JUMATATU na Jumatano wiki hii zimeweka Watanzania katika hali ya
majonzi na taharuki kubwa kutokana na ajali mbili za barabarani,
zilizotokea mkoani Njombe Kusini mwa Tanzania na Mwanza katika Kanda ya
Ziwa.
Katika muda saa zipatazo 48 tu, tulipoteza maisha ya jumla ya
Watanzania 25 na wengine zaidi ya 40 wakiachwa majeruhi katika ajali
hizo mbili, zilizohusisha mabasi mawili na gari dogo moja.
Ajali ya Jumatatu ilitokea eneo la Lilombwe wilayani Njombe katika
mkoa wa Njombe majira ya saa 1.40 usiku, iliyohusisha basi la New Force
lililokuwa linasafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Songea mkoani Ruvuma.
Sababu ya ajali hiyo, ilielezwa na mashuhuda kuwa ni mwendo kasi.
Nayo ajali ya pili ilitokea jana majira ya saa 12.15 asubuhi,
ikihusisha basi la abiria la Super Shem na gari dogo la abiria,
zilizogongana katika eneo la Mwamanya wilayani Kwimba katika mkoa wa
Mwanza huku basi kubwa likiwa linatoka mkoani Mbeya kwenda jijini Mwanza
na basi dogo likitokea kijiji cha Shirima wilayani Kwimba kwenda jijini
humo pia.
Sababu iliyotolewa kwa ajali hiyo ya Mwanza ni kwamba dereva wa basi
hilo dogo, aliingia barabara kuu bila kuwa mwangalifu na hatimaye
kukumbana na basi hilo kubwa na kusababisha maafa hayo.
Upo msemo maarufu usemao ' Ajali haina kinga'. Lakini ni ukweli pia
kwamba kama madereva wa mabasi na gari gari hilo dogo, wangefuata sheria
na taratibu za usalama barabarani, huenda tusingepoteza maisha ya
wenzetu hao na kuwatumbukiza wengine kwenye janga la kujeruhiwa.
Kwa bahati mbaya pia, ajali zote mbili zimetokea wakati tunaadhimisha
Wiki ya Usalama Barabarani. Hivi inakuwaje dereva uliyefundishwa ukiwa
na akili timamu, unaliingiza gari lako kwenye barabara kuu bila kusimama
na kuhakikisha kwamba hakuna gari au chombo kingine; au hata abiria
kabla hujaingia moja kwa moja barabara kuu?
Kama ulisomea kweli kazi hiyo na kufuzi vilivyo, unahitaji mafunzo ya ziada gani kuhusu suala hilo muhimu kulifahamu?
Katika ajali ya mkoani Njombe, hali ilikuwa ya kushangaza zaidi.
Abiria walionusurika walieleza wazi kwamba kabla ya ajali hiyo kutokea,
walinusurika kupinduka mara mbili kutokana na mwendo kasi wa dereva wa
basi hilo.
Hivi inakuwaje abiria wote zaidi ya 50, wasichukue hatua ya
kumdhibiti dereva husika na msaidizi wake kwa kuwashinikiza wasimamishe
basi na kutafuta msaada wa polisi wa usalama barabarani, awanusuru kwa
kutafuta ufumbuzi wa hatari inayowakabili?
Tunapenda kutoa mwito maalumu kwa abiria wote, wanaosafiri kwa mabasi
ya abiria, kuchukua hatua za makusudi kabla ya kuingia kwenye mabasi
hayo, kuhakikisha wanapeana namba ya kuwasiliana na polisi wa usalama
barabarani ili wakipatwa na dereva wa aina hiyo, mwenye 'pepo' wa mwendo
kasi, aripotiwe polisi.
Lakini pia abiria ambao naamini ni wengi kuliko dereva na wasaidizi
wake, wasikubali kuendelea na safari hadi apatikane dereva mwingine,
atakayefuata matakwa ya mwendo wa abiria ulio salama. Kinyume chake,
tutaendelea kuuawa na madereva wazembe kama hao na kuendelea kutuachia
yatima na vilema.
Hali hii sasa tuikatae, kwa abiria kushirikiana kwa vitendo na askari
wetu wa usalama barabarani na kuwakataa kwa vitendo madereva wa aina
hiyo. Sasa tuseme basi inatosha.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment