Image
Image

Bil. 100/- zilizoyeyuka Tamisemi pasua kichwa



KIU ya kujua zilipo Sh. bilioni 100 ambazo Hazina iliipa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa -Tamisemi (wakati huo ikiwa chini ya ofisi ya Waziri Mkuu 2014/15), huenda isikatwe kama ambavyo wengi walitarajia.

Septemba mosi, mwaka huu, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ilipokuwa ikipitia hesabu za Tamisemi kwa mwaka wa fedha 2014/15, ilibaini miamala isiyo ya kawaida kati ya Tamisemi na Hazina, ambapo Sh. bilioni 100.5 zilikuwa hazina maelezo ya kutosha juu ya zilipo huku Tamisemi ikisema zilirudishwa hazina nao hazina wakisema hakuna fedha iliyorudi kwao.
Katika kikao hicho, mjumbe wa PAC, Joseph Kakunda, wakati akipitia ripoti ya Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu hesabu za wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2014/15, alibaini vitabu vya hesabu za Tamisemi zinaonyesha ilipewa Sh. bilioni 286 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kwamba asilimia 99.9 ya fedha hizo zilitumika.

Hata hivyo, Kakunda ambaye pia ni Mbunge wa Sikonge (CCM), alisema hesabu hizo zilikuwa zinajichanganya kutokana na kuonyesha kwamba kati ya fedha hizo za maendeleo zilizotolewa na Hazina, Sh. bilioni 100.5 zilirudishwa kwenye mfuko mkuu huo wa serikali bila kutoa taarifa kwa Tamisemi.
Alifafanua kuwa kama Sh. bilioni 100.5 zilichukuliwa na Hazina, ina maana kwamba fedha zilizotumika ni Sh. bilioni 185.5 ambayo ni sawa na asilimia 53 ya fungu lote lililokuwa limetengwa kwa ajili ya wizara hiyo na siyo 99 kama inavyoonekana kwenye vitabu vya wizara hiyo vilivyowasilishwa mbele ya PAC mjini hapa siku hiyo.
"Kwa maana hiyo, miradi ya maendeleo ambayo ni pamoja na elimu, afya na barabara ambayo ilikuwa inategemea fedha hizo haikufanyika, na hapa tuna taarifa ambayo imetoka Hazina inasema wao walishatoa hizo fedha zote na zimetumika," alisema Kakunda.
Mbunge huyo aliendelea kueleza kuwa kukinzana kwa taariza za Hazina na Tamisemi ni ishara ya kuchukuliwa kinyemela kwa kiasi hicho cha fedha kwa kuwa taratibu za Wizara ya Fedha na Mipango zinaelekeza kuwa kabla ya kutolewa kwa fedha na Hazina, kuna kamati maalum ambayo ni lazima ikae na kubariki kuzitoa.
Alisema kama Hazina inataka kupanga matumizi mengine kwa fedha ambazo tayari zimeshatolewa, kamati hiyo hukaa tena ili kubadilisha matumizi yake, jambo ambalo halikufanyika katika kuchukuliwa kwa Sh. bilioni 100.5 za Tamisemi.
Akijibu hoja za PAC siku hiyo, Katibu Mkuu wa Tamisemi, Musa Iyombe, alisema alipoanza majukumu yake kwenye wizara hiyo, alielezwa kwamba fedha hizo zilitolewa na Hazina na baada ya muda zikachukuliwa tena na Hazina wenyewe.
Alisema baada ya hapo, alianza kuwa anawaandikia Hazina barua ili watoe fedha hizo, lakini hawajajibu hata moja.
"Hawajibu barua hata moja, lakini wamekuwa wakirudisha fedha kidogokidogo, mara ya kwanza walileta Sh. bilioni saba na mara ya pili wakaleta Sh. bilioni 10, kwa hiyo sasa tunawadai Sh. bilioni 83," alisema Iyombe.
Kutokana na majibu hayo, Kakunda alihoji utaratibu unaotumiwa na Hazina kuzirudisha Tamisemi fedha hizo kidogokidogo ilhali taarifa waliyoiwasilisha bungeni inasema mfuko mkuu huo wa serikali ulishatoa fedha na zikatumika.
