Na: Abushehe Nondo - MAELEZO
Naibu
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi. Edwin A. Ngonyani
amelitaka gazeti la Mseto kumuomba radhi na kumlipa fidia ya shilingi
bilioni moja kutokana na kuandika habari ya kumchafua.
Akizungumza na
waandishi wa habari Ofisi kwake Waziri Ngonyani amesema kuwa Gazeti
hilo la tarehe 4 Agosti 2016 liliandika habari yenye kichwa cha Habari
“Waziri amchafua JPM” ikimuhusisha na upokeaji wa fedha kutoka moja ya
Kampuni ya Madini wakati akiwa Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Madini la
Taifa (Stamico).
“Nimewaandikia notisi ya siku saba ikiwataka waombe
radhi na kunilipa fidia, na wasipofanya hivyo hatua stahiki kuwapeleka
mahakamani akiwemo Mwandishi Josephat Isango, Mwanahalishi Publisher na
Mchapaji wa gazeti hilo”. Alisema Mhandisi Ngonyani.
Mhandisi
Ngonyani amesema kuwa habari hiyo siyo ya kweli na mwandishi ametumia
nyaraka za kughushi ikiwemo barua iliyoandikwa tarehe 24 Julai na
kutiwa saini yake akiwa Kaimu Mkurugenzi wa STAMICO wakati ukweli ni
kwamba tarehe hiyo yeye alikuwa ni Mkurugenzi kamili na siyo Kaimu kama
barua hiyo inavyosomeka.
Ameongeza kuwa habari hiyo imewachafua watu
wengi ikiwemo familia yake, wapiga kura wake wa jimbo la Namtumbo ambao
walijitoa katika kumsaidia wakati wa kampeni na hali kadhalika
zimemchafua Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kumhusisha na fedha
kutoka kwa wawekezaji wa nje kwa kuwaahidi kuwa mitaji yao nchini
itakuwa salama.
“Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli alishasema kama kuna
mfanyabiashara yeyote aliyechangia kuingia kwake ikulu ajitokeze na
hakuna aliyefanya hivyo, Iweje leo mtu tu anaibuka na kuandika habari za
kugushi? ”. Aliongeza.
Aidha Naibu Waziri huyo ametumia fursa hiyo
kuwataka waandishi wa habari nchini kuwa waangalifu pindi wanapoandika
habari za kutunga kwa kutotumia majina halisi kwani kufanya hivyo ni
kwenda kinyume na kanuni za uandishi wa hadithi (Habari za kutunga).
“Waandishi
wa habari mnatakiwa kufuata maadili ya kazi yenu kwa kuandika habari
zenye ukweli ili kuliepusha taifa kuingia katika machafuko na migogoro
isiyo ya lazima” Alisema Naibu waziri huyo.
Home
News
Slider
Ngonyani atoa Siku 7 kwa Gazeti la Mseto kumsafisha na kumlipa fidia ya shilingi bilioni moja.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)


0 comments:
Post a Comment