WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewataka wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa
halmashauri nchini kuwachukulia hatua watumishi wote wa sekta ya afya
wanaojihusisha na wizi wa dawa.
“Fuatilieni na kuwachukulia hatua
watumishi wa Zahanati wanaoiba dawa. Hawa hawana nafasi ya kuendelea
kufanya kazi kwa sababu ni wauaji,” alisema.
Waziri Mkuu ametoa
agizo hilo juzi jioni (Jumamosi, Agosti 20, 2016) wakati akipokea
taarifa ya mkoa wa Katavi mara baada ya kuwasili mkoani hapa kwa ziara
ya kikazi ya siku tatu.
Alisema kila kiongozi kwenye eneo lake
ahakikishe dawa zinazopelekwa na Serikali kwa ajili ya kuwahudumia
wananchi zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa. Pia ameitaka Bohari Kuu
ya Dawa (MSD) kujenga duka la dawa mkoani Katavi kwa ajili ya
kurahisisha upatikanaji wa dawa katika mkoa huu pamoja na mikoa jirani.
Wakati
huo huo Waziri Mkuu aliwataka Waratibu wa Elimu katika ngazi ya Kata na
Wakuu wa shule za sekondari wasiokuwa na shahada waende wakasome kama
wanahitaji kuendelea kuwa na wadhifa huo.
Alisema Mratibu wa Elimu
katika ngazi ya Kata ni lazima awe na shahada ili aweze kutekeleza
majukumu yake ya kusimamia utolewaji wa elimu katika shule za sekondari
na msingi.
Kwa upande wa walimu wakuu katika shule za msingi, Waziri
Mkuu alisema ni lazima wawe na diploma, hivyo aliwataka walimu wakuu
wote wasiokuwa na diploma kwenda kusoma kabla hawajaondolewa kwenye
wadhifa huo.
Alisema Serikali imetenga zaidi ya sh. bilioni tano kwa
mwezi ambazo ni posho ya madaraka, ambapo Waratibu Elimu Kata wanapewa
sh 250,000 kwa mwezi huku Wakuu wa shule za sekondari na walimu wakuu
katika shule za msingi wanapewa sh. 200,000.
Awali Mkuu wa Mkoa wa
Katavi Meja Jenerali (Mstaafu) Raphael Muhuga alisema mkoa umeendelea
kuongeza bajeti ya dawa ili kuhakikisha dawa zinapatikana katika ngazi
zote za kutolea huduma.
“Mwaka 2012 bajeti ya dawa na vifaa tiba
ilikuwa sh. Milioni 558 ambayo ilitosheleza upatikanaji wa dawa na vifaa
tiba kwa asilimia 70. Katika bajeti ya mwaka 2016/2017 mkoa umetengewa
jumla ya sh bilioni 1.3 ambayo tunaamini itamaliza tatizo la upatikanaji
wa dawa na vifaa tiba,” alisema.
Mkuu huyo wa mkoa alisema mfumo
mpya wa usambazaji dawa kupitia MSD umesaidia dawa, vifaa tiba na
vitendanishi kupelekwa moja kwa moja hadi katika ngazi ya zahanati hali
iliyosaidia dawa kufika kwenye vituo vya kutolea huduma kwa asilimia
100.
Mapema jana Waziri Mkuu alifanya ziara katika hospitali ya
Manispaa ya Mpanda ambapo alisema Serikali itahakikisha hospitali hiyo
inaongezewa huduma zaidi kwa sababu ni ya wilaya ila inahudumia wagonjwa
wa mkoa wote.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)


0 comments:
Post a Comment