Akichangia hoja hiyo, Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki (CCM), Omary Mgumba, alisema kinachooneka kwenye hesabu za Tamisemi ni kwamba fedha hizo ziliingia na kutolewa na watu wachache ambao sasa wanafanya biashara na kuzirejesha kidogo kidogo baada ya kupata faida.
Naye Mbunge wa Vwawa (CCM), Japhet Hasunga, alihoji: "Hoja yetu hapa ni fedha hizo baada ya kurudishwa Hazina zilienda wapi?"
Wajumbe wa PAC pia walihoji sababu za Hazina kutotaka kujibu barua za Tamisemi na kueleza kuwa ni eneo jingine linaloongeza wasiwasi.
Kutokana na suala hilo kuibua maswali mengi yasiyokuwa na majibu, wajumbe wa kamati hiyo walikubaliana na Tamisemi warudishwe wakajipange kwa siku sita ili Septemba 7, warejee kwenye ofisi za bunge wakiwa na majibu ya uhakika kuhusu kufanyika kwa muamala huo wa uchepushaji wa kiasi hicho cha fedha kinyume cha sheria.
Hata hivyo, katika mahojiano na Nipashe kwenye ofisi za bunge mjini hapa mwishoni mwa wiki, Makamu Mwenyekiti wa PAC, Aeshi Hilaly, alisema wizara hiyo bado haijawapa taarifa kuhusu uchepushaji huo.
"Kamati iliiona kuna utofauti mkubwa, ikaona CAG mwenyewe aje aone ripoti zao zinavyokinzana na ripoti zake," alisema Aeshi.
"Baada ya kuwaambia waje Septemba, yapo mambo mawili yaliyojitokeza. Kwanza, kuna taasisi zingine mbali na hiyo wizara (Tamisemi) ambazo nazo tuliagiza zirejee hapa bungeni siku hiyo, lakini ili tuzihoji zinahitaji idhini ya Msajili wa Hazina ambaye alituomba tusipate muda zaidi ziitishe vikao vya bodi na kuandaa taarifa mpya tunayoitaka.
"Pili, tulipowaagiza Tamisemi warejee Septemba 7, hatukupata muda tena wa kukaa kama kamati kupitia taarifa yao maana muda wa kamati kukutana ulikuwa umekwisha, tulipewa muda wa wiki tatu tu na uongozi wa bunge kuzihoji taasisi mbalimbali. Taarifa yao nyingine bado sijaipata.
"Tutakapoita kamati kwa ajili ya kuandaa ripoti zetu kwa ajili ya kuwasilisha bungeni katika mkutano ujao wa bunge utakaofanyika Novemba, ndipo tutawaita wote kuja kuwahoji tena."
VIFO VYA UZAZI
Wakati PAC ikiendelea kuwasaka waliochepusha fedha hizo, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni zimebainisha changamoto kadhaa za kiafya na elimu zinazopaswa kutatuliwa na Tamisemi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Peter Serukamba, wakati wa mjadala wa makadirio ya bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2016/17 mjini hapa mwaka huu alisema Tanzania sasa ina kata 38,000, hivyo kunapaswa kuwa na vituo vya afya 38,000, lakini kamati yake imebaini vituo vya afya vilivyopo nchini kwa sasa ni 716 tu, sawa na asilimia 18.8 ya mahitaji ya kisera.
Kati ya vituo hivyo, Serukamba alisema serikali inavimiliki 484, mashirika ya dini yana vituo 141 wakati vituo vya afya binafsi ni 79 na vya taasisi viko 12.
AJIRA SEKTA YA AFYA
Serukamba ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CCM), alisema nchi inakabiliwa na uhaba wa wataalamu wa afya, lakini serikali katika mwaka huu wa fedha imetoa kibali cha kuajiri wataalamu 10,000 kati ya 30,000 waliohitimu mafunzo, sawa na theluthi moja ya wataalamu waliopo ambao hawajaajiriwa.

ONGEZEKO LA WATU
Huku Sh. bilioni 100.5 zikichepushwa kutoka Tamisemi, Serukamba alisema kamati yake inaishauri serikali kutenga bajeti ya kutoa elimu ya uzazi wa mpango ili kudhibiti ongezeko la watu nchini.

