yoyote. Wajumbe wengine wa Bara walitaka maamuzi yafanyike, kwa hiyo
Tanzania Bara iligawanyika nusu kwa nusu kwenye jambo hilo. Hofu ya
wajumbe wa Bara waliokataa maamuzi yasifanywe ilikuwa ni kuwa
yakifanyika yataathiri mipango yao.
6. Majira ya saa 8 mchana
wakati mkutano ukiendelea na baadhi ya wajumbe wa bara wakiomba mkutano
mkuu umuite Prof. Lipumba, ndipo Profesa alipojitokeza akiwa na kundi la
MABAUNSA wapatao 30 wakisindikizwa na Ofisa wa POLISI aliyekuwa na
RADIO CALL (Angalia picha ya ukurasa wa mbele gazeti la Mtanzania).
Kundi hilo liliwazidi nguvu walinzi wapatao 10 waliokuwa kwenye lango
kuu na hivyo Prof. Lipumba akaingia mkutanoni kwa nguvu na kuketi upande
mmoja na "genge" lake. Baadhi ya wajumbe wa bara wapatao 150 hivi kati
ya 320 waliohudhuria walisimama na kushangilia ujio wa Lipumba kwa
dakika kadhaa. Mwenyekiti wa Mkutano aliwatuliza
7. Mwenyekiti
wa Mkutano aliwajulisha wajumbe kwamba kwa hatua iliyopo lazima wafanye
uamuzi aidha wa kumrejeshea uenyekiti Lipumba au kumuondoa kabisa, kwa
kupiga kura. Wajumbe walewale takribani 150 wa Bara waliendelea kupinga
kitendo chochote cha kupiga kura, wakitaka mkutano mkuu umuidhinishe
Lipumba kurudi kwenye uenyekiti "kienyeji" na bila kutumia kura.
8. Mwenyekiti wa Mkutano alitoa OPTION ya pili kwamba Mkutano Mkuu uache
ajenda ya kwanza uhamie ajenda ya pili na kufanya uchaguzi wa Makamu
Mwenyekiti wa chama na ule wa wajumbe wanne wa baraza na kwamba Mjadala
juu ya Lipumba uahirishwe na pia uchaguzi wa nafasi ya Mwenyekiti
uahirishwe. Wajumbe wa bara walewale takribani 150 kati ya 320 walikataa
OPTION hii ya pili wakasimama na kupiga makelele kuwa Lipumba arudishwe
bila uamuzi wa kikatiba wa Ibara ya 112.
9. Mwenyekiti wa
Mkutano Ndg. Julius Mtatiro aliuahirisha mkutano kwa zaidi ya saa moja
ili wajumbe wakapate chakula. Katika muda huo wa mapumziko viongozi wa
kitaifa wa CUF waliwasiliana na viongozi wa jeshi la Polisi kuanzia
kanda, mkoa, wilaya ili kujua ni kwa nini polisi waliokuwepo walimruhusu
na kumsindikiza Lipumba ukumbini na kutaka kujua ni kwa nini
wanashindwa kumuondoa kwa sababu si mjumbe. Polisi walieleza kuwa wanao
ulinzi wa kutosha hapo hotelini na kwamba mkutano ukirejea wataimarisha
ulinzi na kuzuia makundi yoyote yasiyo wajumbe kuvamia mkutano kama
lilivyofanya kundi la Lipumba na watu wake. Polisi walikataa katakata
kumuondoa Lipumba na genge lake ukumbini.
10. Mkutano uliporejea,
Mwenyekiti wa kikao aliwaongoza wajumbe kufanya maamuzi ikiwa LIPUMBA
aondoke au abaki kwa mujibu wa katiba ya CUF ibara ya 117 (2). Wajumbe
takribani 150 wa bara walisimama na kupinga. Wajumbe takribani 130 wa
bara na wajumbe takribani 340 wa Zanzibar walipiga kura na kuamua kuwa
Lipumba AONDOKE RASMI. Jumla ya wajumbe waliomuondoa Lipumba ni kwa kura
zilizphesabiwa rasmi ni 476 huku waliosema ASIONDOKE wakiwa 14 tu.
