TAARIFA rasmi ya mwisho ya utekelezaji wa kuwaondoa watumishi hewa
serikalini na taasisi zake zote, itawasilishwa kwa Rais John Magufuli
Ijumaa wiki ijayo na kwamba hadi sasa wameshabainika watumishi hewa
16,127 na wameondolewa kwenye mfumo wa utumishi.
Aidha, mbali ya serikali kuokoa Sh bilioni 16.15 kwa mwezi huu wa
Agosti baada ya watumishi hewa hao kuondolewa kwenye mfumo wa utumishi,
ambao kama wasingeondolewa fedha hizo zilikuwa ziwalipe mshahara, posho
na malipo mengine, waajiri 145 hawajawasilisha taarifa kuhusu uhakiki
wao.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki alipozungumza na
waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuhusu utekelezaji wa
agizo la Rais Magufuli la kuwataka waajiri wote wa umma na serikali,
kuwaondoa watumishi hewa.
Akifafanua taarifa hiyo, Kairuki alisema Agosti 26, mwaka huu
watamkabidhi rais taarifa rasmi ya utekelezaji wa agizo hilo huku
akiwataka waajiri 145 ambao hawajawasilisha taarifa za ama uwepo wa
watumishi hewa au la, kuhakikisha wanaziwasilisha taarifa hizo kabla ya
Ijumaa wiki ijayo.
“Tunawapa muda hadi Ijumaa wiki ijayo wawe wamewasilisha taarifa za
kama wana watumishi hewa au la na sisi Agosti 26, mwaka huu ndio
tunamkabidhi rais taarifa rasmi ya mwisho ya utekelezaji wa agizo
alilotoa,” alisema Kairuki akizungumzia hatua ya Rais Magufuli kuagiza
uhakiki huo Machi mwaka huu.
Akielezea hatua zilizochukuliwa hadi sasa na waajiri hao, Kairuki
alisema nchi ina jumla ya waajiri 409 wa serikali na taasisi mbalimbali
za umma, na kati ya waajiri hao, hadi sasa waajiri 264 ndio
waliowasilisha taarifa za utekelezaji wa agizo hilo.
Alisema kati ya waajiri hao 264 waliowasilisha, waajiri 63
wamethibitisha hawana watumishi hewa, huku waajiri 201 wakibaini uwepo
wa watumishi hewa kuanzia mmoja na kuendelea.
“Tumepokea taarifa za utekelezaji wa agizo la rais alilitoa Machi 15,
mwaka huu na hadi sasa waajiri 264 kati waliotekeleza agizo hilo, 201
wamebaini wana watumishi hewa,” alisema Kairuki.
Akizungumzia hatua zitakazochukuliwa baada ya kufikia tarehe ya
mwisho wa kupeleka taarifa hizo, Kairuki alisema jukumu lao ni kuzipokea
na kukabidhi mamlaka ya uteuzi ambayo ndiyo iliagiza na ambayo ndiyo
itaamua hatua za kuchukua.
Sambamba na hilo, Kairuki alisema hadi sasa jumla ya watumishi hewa
606, wameanza kuchukuliwa hatua za kisheria, ikiwemo mashauri yao
kupelekwa polisi na hivi sasa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa
(Takukuru), wanafanya uchunguzi na hatimaye watuhumiwa hao wafikishwe
kwenye vyombo vya juu vya sheria.
Aidha, maofisa utumishi 233 waliohusika kwenye malipo ya mishahara
hewa mashauri yao, wamefikishwa kwenye mamlaka husika kwa uchunguzi,
ilhali watatu wamefukuzwa kazi, huku wizara ikiendelea kufanya uchunguzi
kwenye taasisi 75 za umma ili kujiridhisha kuhusu suala la watumishi
hewa.
Kuhusu waajiri 145 ambao hawajawasilisha taarifa za uhakiki wa
watumishi wao, Kairuki alisema zimo taasisi, wakala, bodi, mabaraza,
vyuo, hospitali, ofisi za Makatibu Tawala wa Mikoa, tume na mamlaka
kadhaa ambazo hazijawasilisha taarifa zao.
Kwa upande wa mabaraza nchini, Kairuki alisema mabaraza mbalimbali 10
hayajawasilisha taarifa za uhakiki wa watumishi na baadhi yao ni kama
vile Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC), Baraza la Elimu ya Ufundi
(Nacte), Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), Baraza la Mitihani la Taifa
(NECTA) na Baraza la Michezo la Taifa (BMT).
Aidha, jumla ya vyuo vya umma 25 nchini havijawasilisha taarifa zao
za uhakiki wa watumishi hewa na baadhi yao ni Dodoma (Udom), Chuo KIkuu
Huria (OUT), Chuo Kikuu Mzumbe, Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi
Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Chuo cha Diplomasia, Chuo Kikuu cha Elimu
Dar es Salaam (Duce), Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) na Chuo cha
Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere na Chuo Cha Taifa cha Usafirishaji (NIT).
Upande wa Bodi mbalimbali ambazo hazijawasilisha taarifa zao jumla
yake ni 10 na baadhi ya bodi hizo ni pamoja na Bodi ya Korosho Tanzania,
Bodi ya Tumbaku, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) na
Bodi ya Utalii na Bodi ya Maziwa.
Pia zimo hospitali teule za rufaa tatu ambazo ni Hospitali ya CCBRT,
Hospitali ya Rufaa Bugando na Hospitali ya Rufaa KCMC na kwamba katika
hospitali kama hizo zilizowasilisha taarifa zake, wamebainika na
kuondolewa watumishi hewa 4,000.
Kwenye taasisi za Umma na Wakala ambazo hazijawasilisha taarifa zao
jumla ziko 30 na baadhi yao ni Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Mfuko
wa Pembejeo za Kilimo, Makumbusho ya Taifa, Shirika la Utangazaji la
Taifa (TBC), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Shirika la Madini la
Taifa (Stamico), Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), Wakala wa
Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC).
Pia zipo Ofisi za Makatibu Tawala wa Mikoa 12 ambazo baadhi yake ni
Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Dodoma, Dar es Salam, Mbeya,
Pwani na Kagera; kwa upande wa mamlaka zipo sita ambazo ni Mamlaka ya
Elimu Tanzania (TEA), Mamlaka ya Maeneo Maalumu ya Uwekezaji kwa Mauzo
ya Nje (EPZA), Mamlaka ya Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA)
na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA).
Aidha, zipo tume 10 ambazo hazijawasilisha taarifa zake na baadhi
yake ni Tume ya Pamoja ya Fedha, Tume ya Atomiki, Tume ya Elimu Taifa,
Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya, Tume ya Sayansi na Teknolojia
Tanzania na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU).
Pia zipo Mamlaka za Serikali za Mitaa 38 zikiwemo Halmashauri ya Jiji
la Mwanza, Manispaa ya Iringa, Nyamagana, Halmashauri ya Mji, Kasulu,
Halmashauri ya Wilaya ya Dodoma na Halmashauri ya Wilaya ya Misenyi.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)


0 comments:
Post a Comment