Alisema hadi kufikia 2100, Tanzania itakuwa nchi ya saba duniani na ya pili barani Afrika kwa kuwa na idadi kubwa ya watu kwa kuwa takribani watu milioni moja huongezeka kila mwaka, sawa na uzazi wa watoto watano kwa kila mwanamke aliye katika umri wa kuzaa.
Kadhalika, wakati PAC inaendelea kuwasaka waliochepusha Sh. bilioni 100.5 kutoka kwenye akaunti za Tamisemi, Serukamba pia aliishauri serikali kuhakikisha watoto wenye chini ya miaka mitano, wazee na wajawazito ambao ni zaidi ya asilimia 70 ya wananchi wote, wanatiwa bima ya afya kuwawezesha kupatiwa huduma za afya zenye uhakika.
Kuchepushwa kwa mabilioni hayo ya shilingi pia kumetokea katika kipindi ambacho takwimu za Benki ya Dunia (WB) zinaonyesha Tanzania ina vifo 42 kila siku vinavyotokana na uzazi.
Mei 11, mwaka huu, Dk. Godwin Mollel, Mbunge wa Siha (Chadema), wakati akiwasilisha bungeni maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu makadirio ya bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2016/17, alisema hali ya vifo vinavyotokana na uzazi nchini inatisha.
Akinukuu ripoti ya WB iliyotolewa mwanzoni mwa mwaka huu, Dk. Mollel alisema kina mama 1,255 nchini hufariki dunia kila mwezi kutokana na uzazi, sawa na kina mama 42 kila siku na kina mama wawili kila saa.
"Kama ukiwakusanya kina mama wanaofariki kutokana na uzazi kila siku, ni sawa na abiria wa basi dogo aina ya Costa," alifafanua Dk. Mollel.
BAA VIFO VYA UTAPIAMLO
Uchepushaji wa mabilioni hayo ya shilingi pia umefanyika katika kipindi ambacho Tamisemi inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa chakula na lishe duni nchini inayoathiri familia nyingi hasa watoto chini ya umri wa miaka mitano.

Akinukuu utafiti wa Taasisi ya Afya Ifakara siku hiyo, Dk. Mollel alisema mtoto mmoja nchini hufariki dunia kila dakika 12 kutokana na utapiamlo.
Alisema utafiti huo unabainisha kuwa zaidi ya watoto milioni 2.5 nchini wamedumaa na takribani 430,000 ni miongoni mwa walio katika hatari ya kufariki kila mwaka ikiwa hatua za haraka zisipochukuliwa.
Aidha, msomi huyo alisema takwimu za Shirika la Utafiti la Twaweza zinaonyesha Tanzania sasa ni nchi ya 10 duniani kwa ukubwa wa changamoto hiyo, akiilinganisha pia na nchi za Ethiopia inayoshika nafasi ya saba na Sudan Kusini (15) ambazo zimekuwa zikikumbwa na mabaa ya njaa mara kwa mara.
DENI LA MSD
Ufisadi huo pia umefanyika wakati ambao Bohari ya Dawa (MSD) inaidai serikali Sh. bilioni 131 na kusababisha uhaba wa dawa, vitendanishi na kinga katika hospitali za umma.

"Serikali imetenga Sh. bilioni 108 kulipa deni hilo (katika mwaka huu wa fedha), hivyo kubakiza deni la Sh. bilioni 23. Kiasi hiki kilichotengwa kinakidhi mahitaji ya MSD kwa miezi minne tu. Je, serikali inataka dawa na vifaa tiba viozee kwenye bohari na bandarini kwa miezi mingine kama ilivyotokea hivi karibuni?" Alihoji Dk. Mollel.
DENI LA TTCL
Kuchepushwa kwa Sh. bilioni 100.5 kutoka akaunti za Tamisemi pia kumetokea katika kipindi ambacho baadhi ya taasisi, ikiwamo wizara hiyo, zinadaiwa mabilioni ya shilingi na Kampuni ya Mawasilino ya Simu Tanzania (TTCL).