Wajumbe takribani 150 hususani kutoka Tanzania Bara walikataa kushiriki
katika upigaji kura lakini wasingeliweza kuathiri akidi au maamuzi.
Baada ya uamuzi huo muhimu na ukilishwaji wa ajenda ya kwanza,
mwenyekiti wa kikao alikiahirisha kwa saa nzima.
11. Kikao
kiliporejea saa 1 jioni hivi, Mkutano Mkuu ulihamia kwenye ajenda ya
pili ya Uchaguzi wa Nafasi ya Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Wajumbe
wanne wa Baraza. Mwenyekiti wa kikao alimkaribisha Mwenyekiti wa
Uchaguzi wa ndani ya chama Wakili msomi Awadh Said akisaidiwa na Wakili
msomi Job Kralio ili waongoze shughuli uchaguzi. Wakili awadh alitoa
taarifa ya utangulizi akawatambulisha wajumbe wa kamati yake na
wakajipanga mbele ya wajumbe.
12. Wakati Wakili Awadhi
(Mwenyekiti wa Uchaguzi) akiendelea na zoezi lake, wajumbe wale 150 wa
Tanzania bara walisimama wakijaribu kuzuia uchaguzi usifanyike.
Mwenyekiti wa Mkutano Mkuu aliwatuliza na wakamsikiliza lakini ghafla,
milango mikuu ya Blue Pearl ilivamiwa na kundi la vijana zaidi ya 200
wakitokea nje, vijana hao wavamizi ambao kwa vyovyote vile lazima
walikuwa wamekodiwa kwa ajili hiyo, waliwazidi nguvu walinzi wetu wa
mlangoni wakaingia ukumbini.
13. Polisi kikosi kizima waliokuwepo
hawakufanya chochote baada ya hali hiyo, wameshuhudia makundi ya watu
wasio wajumbe wakiingia ukumbini na wamewaacha wafanye hivyo bila
kuwazuia. Viongozi wa Polisi waliokuwepo "walitorokea mlango wa pili"
immediatelly baada ya kundi la wahuni kuvamia.
Kundi lile lote
likawa limo ukumbini ukijumlisha na lile kundi la Lipumba na mabodigadi
wake wa kukodi. Kundi jipya la wavamizi mia mbili lilianza kuleta
vurumai kwa kupiga baadhi ya wajumbe wa mkutano mkuu (wajumbe kamwe
hawakupigana wao kwa wao, hata mara moja, walivamiwa kutoka nje na
wahuni na baadhi ya wajumbe kunyang'anywa viti na kupigwa au kutishiwa
kupigwa).
14. Kutokana na hali hiyo majira hayo kwa mamlaka ya
kikatiba aliyokuwa amepewa na Mkutano Mkuu, ndugu Julius Mtatiro
aliahirisha Mkutano Mkuu wa CUF hadi itakapotangazwa vinginevyo. Baada
ya kuuahirisha viongozi walilindwa na kuondoka mkutanoni kwa utaratibu
na wajumbe wa mkutano mkuu wakaongezewa ulinzi wa hoteli ili wawe
salama.
15. Kwa maoni yangu, pamoja na kuwa Prof. Lipumba ameamua
rasmi kuingia vitani na chama chake tena kwa malengo halisi ya AJENDA
NA MASLAHI YAKE BINAFSI, ukweli unabakia kuwa POLISI walikuwa ni sehemu
ya Mkakati wa kuuvuruga mkutano wa CUF. Kama Polisi wangelitoa ulinzi
kidogo tu, mkutano ungelifanyika na uchaguzi ungelifanyika hadi mwisho.
Lakini USALITI wa LIPUMBA akishirikiana na VYOMBO VYA DOLA unaweza kuwa
mzizi mkuu wa hali ya jana.
#Note 1: Leo nimeelezea kwa kirefu nini kilitokea mkutanoni jana. Kesho ntaeleza maoni yangu binafsi kwa ujumla.
Home
News
Slider
Mtatiro afunguka mambo 15 yaliyosababisha mkutano (CUF) kuvunjika jijini Dar es Salaam.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)


0 comments:
Post a Comment