Agosti 31, mwaka huu, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu ilipitia hesabu za kampuni hiyo mjini hapa na kubaini inaidai serikali Sh. bilioni 9.3.
Makamu mwenyekiti wa kamati hiyo, Moshi Kakoso, alisema watalishauri Bunge lisipitishe bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano katika mwaka ujao wa fedha ikiwa serikali itashindwa kulipa deni inalodaiwa na kampuni hiyo.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Dk. Kamugisha Kazaura, alisema siku hiyo kuwa hadi Juni 30, mwaka huu, walikuwa wanaidai serikali Sh. bilioni 9.3, ikiwa ni malipo ya huduma walizotoa kwa idara na taasisi mbalimbali.
Alizitaja baadhi ya taasisi hizo kuwa ni pamoja na Jeshi la Polisi ambalo alisema linadaiwa zaidi ya Sh. bilioni 2.7, Tamisemi Sh. bilioni 1.4, Tanroads Sh. milioni 807, Wizara ya Fedha na Mipango Sh. milioni 371, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) Sh. milioni 335, Idara ya Uhamiaji Sh. milioni 332, Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi Sh. milioni 209, Shirika la Reli Tanzania (TRL) Sh. milioni 179 na Shirika la Ndege Tanzania (ATC) Sh. milioni 178.
HALI YA ELIMU INATISHA
Ufisadi wa Sh. bilioni 100.5 za Tamisemi pia umeripotiwa wakati ambao hali ya elimu nchini inatisha huku Rais John Magufuli na Bunge wakilazimika kuanzisha mkakati maalum wa kusaka fedha kwa ajili ya kuzinunulia madawati shule za msingi na sekondari ambazo nyingi ziko katika hali mbaya kimiundombinu.

Mei 26, mwaka huu wakati akichangia mjadala wa makadirio ya bajeti ya serikali katika mwaka huu wa fedha, Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe, alisema hali ya elimu nchini inatisha na ni hatari kwa uhai na usalama wa taifa.
Alisema uwezo wa watoto kujifunza kusoma na kuhesabu ni mdogo. Pia miundombinu ya kusomea kama madarasa, mabweni na vyoo bado haitoshi na iliyopo, mingi iko katika hali mbaya.
Ili kutatua changamoto hiyo, Bashe alisema serikali inapaswa kuandaa mpango mkakati wa haraka wa kuhakikisha inatenga bajeti maalum ya kuwezesha miundombinu na idadi ya walimu iongezwe kukabiliana na changamoto ya ongezeko la wanafunzi.
MAABARA SEKONDARI
Uchepushaji wa mabilioni ya Tamisemi umefanyika pia katika kipindi ambacho serikali inakabiliwa na changamoto ya kuhakikisha shule zote za sekondari nchini zinakuwa na vifaa vya maabara na vitabu vya kutosha.

Mei 26, mwaka huu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknojia na Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako, aliiambia Bunge mjini hapa kuwa wizara yake kwa kushirikiana na Tamisemi, inajipanga kununua vifaa vya maabara kwa awamu tatu kuanzia mwaka huu wa fedha.
Prof. Ndalichako pia alisema wameandaa mpango wa ukarabati wa shule kongwe za sekondari nchini na kwamba katika awamu ya kwanza, shule 33 zitakarabatiwa.
Alizitaja shule zilizo kwenye mpango wa kukarabatiwa kuwa ni pamoja na Ihungo, Iliboru, Kilakara, Mwenge, Msalato, Mzumbe, Ngaza, Pugu, Same, Tabora Boys na Tabora Girls.
Zingine ni Azania, Jangwani, Kantalamba, Mpwapwa, Tosamaganga, Malangali, Milambo, Nangwa, Kibiti, Minaki, Ifakara, Songea Boys, Ndanda, Kigoma, Kibaha na shule za ufundi za Bwiru Boys, Ifunda, Iyunga, Moshi, Mtwara, Musoma na Tanga.
"Mazingira ya kufundishia na kujifunzia yana mchango mkubwa katika kuinua ubora wa elimu katika ngazi zote," alisema Prof. Ndalichako.
Mbali na ukarabati wa shule kongwe, waziri huyo alisema serikali kupitia mamlaka ya elimu, itaendelea na uimarishaji wa miundombinu ya shule na vyuo vya ualimu ikiwamo ujenzi wa nyuma za walimu 30 zenye uwezo wa kuchukua walimu 180 katika maeneo yasiyofikiwa kwa urahisi.
Alisema pia watajenga vyumba 25 vya madarasa na matundu 200 ya vyoo katika shule zenye uhitaji mkubwa wa miundombinu hiyo.
Source:Nipashe.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment